WATANZANIA KUSHUHUDIA COPA AMERICA LIVE KUPITIA STARTIMES
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya StarTimes Tanzania, Mohamed Kimweri (kushoto), akizungumza katika na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu kampuni hiyo kupata haki za kuonesha michuano ya Copa Amerika moja kwa moja ambayoitafanyika nchini Marekani kuanzia Juni 3 mpaka Juni 26 mwaka huu. Kulia ni Meneja Maudhui wa kampuni hiyo, Paulina Kimweri.
Meneja Maudhui wa kampuni hiyo, Paulina Kimweri, akizungumza katika mkutano huo.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Na Dotto Mwaibale
KAMPUNI ya StarTimes Tanzania imefanikiwa kupata haki za kuonyesha michuano ya Copa America moja kwa moja ambayo itafanyika nchini Marekani kuanzia Juni 3 mpaka Juni 26 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi wakati wa uzinduzi huo Makamu wa Rais wa kampuni hiyo nchini, Zuhura Hanif alisema kuwa kupatikana kwa haki za kuonyesha michuano hiyo mikubwa na mikongwe ulimwenguni ikiwa inatimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwake ni jitihada za kuhakikisha kuwa wateja wao wanafurahia vipindi bora vya michezo na burudani.
“Leo StarTimes inayo habari njema kuwataarifu kuwa tumepata haki maalum za kuonyesha michuano ya Copa America moja kwa moja kutoka nchini Marekani kuanzia Juni 3 mpaka Juni 26 mwaka huu. Ninaposema haki maalumu manake ni kwamba watanzania hawataweza kushuhudia michuano hii sehemu yoyote isipokuwa kupitia king’amuzi cha StarTimes pekee.
Alisema wateja wao na wapenzi wa soka nchini wataweza kushuhudia michezo yote 32 ambapo itazikutanisha timu 16 za bara la Amerika ya Kusini na mwenyeji Marekani zitazoumana katika viwanja 10 tofauti nchini Marekani ikiwa ni kwa mara ya kwanza kufanyikia huko.” Alisema Hanif.
Hanif aliwataka watanzania na wapenda soka kwa ujumla kujiandaa kushuhudia mechi kali za miamba ya soka kutoka bara la Amerika ya Kusini ambazo itayakutanisha majina makubwa katika ulimwengu wa mpira wa miguu kama vile; Lionel Messi, Kun Aguero (Argentina), Alexis Sanchez, Arturo Vidal (Chile), Neymar, Marcelo (Brazil), Luis Suarez, Edinson Cavani (Uruguay) na wengineo.
“Ninafahamu kuwa watanzania ni miongini mwa mashabiki wakubwa wa mchezo wa soka hivyo watafurahia zaidi kuwatazama wachezaji wanaowapenda wakiwakilisha mataifa yao katika michuano hii. Tayari tumekishashuhudia ligi mbalimbali ulimwenguni zikielekea ukingoni kama vile ligi za Bundesliga na Serie A za Ujerumani na Italia ambazo tayari timu za Bayern Munich na Juventus zimaeshatangazwa mabingwa. Na nafurahi kuwa ligi hizo zote mbili zilionekana moja kwa moja kwenye chaneli za michezo za ving’amuzi vyetu kwa malipo ya gharama nafuu kabisa ya mwisho wa mwezi kuanzia sh. 5,000 aliongezea
“Ningependa kuchukua fursa hii kuwataka watanzania na wateja wetu kwa ujumla kuwa michezo na burudani kwetu StarTimes ndio nyumbani. Kwa kuliona hilo baada ya kufaidi mechi za ligi kuu za Ujerumani na Italia sasa tumewaletea Copa America kuhakikisha kuwa mnafurahia vema luninga zenu.
Mbali na michuano hii tunaahidi kuendelea kuwaletea michuano mingine kama awali tulivyofanya kwa Kombe la Dunia la Wanawake, Kombe la Vilabu Bingwa Duniani, Kombe la Dunia la Vijana chini ya Miaka 20 na miningineyo. Nawasihi wateja wetu kukaa mkao wa kula na wasiojiunga nasi wafanye hivyo ili kufaidi uhondo huu utakaowajia hivi punde kwenye luninga zao.” Alisema Hanif.
Michuano ya Copa Amerika inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi Juni kuanzia tarehe 3 mpaka 26 mwaka 2016 ni michuano mikongwe zaidi duniani ikiwa inatimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwake ambapo nchi ya Uruguay inashikilia rekodi ya kuchukua mara nyingi zaidi, mara 15 ikifuatiwa na Argentina mara 14. Michuano ya mwaka huu itakuwa ni ya kusisimua zaidi hasa kwa bingwa mtetezi nchi ya Chile kutetea ubingwa wake, ambapo aliuchukua mwaka 2015 baada ya kuishinda timu ya taifa ya Argentina kwa mikwaju ya penati.