WANANCHI KAGERA WAASWA KUACHA KUTUMIA VISHOKA KATIKA KUTAFUTA HUDUMA YA HAKI MAHAKAMNI – JAJI MWANGESI
Siku ya Sheria nchini
Mkoani Kagera imeadhimishwa katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba
ambapo wananchi kama wadau muhimu wa Mahakama wameaswa kuepukana na vishoka wa
sheria katika kutafuta haki yao Mahakamani
na kutumia wataalam wa sheria kupata haki isiyo na mashaka ya kisheria.
Rai hiyo ilitolewa na Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba
Sivangilwa Mwangesi alipokuwa akihutubia wananchi na wadau mbalimbali wa
Mahakama waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini Mkoani Kagera
Februari 4, 2016 katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.
Jaji Mfawidhi Mwangesi alisema kuwa madhumuni ya kuadhimisha Siku ya
Sheria ni kufungua mwaka mpya wa Kimahakama ambapo shughuli zote za Mahakama
huanza rasmi kwa mwaka husika, Pili ni kuwaombea dua wale wote wanaofanya kazi
za Kimahakama ili watekeleze majukumu yao ipasavyo, na Nne ni kuelimisha
wananchi juu ya kaulimbiu ya mwaka husika.
Kaulimbiu ya mwaka huu 2016
inasema, “Huduma ya Haki Kumlenga Mwananchi ni Wajibu wa Mahakama na Wadau”.
Jaji Mfawidhi Mwangesi akifafanua kaulimbiu hiyo alisema kuwa mchakato wa kutoa
haki unahusisha kufungua mashauri Mahakamani,
kuyasikiliza, kuyatolea hukumu na mwisho hukumu hiyo kutekelezwa ambapo
mchakato huo huwahusisha wadau wote wa
Mahakama.
Jaji Mfawidhi Mwangesi
alitoa wito kwa wananchi kuiamini Mahakama na kuacha kutumia vishoka wa sheria katika
kutafuta huduma ya haki Mahakamani bali watumie Mawakili wenye weledi mzuri
katika sheria ili kupata haki. Aidha, alisema Mahakama kwa sasa imejipanga
kutoa huduma ya haki kulingana na sheria kwa kila mwananchi bila kujali uwezo
wake wa kifedha ilimradi sheria ifuatwe.
Mwanasheria Mfawidhi wa
Serikali Mkoani Kagera Hashim Ngole katika maadhimisho hayo alisema Mahakama
ina wajibu wa kuijisikia kila mara kutoa huduma ya haki kwa wananchi wake, Pili
Mahakimu wana wajibu wa kutoa dhamana kwa watuhumiwa kulingana na sheria
isemavyo, Tatu Mahakama kuzingatia sheria wakati wa kutoa huduma ya haki kwa
wananchi, na Nne Mahakama inaowajibu wa kutoa huduma ya haki bila kufungamana
na upande wowote.
Bw. Ngole akiwataja wadau
wa Mahakama na majukumu yake alisema, Mdau wa kwanza wa Mahakama ni Ofisi ya
Mwanansheria Mkuu wa Serikali mwenye jukumu la kufungua na kuendesha mashauri ya
wananchi kwa weledi Mahakamani, Kuhakikisha mashahidi wanahudhuria Mahakamani,
Kupokea na kujibu malalamiko ya wananchi
kuhusu masuala ya kisheria.
Wadau wengine ni Jeshi la
Polisi na wajibu wao ni kupeleleza mashauri kujua ukweli wa makosa, Magereza
wajibu wao ni kuhakikisha wafungwa wanahudhuria Mahakamani bila kukosa,
Mawakili kuhakikisha wanasimamia kesi za wananchi kwa weledi ili haki
ipatikane, Bunge wajibu wake ni kutunga sheria ambazo siyo kandamizi na mwisho
ni Wananchi wanaotakiwa kutoa ushahidi wenye ukweli Mahakamani.
Naye Mkuu Mkoa wa Kagera
ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya sheria akiwasalimia
wananchi aliipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kwa kufanya vizuri kwa mwaka
2015 kwa kuvuka malengo ya kutoa haki na kushughulikia mashauri mengi
yaliyokuwa yamekwama aidha, Mahakama hiyo kuwa ya kwanza kati ya mikoa mitatu
iliyofanya vizuri nchini.
Aidha, Mhe Mongella alitoa
wito kwa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kuhakikisha inaongeza nguvu kwa Mahakama
za chini hasa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo ili kutoa huduma ya haki
kwa wananchi walio wengi zaidi ili kupunguza malalamiko kutoka kwa kwenye jamii.
Mikakati ya Mahakama Kuu
Kanda ya Bukoba kwa Mwaka 2016
Kuanzisha
Dawati la Malalamiko ili kupokea malalamiko ya wananchi na kutoa ushauri wa
kisheria kwa wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria pia kutoa majawabu ya
malalamiko yao.
Mahakama Kuu kuondoa
mashauri yote Mahakamani ambayo yamekaa kwa muda wa miaka mitano, Mahakama ya
Mkoa kuondoa mashauri yote yaliyokaa miaka miwili na Mahakama za Mwanzo
kuhakikisha mashauri yote yaliyokaa mwaka mmoja yanaondolewa na kubaki na
mashauri ya chini ya mwaka mmoja.
Majaji na Mahakimu
kutembelea Magereza ili kuondoa kesi zenye mikwamo za wafungwa ili kupunguza
msongamano katika Magereza. Aidha, mashauri ya jamii au yenye maslahi mapana
katika jamii kuhakikisha yanaondolewa au kushughulikiwa haraka ili kupunguza misuguano katika jamii mfano
kesi za uchaguzi.