WENGI WAJITOKEZA KATIKA UZINDUZI WA MAADHIMISHO YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE JIJINI DAR ES SALAAM
Maelfu wajitokeza katika maandamano ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, hapa wakiendelea na matembezi ya kupinga ukatili wa Kijinsia
Maandamano yakipokelewa na Mkurugenzi wa shirika la misaada la Marekani USAID Daniel Moore, Mwakilishi wa Balozi wa Ireland
nchini Maire Matthews, Mwakilishi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa Wanawake
Lucy Melele, Mkurugenzi wa shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo
barani Afrika - WiLDAF, Dr. Judith Odunga, pamoja na wawakilishi wa mashirika
wahisani na viongozi mbalimbali.
Dr. Judith Odunga kutoka WiLDAF akiwakaribisha wageni.
Mwanaharakati mama Siwale, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Anna Mghwira(wa kwanza kulia) ni miongoni mwa waliohudhuria maadhimisho hayo.
Wageni mbalimbali
Maigizo kuhusu uchapaji wa viboko kwa wanafunzi
Mwakilishi wa Balozi wa Ireland Maire Matthews akizungumza
Lucy Melele kutoka shirika la UN Women akizungumza
Mwalimu akitoa ushuhuda
Paulina Mkonongo(wa kwanza kulia), Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Akisikiliza jambo
Mgeni rasmi Bi. Paulina Mkonongo Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi akitembelea sehemu za maonyesho kutoka kwa mashirika mbalimbali.
Baadhi ya wadau wakitembelea mabanda
Wadau mbalimbali waliohudhuria maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake.
Maadhimisho
ya Siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake leo yamefunguliwa rasmi kwa
kuanza na maandamano ya amani yaliyoanzia uwanja wa Tipi Sinza darajani hadi
ukumbi wa hoteli ya Blue Pearl iliyopo jengo la Ubungo Plaza jijini Dar es
salaam.
Maandamano
hayo yalihudhuriwa na maelfu ya watu yaliongozwa na bendi ya jeshi la polisi
kupitia njia za Shekilango kisha barabara ya Morogoro hadi katika jengo la
Ubungo Plaza ambapo yalipokelewa na Mkurugenzi wa shirika la misaada la
Marekani USAID Daniel Moore, Mwakilishi wa
Balozi wa Ireland nchini Maire Matthews, Mwakilishi kutoka shirika la Umoja wa
Mataifa Wanawake Lucy Melele, Mkurugenzi wa shirika la Wanawake katika Sheria
na Maendeleo barani Afrika - WiLDAF, Dr. Judith Odunga, pamoja na wawakilishi
wa mashirika wahisani na viongozi mbalimbali.
Akitoa
neno la ukaribisho, Dr. Judith Odunga alisema kampeni ya siku 16 kwa mwaka huu
imelenga zaidi kuzungumzia suala zima la usalama mashuleni. Lengo kuu ikiwa
kuhamasisha umma kuhusu ukubwa wa ukatili wa kijinsia kwa vijana na watoto wetu
mashuleni.
“Ni
kutokana na unyeti wa tatizo la ukatili wa kijinsia mashuleni, WILDAF na wadau
mbalimbali tumeona kuna umuhimu wa kushirikisha Wizara ya elimu na ufundi stadi
ili kuzungumzia ukatili wa kijinsia mashuleni na kujenga mikakati ya kuzuia
ukatili huo” Aliongezea.
Dr.
Odunga aliitaja kauli mbiu ya mwaka huu kuwa ni FUNGUKA! CHUKUA HATUA, MLINDE
MTOTO APATE ELIMU. “Kauli hii inalenga kumshawishi mtu binafsi, kuwashawishi
walimu, wanafunzi, wazazi na jamii kwa ujumla, kuwalinda watoto dhidi ya
ukatili wa kijinsia na kuhakikisha kwamba shule ni mahala salama. Ni vyema
kutafakari kwa kina jinsi vitendo vya ukatili wa kijinsia mashuleni
vinavyoathiri maendeleo ya watoto wetu kielimu.” Alisema Dr. Odunga.
Dr.
Odunga alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali kufanya yafuatayo:
1.
Kufutwa kabisa kwa adhabu ya viboko mashuleni na
waalimu kufundishwa au kutafuta mbinu za kutoa adhabu mbadala.
2.
Kutengeneza mwongozo wa utekelezaji wa sera ya
elimu ya mwaka 2014 utakaoelekeza upatikanaji wa elimu ya msingi iliyo bora na
salama.
3.
Kuboresha miundombinu rafiki ya elimu ikiwa ni
pamoja na kuwa na madarasa ya kutosha, madawati, vyoo na sehemu za kujisitiri
watoto wa kike, mabweni, uzio pamoja na kuwa na usafiri wa uhakika kwa
wanafunzi.
4.
Serikali kuweza kuunda na kusimamia mabaraza
yatakayo kuwa yanasikiliza malalamiko ya wanafunzi mashuleni.
5.
Tunaomba Wizara ya elimu na ufundi stadi kushirikiana
na wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
kutunga Sheria ya Ukatili wa Majumbani sambamba na kubadilisha Sheria ya Ndoa
ya mwaka 1971 inayoruhusu ndoa kwa mtoto chini ya miaka 18.
Akifungua
rasmi kampeni hizi, mgeni rasmi Paulina Mkonongo ambaye ni Mkurugenzi wa Elimu
ya sekondari kutoka Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi aliyemuwakilisha
Katibu mkuu wa wizara hiyo alisema, “ukatili wa kijinsia huleta athari hasi
katika utoaji na upatikana wa fursa mbalimbali za kijamii ikiwemo fursa ya
elimu kwa watoto wetu, hivyo kuwa ni kikwazo katika kujenga usawa wa kijinsia
nchini.
Aidha
Mkonongo alisema serikali imefanya juhudi za makusudi kuzuia ukatili na kuleta
usawa katika kupambana na ukatili wa kijinsia kwa kuweka sera na mipango
inayozingatia usawa na kupinga ukatili kwa makundi mbalimbali, katika jamii
ukiwemo ukatili wa kijinsia.
Mkonongo
alitoa wito kwa wananchi wote kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili na
kwamba kila mtoto ana haki ya kulindwa popote anapokuwepo iwe nyumbani,
shuleni, kwenye vyombo vya usafiri, michezoni na njiani wanapokwenda na kurudi
shuleni pia kuwapa mbinu za kujilinda wenyewe.
Naye
mwakilishi wa Balozi wa Ireland nchini Bi. Maire Matthews alisema kuwa takwimu
za hivi karibuni zinaonyesha kuwa wastani wa asilimia 45 ya wanawake Tanzania wenye
umri kati ya miaka 15 – 49 waliripoti kuwahi kufanyiwa ukatili wa kimwili au
kingono katika maisha yao. Alisema takwimu nyingine zinakadiria kiwango hicho kuwa
kati ya 41 – 56%.
Kwa
upande wake Lucy Melele kutoka shirika la UN Women aliyemwakilisha Mwakilishi
wa shirika hilo hapa nchini Anna Collins alisema wanawake na wasichana
ulimwenguni kote wanapitia aina mbalimbali za ukatili ambayo inawanyima haki
zao za msingi, ni tishio la demokrasia na ni kizuizi cha amani ya kudumu. Hata
hivyo alisema shirika la umoja wa mataifa litaendelea kufanya kazi kwa ukaribu
na wadau wa maendeleo, serikali, mashirika mbalimbali, na jamii katika kampeni
ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Kampeni
ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia pia inafanyika kikanda katika kanda
ya ziwa (Mwanza, Mara na Shinyanga, kanda ya Kaskazini (Manyara, Arusha,
Kilimanjaro na Tanga), kanda ya kati (Dodoma, Morogoro na Singida), kanda ya
Kusini (Mtwara, Songea, Mbeya, Iringa na Lindi, Kanda ya Pwani (Dar es salaam
na Pwani) zikisimamiwa na wadau mbalimbali wakiwemo mashirika ya Kivulini,
CWCA, NAFGEM, Morogoro Paralegal, Mtwara
paralegal, WiLDAF, TWCWC pamoja na jeshi la Polisi.