BARAZA LA WAFANYAKAZI SEKRETARIETI YA MKOA WA KAGERA LAZINDULIWA RASMI NA KUPITISHA BAJETI YA MKOA MWAKA 2016/2017
Sekretarieti ya Mkoa wa Kagera yafanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi
ambacho kilikuwa mahsusi kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wake, pili kuzindua
rasmi Baraza la Wafanyakazi la Mkoa, na tatu kupitia na rasmu ya maandalizi ya
bajeti ya Mkoa kwa mwaka wa fedha 2016/2017
Kikao hicho kilifanyika Februari
11, 2016 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na wajumbe walimchagua
Bw. Pius Ngaiza (Afisa Msimamizi wa Fedha Sekretariet ya Mkoa) kuwa Katibu wa
Baraza na Bw. Egidius Karatunga (Muuguzi Msaidizi Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa) kuwa Katibu msaidizi ambapo Katibu
Tawala wa Mkoa ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo.
Mara baada ya uchaguzi huo Mkuu
wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella alizindua Baraza hilo la Wafanyakazi kwa
kuwakumbusha wajumbe kufanya vikao vya Baraza hilo kama sheria na kanuni
zinavyoelekeza ili masuala mbalimabli ya watumishi yaweze kuongelewa na
kupatiwa ufumbuzi kwa muda muafaka.
“Kutofanyika kwa vikao vya Baraza
la Wafanyakazi kunapelekea kutokuwa na ufanisi wa kazi mahala pa kazi jambo
ambalo linapelekea kutokuwepo mawasiliano kati ya mwajiri na watumishi wake,
aidha, kunakuwepo usimamizi finyu wa utendaji kazi katika ofisi na kupelekea
malalamiko kwa wananchi.” Alistiza Mhe. Mongella.
Katika hatua nyingine Baraza hilo
lilipitia na kujadili mapendekezo ya Bajeti na Mpango wa Maendeleo wa Mkoa wa
Kagera wa mwaka wa fedha 2016/2017 na kuiboresha bajeti hiyo kulingana na maoni
na ushauri kama ambavyo wajumbe waliona inastahili kutokana na idara
walizoziwakilisha ambapo Mkoa unaomba
jumla ya shilingi bilioni 287,798,977,509 katika bajeti ya mwaka 2016/2017.
Pamoja na kujadili na kupitisha
maandalizi ya bajeti ya Mkoa, Baraza la wafanyakazi pia lina jukumu la kufanya
vikao vya kushirikisha wafanyakazi ili
kutatua masuala mbalimbali yanayowahusu kazini kwao, kuishauri Serikali
kuboresha maslahi pamoja na kupandishwa
vyeo kwa watumishi.
Katibu wa TUGHE mkoa akitoa
nasaha zake wakati wa kufunga kikao hicho aliwakumbusha wajumbe kuwa watetezi
wa watumishi kwa kufanya kazi kwa uwajibibikaji mkubwa ili kuondoa malalamiko
ya watumishi kazini, pia alisema TUGHE haipo kwa ajiri ya kugombanisha
watumishi na waajili wao bali kuwaunganisha ili kuwepo ufanisi wa kazi.
Baraza la Wafanyakazi la Mkoa
linajumuisha wajumbe kutoka Sekretarieti ya Mkoa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,
na Ofisi za Makatibu Tawala wa Wilaya.