LHRC YAADHIMISHA MIAKA 20 TANGU KUANZISHWA KWAKE SEPTEMBA 26, 1995
Mgeni rasmi katika Maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Septemba 26,1995, Jaji Mstaafu Osebia Munuo (katikati), akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kitabu cha maadhimisho ya miaka 20 cha LHRC yaliyofanyika Makao Makuu ya LHRC Kijitonyama Dar es Salaam jana. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya LHRC, Geoffrey Mmari na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk.Helen Kijo-Bisimba.
Mgeni rasmi katika Maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jaji Mstaafu Osebia Munuo (kushoto), akikata keki maalumu ya Maadhimisho ya miaka 20 cha LHRC yaliyofanyika Makao Makuu ya LHRC Kijitonyama Dar es Salaam jana. Anayeshuhudia kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya LHRC, Geoffrey Mmari na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk.Helen Kijo-Bisimba.
Wimbo wa taifa ukiimbwa kabla ya kuanza maadhimisho hayo.
Waimbaji wa Kwaya ya LHRC ya Mwalusanya wakiimba wa wimbo wa Taifa.
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Kwaya ya LHRC ya Mwalusanya ikifanya vitu vyake katika maadhimisho hayo.
Hapa ni Kwaya ya Mwalusanya ikiserebuka kwa kwenda mbele. 'Jamaa wa mbele kushoto yupo vizuri kiuchezaji chezea maadhimisho ya miaka 20 ya LHRC wewe'
Mwenyekiti wa Bodi ya LHRC, Geoffrey Mmari (katikati), akitoa hutuba fupi katika maadhimisho hayo. Kulia ni Mwakilishi kutoka Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Rehema Ntimizi na kushoto ni Mgeni rasmi wa hafla hiyo, Jaji Mstaafu, Osebia Munuo.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk.Helen Kijo-Bisimba (katikati), akisoma hutuba yake ya maadhimisho hayo. Kushoto ni Mjumbe wa LHRC, Emeliana Mboye.
Meza Kuu ikionesha Kitabu cha Maadhimisho ya Miaka 20 tangu kuanzishwa LHRC baada ya kuzinduliwa kwenye hafla hiyo. Kutoka kushoto ni Mdau wa LHRC, Profesa Chris Peter, Mjumbe wa LHRC, Emeliana Mboye, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk.Helen Kijo-Bisimba, Mgeni rasmi wa hafla hiyo, Jaji mstaafu, Osebia Munuo, Mwenyekiti wa Bodi LHRC, Geoffrey Mmari na Mwakilishi kutoka Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Rehema Ntimizi.
Mdau wa masuala ya haki za binadamu, Ally Said Mwashongo akichangia jambo kwenye hafla hiyo.
Mgeni rasmi Jaji Osebia Munuo akisoma hutuba yake.
Wadau wakisoma kitabu hicho baada ya kuzinduliwa.
Wasanii wakicheza ngoma ya Mganda kwenye uzinduzi huo.
Na Dotto Mwaibale
MATUKIO ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanayofanywa na vyombo vya dola hususan jeshi la polisi hapa nchini yameongeza kufikia asilimia 60 imefahamika.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo -Bisimba Dar es Salaam jana katika sherehe za maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa LHRC Septemba 26, 1995.
"Matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu kwa vyombo vya dola bado yapo juu ingawa uelewa kwa wananchi kuhusu haki za binadamu ni mkubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma wakati tunaanzisha LHRC" alisema Dk. Bisimba.
Alisema baadhi ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanayofanywa na jeshi la polisi ni pamoja na kuua raia na kesi zinapofikishwa mahakama zinashindwa kuendelea kwa madai ya kukosekana kwa ushahidi.
Dk. Bisimba alisema matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanayofanywa na wananchi hasa familia ni asilimia 40 ambapo wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi ya kuua watu wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali pamoja na kuvamia vituo vya polisi na kupora silaha.
Alisema katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa LHRC jamii imekuwa na uelewa mkubwa wa matukio ya kifisadi yaliyowahi kutokea kama Sakata la Epa, Richmond, ununuzi wa ndege ya rais, mfuko wa kufufua uchumi na Escrow.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo Jaji Mstaafu Osebia Munuo alitoa pongezi kwa LHRC kutimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake na kutetea haki za binadamu.
Munuo alikiomba kituo hicho na mashirika mengine kuendelea kuhamasisha wananchi waliojiandikisha kujitokeza kwenda kupiga kura wakati utakapo wadia na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kuharibu amani ya nchi yetu.
"Naamini sauti ya kituo cheni cha LHRC ni kubwa hivyo baso muitumie vizuri kuhakikisha makundi yote katika jamii yanashiriki vyema katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu bila ya kubaguliwa" alisema Jaji Munuo.