Bukobawadau

KANALI MKISI AANZA KUSHUGHULIKIA KERO ZA USHURU WA MAZAO KWA WAKULIMA WADOGO KASULU



Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Kanali Martin Mkisi akiongea na wakulima wadogowadogo wanaosafirisha mazao yao ya chakula kutoka mashambani mwao wakati alipokutana nao njia akiwa katika ziara vijiji vya Kata ya Kagera Nkanda.



Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Martin Mkisi (mwenye sare za jeshi) akiongea na viongozi wa vijiji vya Kagera Nkanda, na kutafuta ufumbuzi wa kero za wananchi katika vijiji vyao.


Viongozi wa vijiji vya Kata ya Kagera Nkanda, pamoja na wakuu wa idara mbalimbali wa halmashauri ya Wilaya wa Kasulu, wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa wilaya.
***************
Na Father Kidevu Blog, Kasulu
 MKUU wa Wiaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Kanali Martin Mkisi amepiga marufuku usafirishaji wa mazao nyakati za usiku na kuagiza wakulima wadogo Wilayani humo kutotozwa ushuru wa mazoa na badala yake ushuru huo utozwe kwa wakulima wakubwa pekee.

Kanali Mkisi alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza kwa nyakati tofauti alipofanya ziara katika ya Kagera Nkanda na vijiji vyake kutatua kero hiyo ya ushuru wa mazao iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa maeneo hayo kwa muda mrefu.

Mkisi aliyeambatana na watendaji wengine wa serikali Wilayani humo, akiwepo Mkurugenzi wa Hamashauri, Katibu Tawala Wilaya pamoja na Mwekahazina wa Wilaya na maafisa wengine.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza viongozi wa vijiji vyote kuweka utaratibu wa kuwatambua wakulima wadogo katika maeneo yao ili kupata vibali vitakavyowaruhusu kusafirisha mazao yao kutoka shambani hadi nyumbani bila kulipa ushuru.

“Wakulima wadogo wote watambuliwe na serikali za vijiji ili kupata vibali vitakavyowaruhusu kuondoa mazao yao mashambani bila kulipa ushuru, ni dhahiri ushuru huu ni kero ya muda mrefu kwa wakulima hawa wadaogo ambao hulima mazao yao ya chakula na si ya biashara,”alisema Kanali Mkisi.

Pia amewataka wakulima wakubwa wa kilimo cha biashara waishio mjini na kulima vijiji vya Kagera Nkanda waendelee kutoa ushuru kwa mujibu wa sheria namba 9 kifungu cha 7 ya mapato ya mazao na kupiga marufuku usafirishaji wa mazao usiku. 

Kanali Mkisi pia amewataka watendaji wa Vijiji kuboresha namna ya usimamizi na udhibiti wa mapato na kuahidi kushirikiana nao katika kuboresha. 

“Ninaamuru kwamba matumizi ya mapato lazima yaelekezwe kwenye huduma za kijamii, maji,afya, elimu, miundombinu… hususan maboresho ya barabara korofi ya kutoka Kasulu mjini hadi vijiji vya Kagera Nkanda ambayo tayari ina mkandarasi kwaajili ya matengenezo,”aliongeza Kanali Mkisi.      
                      
Mkisi pia ameagiza mazingira ya kufanyia kazi kwa wakusanya ushuru wa mazao na mapato mengine kuboreshwa mara moja huku akiagiza wataalam wa kodi kufika maeneo yote ya vijijini na kutoa elimu ya ulipaji kodi kwa wananchi.

Kero ya wakulima wadogo kutozwa ushuru wa mazao watokapo kuvuna mazao yao hasa katika vijiji viliovyopo katika Kata ya Kagera Nkanda ilikuwa ni ya muda mrefu na imekuwa ikileta usumbufu kwa wananchi.