MKUU WA MKOA MPYA WA KAGERA AKABIDHIWA OFISI NA KUANZA KAZI RASMI KWA KUTOA MAAGIZO YAKE KWA WATENDAJI NA VIONGOZI WA MKOA HUO
Mkuu wa Mkoa mpya wa Kagera Meja
Jenerali Mstaafu Salim Mustafa Kijuu amekabidhiwa rasmi ofisi na kuanza
kutekeleza majukumu yake kama Mkuu wa Mkoa wa Kagera. Makabidhiano hayo yamefanyika
siku ya Jumanne Machi 22, 2016 kati yake
na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella aliyehamishiwa Mkoani
Mwanza.
Katika hafla fupi ya makabidhiano
hayo Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Kijuu akiongea na wadau mbalimbali wa Mkoa
aliwaomba wananchi wote wa Kagera
kuonesha ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake aidha
aliongelea mikakati yake katika kutekeleza majukumu yake hapa Mkoani.
Watumishi wa Umma
Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Kijuu
aliwakumbusha watumishi wa umma katika Mkoa wa Kagera kuifahamu vizuri dhamira
ya Serikali ya Awamu ya Tano kuwa ni kuwajibika kwa kufanya kazi kwa kasi
inayotakiwa, kwa nguvu, maarifa, upendo na uadilifu mkubwa bila kusukumwa na
mtu yeyote aidha, kila mtumishi afanye kazi kwa uwezo wake wote.
“Mtumishi wa umma anatakiwa
kufahamu wajibu wake hasa kwa kuwatumikia wananchi ili kusukuma maendeleo yao
mbele kwa kufanya kazi kwa kujituma bila kubabaisha, pili kufanya kazi kwa
kutenda haki bila kudhurumu wananchi haki zao.”
Alitoa ilani Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Kijuu.
Maagizo
Mkuu wa Mkoa Mpya wa Kagera Mhe.
Meja Jenerali Mstaafu Kijuu aligiza kuundwa mara moja mabaraza ya kushughulikia
haki za wananchi kama hayapo na kama yapo yaanze kufanya kazi zake mara moja
kwa kuwahudumia wananchi ili kupata haki zao. Wakuu wa Wilaya kuhakikisha
wananhimiza wananchi kufanya kazi kila mtu kwa nafasi yake bila kutega.
Sekta ya Afya, Vituo vyote
vya kutolea huduma za afya vinatakiwa kuwa katika hali ya usafi na kutoa huduma
stahiki kwa wananchi. Watoa huduma wanatakiwa kuhakikisha kuwa dawa
zinapatikana muda wote kama ambavyo Serikali imekuwa ikiagiza mara kwa mara.
Ulinzi na Usalaama wa Mkoa, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Kijuu
alisema kuwa wale wote ambao wanafanya vitendo vya uvunjifu wa amani hasa kwa
kuteka wananchi na vyombo vya usafiri maporini, atahakikisha anasafisha uchafu
huo wote kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalaama ili kukomesha tabia
hiyo.
Wahamiaji Haramu, Mkuu wa Mkoa Mpya amewaagiza Wakuu wa Wilaya za
mpakani kutoa au kugatua madaraka kwa Wenyeviti wa vijiji na Vitongoji ili
waweze kufuatilia mienendo ya wageni wanapoingia nchini ili waweze kuwarudisha
mara moja walikotoka. Aidha, aliwaagiza Afisa Uhamiaji Mkoa na Jeshi la Polisi
kufanya kazi zao kikamilifu ili kuondoa wahamiaji haramu.
Chakula, Kwakuwa Mkoa wa Kagera hauna baa la njaa Mkuu wa Mkoa
alisema kuwa wananchi wanatakiwa kuhamasishwa kutunza chakula hata kama hakuna
baa la njaa ili kujihakikishia akiba ya mbeleni bila kuuza chakula chote cha
akiba.
Ukusanyaji wa Mapato ya serikali, Mkuu wa Mkoa aliziagiza taasisi
zote za Serikali kuhakikisha zina kusanya mapato kwa njia ya kielekitroniki ili
Serikali ipate mapato ambayo yanarudishwa Mkoani kwetu ili yatekeleze miradi ya
maendeleo kwa wananchi.
Mishahara Hewa, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Kijuu aliagiza kwa
watendaji wa Serikali kama kuna watumishi hewa waondolewe mara moja kabla ya
tarehe 30/03/2016 na baada hapo utafanyika uhakiki kwa kupokea mishahra
dirishani kama mwaka 1994 na
atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Elimu, viongozi na na watendaji wanatakiwa kutekeleza Sera ya Serikali
ya Elimu Bure kwa kukabiliana na changamoto mabalimbali ambazo zimejitokeza
mara baada ya kuanzishwa Sera hiyo kama uhaba wa madawati na vyumba vya
madarasa na kufikia Juni 30, 20116 changamoto hizo ziwe zimefanyiwa kazi na
kumalizika.
Milioni
Hamsini kila Kijiji, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Kijuu alimalizia kwa
kuwaagiza viongozi na watumishi wa Serikali hasa ngazi za Serikali za Mitaa kuwaandaa wananchi kwa kuwaelimisha juu ya uibuaji
wa miradi ya maendeleo ili Milioni Hamsini zilizohaidiwa katika kampeini ambazo
zipo karibu kuletwa ziwanufaishe wananchi katika vikundi na siyo kuzigawana tu.
Kwa upande mwingine aliyekuwa
Mkuu wa Mkoa wa Kagera aliyehamishiwa Mkoani Mwanza Mhe. John Mongella
aliwashukuru wananchi wa wote wa Kagera kwa kipindi alichokuwepo Mkoani kwa
ushirikiano wao mkubwa na kuwaomba ushirikiano huo wauendeleze kwa Mkuu wa Mkoa
Mpya Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Kijuu.
Historia Fupi
Mkuu wa Mkoa mpya Meja Jenerali
Mstaafu Salim Mustafa Kijuu amehudumu
katika Jeshi la Wananchi Tanzania kwa miaka arobaini (40) na alistaafu Jeshini
Januari 30, 2016 akiwa Kamanda wa Majeshi ya nchi kavu. Aidha, Aliteuliwa kuwa
Mkuu wa Mkoa wa Kagera tarehe 13/03/2016 na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli tarehe 15/03/2016.
Mkuu wa Mkoa mpya Meja Jenerali
Mstaafu Salim Mustafa Kijuu anakuwa Mkuu
wa Mkoa wa Kagera wa 22 tangu uhuru mwaka 1961 amabpo Mkuu wa Mkoa wa kwanza wa
Kagera alikuwa Marehemu Samwel Ntambala Rwangisa.