Bukobawadau

KUHUSU ZAAKAATUL FITWR

ZAKATUL FITRI , ambayo pia hujulikana kama Sadaqatul Fitri , kilugha inatokana na neno la kiarabu fitri na maana yake ni kula.
Kwa mujibu wa sheria ya kiislamu Zakatulfitir ni ile sadaqa inayotolewa mwishoni mwa mwezi wa Ramadhan na kabla ya kusaliwa Eid na kupewa wanaostahiki
Ndugu zangu waislamu Mwezi Mtukufu wa Ramadhani sasa unaelekea mwisho, na hapa ndo pahala muhimu ambapo muislamu anaeyewajibika kutoa zakatul’fitr anapaswa kuitoa
ULAZIMA WA SWADAQAH HII
Zakatul Fitri ni wajibu kwa kila muislam awe mwanamke au mwanamme ,mkubwa au mdogo ,almuradi ana uwezo wa kuitoa au kutolewa kwa niaba yake ikiwa yuko anaemuangalia. Zakatulftri imefaradhishwa na maneno ya Mtume Muhammad kama alivyosimulia ‘Abdullah Ibn ‘Umar, Allah awawie radhi(yeye na baba yake), kwamba Mtume Muhammadi amesema :
Amefaradhisha Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam Zakatul Fitri katika Ramadhaan kwa kila mtu miongoni mwa waislamu huru na mtumwa, mwanamke na mwanamme, mdogo na mkubwa kutoa pishi moja ya tende au pishi moja ya uwele, Na akaamrisha kutolewa kabla ya watu kutoka kwenda kusali (Eid) (Bukhari)
Kwa mujibu wa hadithi hii, Zakatul Fitri itabidi itolewe kwa waislamu wa aina zote bila ya kujali hali, jinsi na mazingira ya muislamu husika pindi uwezo ukiruhusu na huyu muislamu kuushuhudia mwezi mtukufu wa Ramadhan.Uwezo unaokusudiwa ni kwa muislamu kuweza kuwa na vya kujitolesheza katika siku ya eid na bado kuwa na cha ziada.
Kwa hivyo kama muislamu ni mwenye jukumu la kuwahudumia wengine kwa mahitaji yao ya lazima basi ni wajibu kwa mtu huyo pia kuwatolea wale wote ambao wako chini ya jukumu lake katika kuwahudumia. Hii ni kutokana na ufafanuzi uliotolewa na Sahaba Abu Saeed Al Khudhriy ,Allah amuwie radhi, pale aliposema -:
“Tulikuwa tukitoa enzi za Mtume Muhammadi swalallahu alaiwasalama tulikuwa tukitoa pishi moja ya nafaka au pishi moja ya tende au pishi moja ya uwele au pishi moja ya zabibu.” (Bukhari na Muslim)
Kwa mfano kama mtu ana mke na watoto watatu,na pia mtoto wa dada yake ambaye anamlea na kumshughulikia na mama yake mzazi;
Ni wajibu kwa mtu huyo kutoa Zakah kwa nafsi yake mwenyewe kwanza na kisha hawa watu watano ambao wako chini ya dhamana yake.
KWANINI ZAKATULFITWI NI FARADHI?
Kuna mambo mengi yamezingatiwa katika kulazimisha waja wa Mwenyezimungu kutoa sadaqah hii nayo ni
1. kuondoa tabaka lililokuwepo kati ya matajiri na maskini kwani kila mtu hupaswa kujitolea yeye mwenyewe na pia wale wote wanaomtegemea na sadaqa hiyo kwenda kwa maskini na mafakiri.
2. Sweadaqa hii ujenga na kuimarisha mahusiano ya karibu kati ya aliyekuwa nacho na yule ambae hana kitu hasa kwa ile siku ya furaha ambayo waislam wote hutakiwa kufurahi, na pia kuwafunza wale wenye nacho kuwaangalia sana wale ambao hawana.
3 Inatoa nafasi kwa wale ambao wamefunga na katika funga zao walifanya baadhi ya makosa madogo madogo ambayo yanaweza kuathiri kukubalika kwa funga zao kuisafisha.
Imepokewa kutoka kwa Sahaba ‘Abdullah Ibn ‘Abbass, Allah amuwie radhi, kwamba:-
“Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam amefaradhisha Zakatul Fitr kwa wale waliofunga ili iwatoharishe na yale mambo ya kipumbavu na maneno machafu (waliokuwa wakifanya na kuongea wakati wa kufunga) na pia kwa wale maskini wapate kulishwa. Yoyote mwenye kuitoa kabla ya sala basi hiyo ni Zakah iliokubalika , na mwenye kuitoa baada ya sala itahesabika kama ni sadaqa miongoni mwa sadaqa” ( Abu Daaud, Ibnu Majah na Ad daaru Qutniy)
4 Kuendeleza malezi ya kiroho miongoni mwa waumini hasa kwa kuiangalia mali katika mtazamo wa kutoa sadaqa, msaada na kuwa wakarimu ikiwa ni moja katika njia ya kumshukuru Allah Mwenyezimungu kwa neema hii.
HUKUMU YAKE .
Wajibu huu ni wa muda maalum tu na mtu kwa bahati mbaya akikosa kutoa katika muda wake uliopangwa atakuwa ametenda kosa ambalo atapaswa kurudi kwa mola wake kutubu na kuomba maghfira.
Na mwenye kuacha kuitoa kwa makusudi ilhali ya kuwa na uwezo afahamu kwamba hili ni kosa na dhambi kubwa inayohitaji kurudi kwa mola na kutubu kwani kutotekeleza wajibu ni kuasi amri ya Allah Subhaanahu Wata’aala na Mtume wake . Na wajibu wowote katika sheria ukiachwa basi ni jukumu la asietekeleza kulilipa kama vile muislamu akiikosa sala ya fardhi au funga ya Ramadhaan. Hivyo wajibu wa kuitoa utabaki pale pale licha ya kutekeleza toba ila utoaji wa Zakah hii baada ya muda utakuwa katika hali ya sadaqa na si Zakah tena.
MUDA WA KUTOLEWA
Muda wake ni tokea kutua kwa jua katika siku ya mwisho wa mfungo wa mwezi wa Ramadhan mpaka wakati watu wanapotoka kwenda kusali sala ya Eid.
Hata hivyo Maulamaa wamekubaliana kwamba Zakah hii inaweza kutangulizwa kabla ya muda wake kama walivyokuwa wakifanya masahaba yaani siku kadhaa kabla ya mwezi kuandama wa kuisha kwa Ramadhani. Na hata kwa yule ambaye kwa njia moja au nyengine hakubahatika kutoa Zakah katika muda wake bado anapaswa kutoa sadaqa kama alivyobainisha Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kupitia kwa Ibnu ‘Abbaas Allah awawie radhi (yeye na baba yake) kwamba:
“Mwenye kuitoa kabla ya Sala basi hiyo ni Zakah iliyokubalika na mwenye kuitoa baada ya sala basi hiyo ni sadaqa miongoni mwa sadaqa.”(Imepokewa na Abu Daaud)
WANAOSTAHIKI KUPEWA
Ni waislamu maskini na mafakiri wasiojiweza ili na wao wapate kufurahi katika siku hii.(Hii ni rai iliyowafiki kwani pia kuna rai kwamba wapewe wale watu wanane wanaostahiki kupewa Zakah ya mali). Pia hupaswa kutolewa kwa wasiojiweza waliopo katika nchi/mji wa anaetoa. Kwa mfano mtu yupo hapa tanzania au mkoa wowote au pahala popote, Zakatul fitri itolewe kwa waislamu wasiojiweza wa hapa hapa. Ila tu Maulamaa wamejuzisha kupelekwa nchi nyengine ikiwa shida na mahitaji yao huko ni kubwa na nzito.
WASIOSTAHIKI KUPEWA
Kila muislamu ambae mtoaji ana wajibu wa kumhudumia na kumuangalia. Kama mzazi, mke, mtoto na kadhalika.
Ama ikiwa kuna jamaa wa karibu na ambae hana jukumu la kumhudumia; huyo anaweza kupewa Zakatul fitr ikiwa ni miongoni mwa masikini na mafakiri wasiojiweza. Na ni awlaa (vizuri) zaidi kama Zakah hii atapewa jamaa wa karibu.
KINACHOTOLEWA
Tulieleza kuwa, Kila aliyefunga Mwezi wa Ramadhaan mwenye kumiliki chakula cha kumtosha kwa muda wa siku moja, inamwajibikia kutoa Zakaatul Fitwr, nayo ni pishi ya tende au pishi ya ngano au pishi ya shaiyri na kwa upande wetu ni mchele. Anatakiwa atowe kwa ajili yake na kwa ajili ya kila anayemtegemea kama vile wanawe, wakeze, wazazi wake, watumishi, nk. na kuwapa masikini ili nao wapate kufurahi katika Siku ya Sikukuu.
Kwa vipimo vya kisasa ukilinganisha na pishi moja mbayo iliyokuwa ikitumika wakati wa Mtume Muhammadi (S.A.W) ni mchele kiasi cha kati ya kilo 2.5 na kilo 3, kwa upande wetu wa kutumia chakula hiki. (kuzidisha ndo kheri katika kuondoa mashaka).Zakaah hii ni wajibu kwa kila Muislamu mdogo na mkubwa, mwanamume au mwanamke.
Pamoja na hali ngumu iliyopo tujitahidi kuhakikisha tunawanusuru watu ambao nao wanahitaji kusherehekea siku kama ya IDD, baadhi ya waislamu wamezoea kwenda kusali Idd huku wakiwa wamebeba pesa na au nafaka kwaajili hiyo, lakini la ajabu wanajikuta mpaka swala inaswaliwa na kuisha hajapata wakumpa na hivyo kutoa kwa yeyote na baada ya swala. Jambo kama hili linakuondoa kupata Baraka na malipo ya aliyetoa zakatul’fitr badala yake unapata malipo ya swadaqa ambayo hayataisaidia funga yako juu ya makosa madogomadogo uliyoyafanya katika kipindi chote cha swaumu.
Katikawajibuwamtoaji, inambidi azingatie sana misingi ya ugawaji hasa kujua ni watu gani wanastahili kupewa, tukiangalia maneno yake Mtume Muhammadi yaliyopokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaasradhiza Allah ziwejuuyake, amesema: Mtume Muhammadi (S.A.W) alifaridhisha Zakaah ya Fitwr kwa ajili ya kumtakasa aliyefunga kutokana na dhambi ndogo ndogo zamazungumzo na matendo, na ili wafaidike masikini. Atakayeitoa kabla ya Swalaah (ya Idi) inakubaliwa kama Zakaah ya Fitwr na atakaye itoa baada ya Swalaah inakubaliwa kama Swadaqah ya kawaida. (Abu Daawuud – IbnMaajahna Ad-Daaraqutniy).
Hapa tunaona umuhimu na malengo la zakkah, hivyo tuwape zakatul’fitr masikini na mafuqara, ikiwa jamii haina watu wa sampuli hii, basi inafaa kuwapa wale wale walioelezwa na Mwenyezimungu katika surat TAUBAH (9:60) ambao ni wakusanyaji wa zakkah, wenye madeni,viongozi na waendeshaji wa dini ya Mwenyezimungu, wasafiri na wengine.
Wote hawa usipowapa chochote ili wakitumie katika siku ya IDD inaweza kuwa siku ya Idd kuwa ni siku ya uzuni hali ya kuwa Mwenyezimungu amefanya siku hiyo iwe ya furaha na watu walishane na wasaidiane katika kheri katika kusheherekea siku ya Idd.
Asli yake hutolewa chakula kile ambacho ni maarufu katika mji/nchi kwa mujibu wa hadithi tulizozibainisha hapo juu . Enzi za Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kulitolewa tende na uwele (aina ya mtama). Hivi vilikuwa vyakula maarufu. Na wakati huo pesa zilikuwepo.
Ama kutolewa pesa badala yake ni suala ambalo Maulamaa wametofautiana na kauli ya Jamhuur Ulamaa ni kwamba haipaswi kutolewa pesa. Sheikhul Islam Ibnu Taymiyah amejuzisha kutolewa pesa kwa sharti kwamba kutakuwa na maslaha makubwa zaidi kwa anaepewa kuliko akipewa chakula au nafaka.
Zinaweza kutolewa pesa kwa mfano hapa Tanzania kisha hao watakaokabidhiwa ni kwenda kununua vyakula na kuwapa wanaostahiki nafaka.
Tumuombe Allah Subhaanahu Wata’aala atuwafikishe katika kuitoa Zakah hii katika wakati wake inshaallah. Na azitoharishe funga zetu kutokana Zakah zetu. Na pia tuitoe kwa ikhlaasi huku tukitaraji malipo kutoka kwake Subhaanah.
Nawatakia Ramadhani njema.
Swed Twaibu Swed – Mwenyekiti Mtendaji
Tanzania Charitable and Development organization(TCDO)
Email swedtwaibu@yahoo.com
Next Post Previous Post
Bukobawadau