KATIBU TAWALA MPYA WA MKOA WA KAGERA AKABIDHIWA RASMI OFISI NA KUANZA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE YA KAZI
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera
Bw. Amantius Msole tayari amewasili mkoani hapa ili kutekeleza majukumu yake ya
kazi mara baada ya kuteuliwa tarehe 25 Aprili,
2016 na kuapishwa tarehe 27 Aprili, 2016 na Mhe. Dk. John Pombe Magufuli Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Kagera.
Bw. Amantius Msole aliwasili
mkoani Kagera siku ya Jumapili Mei Mosi, 2016 na kupokelewa na Menejimenti ya
Sekretarieti ya mkoa wa Kagera. Siku ya Jumatatu tarehe 2 Mei, 2016 aliwasili
katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kukabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Katibu
Tawala wa Mkoa Bw.Nassor Mnambila .
Mara baada ya kukabidhiwa ofisi
Katibu Tawala wa Mkoa mpya Bw. Amantius
Msole alikutana na wajumbe wa Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Kagera na
kuongea nao. Katika kikao hicho Katibu Tawala mpya alisistiza sana ushirikiano
kazini ili kutekeleza majukumu yaliyopo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ufanisi.
Aidha Bw. Msole alisistiza juu ya
masuala makubwa mawili, kwanza ni suala la mkoa kutenga maeneo ya uwekezaji
ambayo hayana migogoro ili kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza katika mkoa wa
Kagera kutokana na fursa nyingi zilizopo katika mkoa wetu na kuongeza
ukusanyaji wa mapato zaidi.
Pili Bw. Amantius Msole alisistiza juu ya suala la watumishi hewa kuwa lazima uongozi wa mkoa ufanye kazi kwa kushirikiana ili kuhakikisha unalimaliza tatizo la watumishi hewa ambalo Mhe. Dk. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa akilitilia mkazo sana kila mara.
Vile vile Bw. Msole alikutana na
watumishi wote wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kujitambulisha na kuongea nao ambapo
alisistiza sana suala la ushirikiano kazini kuwa yeye mwenyewe atashirikiana na
watumishi wote na kuomba ushirikiano huo kutoka kwa watumishi.
Bw. Amantius Msole ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera wa Kumi na nane tangu uhuru mwaka 1961 na kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa Kagera alikuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kwaheri Bw. Nassor Mnambila
Katika hatua nyingine Bw. Nassor
Mnambila aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera akiongea na watumishi na kuwaaga aliwashukuru kwa ushirikiano
waliompatia kwa kipindi chote alichokaa katika mkoa wa Kagera na kusema kuwa
ataendelea kuwaombea ili waendelee kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
“Nilifika mkoani Kagera tarehe
23/12/2010 na nimeishi hapa siku 2002 nikiwa kama Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera na ninaamini kupitia nyinyi
tuliweza kufanikisha shughuli nyingi za Serikali nawashukuru kwa ushirikiano wenu, kikubwa
naomba mpatie mwenzangu ushirikiano huo huo
na mniombee afya njema huko niendako.” Alihitimisha Bw. Mnambila.