Bukobawadau

KAITABA STADIUM YAELEKEA KUKAMILIKA KUWEKEWA NYASI BANDIA NAKUREJEA KWA MICHEZO YA RIGI KUU VPL MJINI BUKOBA MWAKA 2016

Hatimaye matengenezo ya dimba(pitch) la kuchezea mpira wa miguu katika Uwanja maarufu wa mjini Bukoba ujulikanao kama Kaitaba Stadium yanaelekea mwisho kukamilika mara baada ya kuwasili kwa raba za kuweka kwenye nyasi bandia na uwanja huo kuanza kutumika hasa kwa michezo ya Ligi Kuu nchini Vodacom Premire League (VPL)

Raba hizo ziliwasili tarehe 12.02.2016 na kupakuliwa uwanjani hapo ili Mkandarasi aweze kumalizia kazi yake ya kutandika nyasi bandia ambapo uwanja wa Kaitaba umekuwa ukitengenezwa kwa awamu mbalimbali tangu Machi 2015
Awamu ya kwanza uwanja huo uliparuliwa kutoa nyasi za asili, kusawazishwa na kushindiliwa kwa changalawe. Awamu ya pili ilikuwa ni kumwaga zege na kujenga mfumo wa kutoa maji uwanjani pindi mvua inaponyesha.

Awamu ya tatu uwanja wa Kataiba ulifanyiwa ukaguzi na tathmini na Shirikisho la Mpira Ulimwenguni FIFA na mara baada ya tathmini hiyo lilitandazwa janvi la nyasi bandia na hatua inayofuata ni kuweka raba ambazo zinafanana na udongo ili kulainisha nyasi bandia  wakati mpira ukichezwa.

Zoezi la kuweka raba katika jamvi la nyasi bandia na kuchora alama zote za dimba la kuchezea mpira likikamilika uwanja wa Kaitaba utakuwa tayari kutumika. 
Ujenzi wa uwanja huo umeratibiwa na Shirikisho la mpira Tanzania (TFF) chini ya ufadhili wa Shirikisho la Mpira Ulimwenguni (FIFA)  kwa pamoja jukumu lao  litakuwa limekamilika lakini mara baada ya uwekwaji wa raba na nguzo za magoli jukumu lingine litakuwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba     kumalizia sehemu ya nje ya dimba la kuchezea mpira kwa kulisawazisha, kushindilia na kupanda nyasi za asili na kutengeneza njia au sehemu ya michezo ya riadha.
Aidha, Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba itatakiwa kuutunza uwanja huo mara baada ya kukamilika ikiwa ni pamoja na ulinzi wake. Wananchi wa Mkoa wa Kagera wana matarajio makubwa hasa uwanja huo ukikamilika na ligi kuu kurejeshwa Kaitaba Stadium.
Next Post Previous Post
Bukobawadau