BONANZA LA MICHEZO KWA SHULE ZA MSINGI LA JAMBO BUKOBA LAFANA KATIKA VIWANJA VYA GYMKHANA BUKOBA MANISPAA
Shirika la Jambo Bukoba lisilo la Serikali linalojihusisha na maendeleo
ya elimu na michezo Mkoani Kagera limefanya Bonanza la michezo kwa shule za Msingi
kutoka Halmashauri zote za Wilaya na Manispaa ya Bukoba lilofanyika 29 Januari,
2016 katika viwanja vya Gymkhana Manispaa ya Bukoba.
Katika Bonanza hilo Bw. Clemence N. Mulokozi mwazilishi wa shirika
hilo wakati wa ufunguzi alisema Jambo Bukoba imekuwa ikijihusisha na mambo makuu
manne ambayo ni kujenga miundombinu shuleni kama vyoo, Kuzisaidia shule katika
upatikanaji wa vitabu, Kuzisaidia shule katika upatikanaji wa vifaa vya michezo
na kutoa elimu ya UKIMWI kupitia michezo, na Kukarabati madarasa na ofisi za
walimu katika shule.
Bw. Clemence aliishukuru Serikali ya Mkoa wa Kagera kwa ushirikiano wanaoupata
shirika la Jambo Bukoba katika kutekeleza majukumu yake aidha, aliwaomba wazazi
kujitoa kushiriki katika kuwasaidia watoto wao katika upatikanaji wa uji na
chakula shuleni ili watoto wacheze kwa afya njema na kushiriki kikamilifu
katika masomo yao.
Mgeni rasmi katika Bonanza
hilo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella ambaye katika hotuba
yake alilipongeza sana Shirika la Jambo Bukoba kwa kazi nzuri wanayoifanya
katika Mkoa wa Kagera pia aliwashukuru wafadhili kutoka Ujerumani kwa kufadhili Jambo Bukoba Mkoani Kagera.
Mhe. Mongella alisema kuwa michezo inasaidia sana watoto kuchangamsha
akili yao katika masomo darasani jambo ambalo linapelekea watoto hao kufaulu
mitihani yao ya kawaida na ya mwisho katika kuhitimu elimu ya msingi tofauti na
kutocheza ambapo watoto hukaa wamezubaa na kutochangamka na kupelekea akili
kudumaa.
Mkuu wa Mkoa Mongella alitoa agizo kwa Maafisa Elimu kupitia kwa
Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya
kuhakikisha wanatenga viwanja vya kuchezea watoto katika shule , kunnuua vifaa vya
michezo na kutoa taarifa za michezo kwa Afisa Elimu Mkoa katika taarifa ya kila
mwezi ya maendeleo ya elimu kwa kila Wilaya.
Aidha, Mhe Mongella aliliomba Shirika la Jambo Bukoba kushirikiana na
Maafisa Elimu wa Wilaya na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi kuendesha vikao vya
wadau katika kila shule ili kuwa na uelewa wa pamoja wa michezo katika Mkoa na
kushirikisha shule nyingi zaidi kuliko ilivyo sasa shule moja kila Wilaya.
Mwisho Mhe. Mongella aliwahakikishia Jambo Bukoba kuwa watapata
kiwanja kikubwa cha kujenga shule au kituo cha michezo kwa ajili ya kufundishia
michezo kwa watoto na watu wazima kucheza michezo mbalimbali katika Mkoa wa Kagera kama walivyoomba kwa
uongozi wa Mkoa na alisema kiwanja hicho kitapatikana kabla ya Machi 1, 2016.
Bonanza hilo lilihusisha wananfunzi wanamichezo 240 kutoka katika
shule za Msingi nane, wanafunzi 30 kila shule moja kutoka kila
Halamashauri, wanafunzi hao wavulana 15
na wasichana 15 waliwakilisha kila Halmashauri wakiwa na walimu wawili wawili
kutoka kila shule bingwa ngazi ya Wilaya.