Bukobawadau

MWANGAZA, Sehemu ya 4:

MWANGAZA, Sehemu ya 4:
Siku moja tukiwa darasa la saba, tulichukuliwa wanafunzi wachache tuliokuwa tunafanya vizuri darasani kwa ajili ya kwenda kushindanishwa na shule nyingine za mkoa wa Singida. Hii ilikuwa ni wiki kadhaa kabla ya kufanya mtihani wa moko (mock). Mashindano hayo hayakuwa na lengo tu la kutupima akili au kutuandaa na mtihani wa mwisho, bali pia yalikuwa na lengo kubwa la kuwapatia baadhi ya watoto wenye uwezo mkubwa darasani lakini wenye hali duni za uchumi wa familia zao fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari. Mwaka huo ilitokea bahati kuwa kulikuwa na wafadhili waliojitolea kufadhili masomo ya sekondari kwa vijana ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa na changamoto za ki uchumi katika familia zao, huku wakitilia mkazo wale tu wanaofanya vizuri darasani.

Kwa bahati shule yetu ilikuwa moja ya shule zilizopata hiyo fursa kuingia kwenye shindano, na watoto watatu tulichukuliwa kushindanishwa na watoto wengine zaidi ya 100 kutoka kwenye shule mbalimbali za vijijini mkoani Singida. Walihitajika washindi kumi tu kati ya vijana wote ambao walitakiwa kushinda kwa wastani wa juu sana ili kupata fursa hiyo. Mimi na Mawazo na mwenzetu mwingine mmoja tulichaguliwa.

Licha ya kuwa nilikuwa nafanya vizuri sana darasani, lakini bado nilikuwa sijiamini vya kutosha kushindanishwa na watoto mahiri na wengi kutoka kwenye shule mbalimbali. Baba yake Mawazo alitafuta mwalimu maalumu kwa ajili yetu ili kutusaidia na maandalizi. Nilipewa ruhusa nyumbani kuhamia nyumbani kwa kina Mawazo kwa muda wa kama mwezi mmoja hivi kabla ya siku ya shindano. Tulisoma usiku na mchana. Mwalimu alitusaidia kufanya na kurudia maswali ambayo mara nyingi huulizwa kwenye mitihani ya mwisho.

Siku zilienda na hatimaye siku ya shindano ilifika. Tuliondoka na mwalimu wetu mmoja shuleni, tukapanda basi kuelekea Singida mjini. Kwa mara ya kwanza kwenye maisha yangu nilifika mjini, nikaona magari mengi, nyumba kadhaa za bloko na umeme kila mahali. Pia nilishangaa kuona maji yakitoka ndani, bombani kwenye chumba tulimolala. Mimi na Mawazo tulilala chumba kimoja, na mwalimu alitafuta chumba kwajili ya mwenzetu wa kike tuliyekuwa naye.

Asubuhi tulipelekwa sehemu ambapo tulikutanishwa na wenzetu wote ambao tungefanya nao mtihani. Ilikuwa ni shule ya bweni, na tulilala hapo siku mbili huku tukiendelea kujiandaa na mtihani na baada ya hizo siku mbili, hatimaye siku ilifika. Tulitumia siku nzima (moja) kufanya mitihani mitatu (Hisabati, Maarifa na Lugha). Baada ya siku hiyo ndefu tulilala tena hapo shuleni siku hiyo na kesho yake tukaanza safari kurejea nyumbani.

Siku kadhaa baada ya matokeo ya mitihani ya moko kutoka, tuliitwa ofisini kwa mwalimu sote watatu. Mwalimu alianza kwa kututia moyo kuwa sote tulifanya vizuri katika lile shindano, na hasa mimi na Mawazo kwani wastani tuliopata ni zaidi ya asilimia 90 kwa kila somo. Pia alisema kwamba hii inaonesha hata kama hatujapata ile nafasi ya kuchaguliwa na kusomeshwa na wafadhili, bado tuna fursa nzuri sana ya kuchaguliwa kusoma shule za serikali baada ya mtihani wa taifa, kwani kwa ufaulu ule, ni lazima tutachaguliwa kusoma shule nzuri za serikali. Maneno ya mwalimu yalinifanya nilowe jasho. Nilijua ushindani uliokuwepo lakini nilikuwa na matumaini makubwa sana ya kuchaguliwa. Ufadhili huo kwangu ungekuwa na maana kubwa sana, kwani sasa si tu kuwa nisingehitaji tena kujilipia ada, bali pia wafadhili waliahidi kutoa msaada wa kifedha kwa familia za watoto husika. Nilikuwa tayari kichwani nina ndoto kubwa kuhusu huo ufadhili na kiukweli, japo Mawazo ni rafiki yangu niliyempenda sana sana, siku ile nilimuonea wivu mwalimu alipotuambia kuwa ni yeye pekeake kati yetu sote watatu aliyefanikiwa kuingia kwenye kumi bora.

Tulioneshwa alama zetu, Mawazo alikuwa amenipita kwa alama moja tu. Ila kwa ushindani uliokuwepo, tofauti hata ya nusu alama ilimaanisha ushindi mkubwa. Nilimtazama Mawazo na kutoa tabasamu feki, na nilitegemea angenionesha furaha japo kidogo, lakini badala yake Mawazo alitoa machozi. Ni dhahiri hayakuwa machozi ya furaha, kwani nikiwa bado najiuliza swali hilo, alimuuliza mwalimu,’Hakuna uwezekano wa kugawa nafasi yako kwa mtu mwingine kama tukiongea nao?’ Mwalimu hakumjibu, alimtoa yule msichana akabaki na sisi wawili. Alimjua Mawazo vizuri na alijua alikuwa akimaanisha alichouliza. Hata mimi pia nilijua kuwa alikua akimaanisha.

Tulikaa na mwalimu wa taaluma karibu saa nzima akijaribu kumueleza Mawazo kuwa japo sikufanikiwa kupata ile fursa, bado nina nafasi nzuri ya kuchaguliwa tena shule nzuri sana. Mawazo aliumia sana kiasi cha kunifanya huzuni na wivu niliojisikia vitoweke na badala yake niliona aibu. Baadaye, alipokubaliana, alianza kunitia moyo. Japo nilimjua Mawazo kwa undani kabla, ila siku hiyo niligundua kuwa nina rafiki mwenye huruma sana. Kwa kiasi kikubwa alinifanya nikubaliane na matokeo. Niliporudi nyumbani mama pia alinisaidia kukubali matokeo yale, kwani yapo alijua kiasi gani nilitamani sana ile nafasi, lakini hakuonesha kuvunjwa moyo nilipomwambia sikupita. Mama alimpa pongezi za dhati Mawazo (alinisindikiza nyumbani siku hiyo), na pia alimshukuru jinsi alivyonisaidia kukubali, kwani alijua hali yangu ingekuwa tofauti kama tusingekuwa wote, (japo wakati huo nilikuwa bado sijamweleza yaliyojiri ofisini kwa mwalimu wa taaluma).

Hatimaye mwaka 2001 tulihitimu darasa la saba. Siku ya maafali ilikuwa siku yenye hisia mchanganyiko kwangu. Kwa upande mmoja nilikuwa mwenye furaha, nilipewa zawadi ya kuwa mwanafunzi mtulivu zaidi kwa mwaka wetu, pia nilipewa zawadi ya usafi na nilipewa zawadi ya kuongoza katika somo la Maarifa kwa mtihani wa moko. Mama yangu alikuja kunipokea kila nilipotoka kupokea zawadi, na furaha aliyoionesha usoni mwake ilifanya nijione mwenye mafanikio makubwa. Hakuwa na zawadi kubwa ya kunipa, lakini alinizawadia kitabu cha wastani chenye jina KUISHI NDOTO YAKO. Yeye hakuona uthamani mkubwa wa zawadi aliyonipa, lakini mpaka leo hii ninaandika hadithi ya maisha yangu, sitaacha kamwe kukumbuka mchango mkubwa wa kile kitabu katika mafanikio na changamoto zote nilizopitia.

Hataivyo kwa upande mwingine nilikuwa mtu mwenye huzuni. Kumaliza shule ya msingi ilimaanisha mwanzo wa safari nyingine ya elimu ambayo mpaka sasa nilikuwa sijajua itakuwaje. Kama mtoto wa kwanza, na kulingana na hali halisi ya nyumbani kwetu, sikutegemea msaada wowote wa kiuchumi kutoka kwa familia yetu. Nilijua lazima ningefaulu kwenda shule nzuri ya serikali, na katika shule nilizochagua, mbili zilikua za mikoa mingine, hivyo ilimaanisha kama ningepata kati ya hizo, ingenilazimu kwenda kuishi mbali na nyumbani kwetu.

Niliwaza nitawezaje tena kujisomesha elimu ya Sekondari, pia niliwaza jinsi gani nitaanza maisha ya kuishi mbali na familia yetu ambayo kwa namna moja ama nyingine nilionekana kama mtu anayetegemewa. Nikiwa katikati ya mawazo mengi juu ya maisha yanayofuata, alinipiga begani Mawazo ambaye alikuwa ametoka kuchukua sahani ya chakula. Nilimuangalia na kutabasamu japo sikuonesha furaha kama aliyokuwa nayo yeye. Ghafula nilipata huzuni zaidi nilipogundua kuwa miezi michache ijayo urafiki wetu utatenganishwa na umbali wa shule tutakazokuwa tunasoma. Nilijihisi kumkosa tayari Mawazo japo nilikuwa hata sijajua ni lini tutatengana.

Sherehe iliendelea, tulikunywa na kula chakula kilichoandaliwa kwa michango kidogo tuliyokuwa tumeichanga, wazazi walifurahi, wanafunzi tulipiga picha za pamoja, na hapo ndipo nilipogundua kuwa vijana wenzangu wengi sana tuliosoma nao walinipenda na kuniheshimu sana, kwani wengi waliomba kupiga picha na mimi, wengi walinitambulisha kwa wazazi wao wakisema ‘huyu ndio Nathani’, na pia kuna ambao hata sikuwachukulia kama marafiki, waliniaga kwa kunikumbatia na wengine kunishukuru. Mara nyingine unaweza ukawa unafanya vitu ambavyo unaona ni vya kawaida tu kwa watu, kumbe vina maana kubwa sana. Nikiwa shule, na hasa nilipoanza kufanya vizuri darasani, mara nyingi wanafunzi wenzangu waliniomba tukae pamoja na kufanya maswali ya nyuma (past papers) pamoja, hasa wakati wa mitihani. Utayari wangu wa kuwasaidia wenzangu wakati mwingine hata kuharibu ratiba zangu za kujisomea au kurudi nyumbani, sikujua kuwa ulinijengea urafiki kwa wenzangu wengi sana. Daima sikupenda kukataa kutoa msaada hasa wa masomo kwani nilitamani kila ninayeweza kumsaidia afanye vizuri kwenye masomo yake, nimsaidie afanye hivyo. Kulingana na hotuba ya mwalimu wa taaluma, mwaka huo walitegemea kupata matokeo bora zaidi kwa vijana kwani lilikuwa darasa lenye ushirikiano mkubwa na motisha ya juu ya kusoma. Mwalimu pia alitaja baadhi ya wanafunzi ambao walionesha juhudi kubwa sana za kuwasaidia wenzao, nikiwemo mimi, na nilipotajwa wanafunzi wenzangu walipiga makofi mengi mno.

Wakati wa chakula tulikuwa pamoja na wazazi wa Mawazo, na hapo mama alipata fursa ya kuwashukuru tena wazazi wake kwa jinsi ambavyo kijana wao amenisaidia kwa kiasi kikubwa kufanya vizuri kwenye masomo yangu. Mama yangu alikuwa ni mtu mwenye utajiri wa shukurani. Mara zote alinifundisha kuwa mtu anaponifanyia kitu, neno la shukurani lina thamani kuliko pesa na mali. Nilitumia wakati huo kujichangamsha na kujisahaulisha shida zangu kwani nilijua hii ni siku ya mwisho ya kufurahi kwa pamoja na wanafunzi wenzangu, hivyo nilikula kwa haraka na kisha kwenda kuendelea na stori za hapa na pale, huku tukikumbushana miaka ya nyuma, tukicheka na kufurahi.

Katika mambo ambayo shule yetu imefanikiwa sana, ni uandaaji wa mahafali. Tofauti na shule nyingi za vijijini, shule ya msingi Kilimahewa inasifika kwa kuandaa mahafali yaliyochangamka sana, na japo uandaaji wake si wa gharama kubwa, walimu walizitumia siku hizo kuwa siku nzuri za kuwakutanisha wazazi na wanafunzi, na pia kutenga muda wa kutosha kufahamiana, kuzungumza na kucheka. Siku hiyo nadhani ilikuwa na furaha zaidi kwani kulingana na mshikamano mkubwa tuliokuwa nao wanafunzi, wazazi wetu wengi walifahamiana na hivyo hawakuwa wapweke.

ITAENDELEA...

SHARE na LIKE Ukurasa wetu wa Bukobawadau Entertainment Media
Next Post Previous Post
Bukobawadau