GARI LA ZIMAMOTO LAZINDULIWA WILAYANI KARAGWE NA ZAIDI YA MILIONI ISHIRINI ZACHANGWA KATIKA HARAMBEE ILI KULIBORESHA GARI HILO
Hatimaye baada ya matukio ya moto
kuikumba Wilaya ya Karagwe mara kwa mara na kusababisha hasara kubwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo
kutokana na kutokuwa na gari la Zimamoto uongozi wa Wilaya hiyo kupitia Mkuu wa Wilaya Mhe.
Deodatus Kinawilo ulifanikisha juhudi za kupata gari la kuzima moto wakati
janga hilo linapotokea.
Gari hilo lilitolewa na Serikali
kupitia Jeshi la Zimamoto nchini na lilizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera
Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu Juni 8, 2016 katika viwanja vya
Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe na kurikabidhi kwa Mkuu wa Kituo cha Wilaya
cha Jeshi la Zimamoto na Uokozi Karagwe Sajenti P.F. Mmbale tayari kwa ajili
kukabiliana na majanga ya moto.
Pamoja na gari hilo kutoka nchini
Japani kuzinduliwa lakini kimuundo limetengenezwa kwa ajili ya kazi za uokoaji
pamoja na kuzima moto maeneno ambayo yana vyanzo vya maji kama ‘fire hydrant’,
visima vikubwa, mabwawa pamoja na sehemu ambazo gari kubwa za zimamoto hazifiki
kwa hiyo kutokana na mazingira ya Wilaya
ya Karagwe kutokuwa miundombinu hiyo ya maji gari linahitaji kuboreshwa.
Maboresho hayo ni pamoja na kuwa
na msaada wa kuwepo na gari linalobeba maji safi (water bowzer) pindi tukio la
moto likitokea bowzer na gari la zimamoto yaongozane kutoa msaada wa maji
wakati wa kuzima moto. Au gari la zimamoto lijengewa tanki la maji kulingana na
uwezo wake angalau lita 2000 kwani gari
hilo lilikuwa halikutengenezwa kwa lengo
la kubeba maji bali ni (Movable Pump).
Baada ya Mkuu wa Mkoa kupokea
taarifa na kuonekana kuwa gari hilo pamoja na kuzinduliwa lakini ili liweze
kufanya kazi linahitaji kuboreshwa na kulikuwa kunahitajika kiasi cha shilingi
milioni (20,000,000/=) Mhe. Kijuu
aliamua kuendesha harambee ambapo wadau mbalimbali na watumishi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Karagwe kwapamoja walichangia
katika harembee hiyo.
Katika harambee hiyo zilipatikana
fedha taslimu 2,710,000/=, hundi shilingi 1,200,000/= , ahadi shilingi
10,850,000/=, kiwanja cha kujenga ofisi za Jeshi la Zimamoto chenye thamani ya
shilingi 8,000,000/= na mabati yenye thamani ya shilingi 500,000/= kwaajili ya
kujenga banda la kuhifadhia gari hilo, jumla ya thamani yote ni shilingi 23,260,000/=.
Akiwashukuru wadau wote na
watumishi waliochangia katika harambee hiyo Mhe. Kijuu alimshukuru pia Mkuu wa
kikosi cha Jeshi la Zimamoto nchini Jenerali Thobias Adengenye kwa kuipa kipaumbele Wilaya ya Karagwe kati ya magari 9 nchini
wilaya hiyo pia nayo imepewa gari moja kutokanan na uhitaji mkubwa uliokuwepo.
Mkuu wa Mkoa pia aliwasistiza
wananchi wa Wilaya ya Kargwe kuona umuhimu wa gari la zimamoto na kulifananisha
na jeshi katika nchi yoyote wakati wa amani kwamba wananchi wanaweza kuona kama
jeshi halina kazi na linatumia fedha za bure lakini vita ikitokea kwa siku moja
huleta madhara makubwa sana kwa nchi kama moto unavyotokea na kusababisha
hasara kubwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karagwe
Mhe. Deodatus Kinawilo alisema kuwa alimua kwenda kwa Mkuu wa Jeshi la
Zimamoto nchini (Jijini Dar es Salaam)
kuomba gari la zimamoto baada ya kupata taarifa kuwa kulikuwa na magari tisa
(9) yaliyokuwa yameletwa nchini baada ya wilaya yake kukumbwa na janga la moto
katika mji mdogo wa Kayanya na kuunguza soko kuu ambapo vibanda 117 viliungua na kuteketea mapema
mwaka huu 2016.
Matukio makubwa ya moto
yaliyowahi kuikumba Wilaya ya Karagwe tangu mwaka 2014 ni shule ya Sekondari ya
St. Peter Clever bweni liliungua na kuteketea, mwaka 2015 Shule ya Sekondari
Kayanga bweni la wavulana liliungua na kuteketea, mwaka 2016 vibanda 117 vya
soko kuu la Kayanga viliteketea kwa moto pamoja na makanisa mawili kuchomwa
moto.