Bukobawadau

MKUU WA MKOA WA KAGERA AHIMIZA VIONGOZI WOTE KUSHIRIKI KATIKA ZOEZI LA KUTOKOMEZA MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE

Katika kikao cha Kamati ya Mkoa wa Kagera cha Huduma ya Afya ya Msingi Mkuu wa Mkoa Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu aliwaagiza uongozi wa Halmashauri za Wilaya kuhakikisha wanawahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la kampeni ya kutokomeza magonjwa yalikuwa hayapewi kipaumbele ili kutokomeza magojwa hayo.
Mhe. Kijuu aliyasema hayo katika kikao cha mkoa cha Kamati ya Huduma ya Afya ya Msingi kilichofanyika mkoani Kagera tarehe 29 Aprili, 2016 na kuhudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa, Waganga Wakuu wa Halmashauri za Wilaya na wadau mbalimbai wa afya katika mkoa.
Kikao hicho Kilicholenga kuweka mikakati ya kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ambapo Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. Thomas Rutachunzibwa aliyataja kuwa ni Kichocho, Minyoo ya tumbo, Trakoma au vikope, Matende / Mabusha au Ngirimaji na ugonjwa wa Usubi.
 Dk. Rutachunzibwa alisema kuwa mkoa umejipanga kutokomeza magojwa hayo yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwa kugawa dawa kila shule ya msingi mkoani Kagera kwa watoto ili kuyatokomeza magonjwa hayo ambayo hapo awali yalikuwa hayapewi kipaumbele na yana madhara lakini yanatibika ambapo Wilaya ya Ngara inaongoza kwa ugonjwa wa Trakoma.
Naye Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu aliwasistiza viongozi wote katika Halmashauri za Wilaya kuhakikisha wanawahamasisha wananchi, wazazi wa watoto kushiriki kikamilifu katika zoezi la watoto wao kupata dawa za magonjwa hayo aidha waeleimishwe umuhimu wa kuwaandalia chakula watoto siku itakayokuwa imepangwa kutoa dawa ili watoto wawe wameshiba ndipo wapewe dawa..
Mhe. Kijuu aliagiza wananchi wote kuendelea kushiriki katika usafi wa mazingira kwa kushiriki kikamilifu kufanya usafi kila siku ya Alhamisi ya kila wiki ambapo ni siku ya mkoa na kila siku ya Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi ambayo ni siku ya kitaifa kufanya usafi.
 Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu alimalizia kikao kwa kusistiza suala la wananchi kuhamasishwa kujiunga na mfuko waa Bima ya Afya ambapo mkoa wa Kagera kwasasa ni asilimia 5% tu ya wananchi waliojiunga na mfuko huo wakati kitaifa inatakiwa kuwa nagalau asilimia 30%.
Pia alitilia mkazo juu ya ujenzi wa vyoo vya kisasa ili kupambana na magonjwa kama kipindupindu ambapo katika mkoa wa Kagera ujenzi wa vyoo bora ni asilimia 89%. Zoezi la kugawa dawa kwa wanafunzi wa shule za msingi kwa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele iliazimiwa kuanza mapema mwezi huu Mei 2016 katika mkoa wa kagera.
Next Post Previous Post
Bukobawadau