NENO LA SHUKRANI KWA WADAU WA “SIASA ZA BUKOBA”
Ndugu
Wadau,
Ni miezi mitatu sasa toka kuanzishwa kwa Jukwaa la
“SIASA ZA BUKOBA” kupitia Mtandao wa Whatsapp. Tulipoanzisha Jukwaa hili, nia
ilikuwa ni kuendeleza dhima ya Bukoba Wadau Media kwa kuwapa fursa wanaKagera
hususani wanaBukoba walioko nje ya mkoa na nje ya nchi waweze kujua nini
kinaendelea kwenye siasa za uchaguzi mkuu kwenye majimbo ya Bukoba. Tunaamini tumelitimiza
vema jukumu hili na tumekidhi hitaji la wadau wetu kwa kuwawezesha kupata taarifa
za papo kwa papo viganjani mwao. Ni imani yetu kwamba tumehabarisha juu ya
mambo yaliyotendeka nyumbani bila ubaguzi wala upendeleo kwa mtu au chama
chochote. Na iwapo katika kutenda kazi hii tulimkwaza mtu, tunaomba msamaha.
Hakika haikuwa dhumuni wala kusudi letu.
Ili kufanikisha zoezi la ukusanyaji taarifa na
habari mbalimbali tuliweka ada ya mwezi ya TZS 5,000 kwa kila mdau.
Tunawashukuru wadau wote waliotuchangia. Na wale waliotuchangia zaidi ya
kiwango tunawashukuru kwa ukarimu wao. Tunaamini
hata wale wote ambao bado hawajalipa ada zao, wataithamini kazi yetu kwa
kufanya hivyo mara moja.
Ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba uchaguzi umeisha
na dalili zote zinaonyesha tumedumisha jadi yetu kwa kukamilisha zoezi hili
salama, kwa umoja na amani. Sasa ni wakati wa viongozi wetu kutimiza ahadi zao.
Bukoba Wadau Media tutaendeleza jukumu letu la kuwafikishia pongezi wakifanya
vema, kuwakosoa wakifanya kinyume na kuwashauri watakapohitaji.
Kwenye Jukwaa letu katika nyakati tofauti tofauti
kumekuwepo na mada zikihitaji muendelezo wa ajenda ya maendeleo kwa ajili ya
Bukoba. Wako wadau waliofika mbali zaidi kwa kupendekeza ianzishwe Asasi ya
Kiraia. Tunapongeza na kuungana na mawazo haya. Sisi kama Bukoba Wadau Media tunaahidi
kuendeleza mchango wetu kwenye jitihada hizi kwa kuwaunganisha wadau wengi
zaidi na kufikisha habari hizi kwa jamii ya ndani na nje ya mipaka yetu. Kulingana
na majukumu na miiko ya tasnia yetu, tunapendekeza usukani wa jitihada hizi
uratibiwe na watu binafsi wataopendekezwa na wadau badala ya kuratibiwa na
Bukoba Wadau Media ambayo ni taasisi rasmi toka mwaka 2013.
Kumekuwa na mapendekezo ya kutaka viongozi wateule
wa ngazi mbalimbali (Udiwani na Ubunge) katika manispaa ya Bukoba kuunganishwa
kwenye Jukwaa hili. Tumelipokea wazo hili na kulifanyia kazi. Wako viongozi
walioonyesha utayari wa kujiunga nasi. Lakini ili viongozi hawa waweze
kushiriki kikamilifu katika mijadala, tunadhani ni tija zaidi kuwa wanaletwa
kwa muda maalumu na kuondolewa baada ya mada au shughuli waliyoitiwa. Kwa
sababu uzoefu umeonyesha kuwa, kuwemo katika Jukwaa si uthibitisho kwamba
mwanachama anasoma au kupitia michango yote. Hivyo kuwa na uhakika, njia bora
ni kuwaalika kwa mada maalumu na kisha kuwaondoa. Tunadhani kwa njia hii, wadau
pia watakuwa huru zaidi kuwajadili viongozi wao.
Jukumu la kwanza la Jukwaa letu liliendeshwa chini
ya jina “SIASA ZA BUKOBA” Sasa limekamilika tena kwa mafanikio makubwa. Tunapokwenda
jukumu la pili tunapendekeza kubadili jina na kuwa “MAENDELEO YA BUKOBA” Hivyo
kama hatutapata pingamizi ndani ya saa 24 tutabadili jina kuakisi jukumu jipya
la Jukwaa letu.
Tunawashukuru sana wadau.
Imetolewa na Uongozi wa Bukoba Wadau Media