SERIKALI YATOA MSIMAMO WAKE KUHUSU BENKI YA TWIGA BANCORP
Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu msimamo wa Serikali kuhusu Benki ya Twiga Bancorp. Kulia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Cosmas Kimario na Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala, Amina Lumuli.
Maofisa wa Benki hiyo wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.
Mpiga picha za magazeti Loveness Benard akiwa kazini ' hapana kuchezea kazi hapa kazi tu'
..............................................................................
MSAJILI wa Hazina Ndugu Lawrence Mafuru ametolea ufafanuzi taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari kuhusu msimamo wa Serikali kwa Benki ya Twigabancorp.
Taarifa hiyo ilieleweka vibaya kuhusu msimamo wa Serikali kwa benki hii ya Twiga Bancorp. Naomba nieleze kwamba kwa hivi sasa Serikali inasubiri mapendekezo ya kitaalamu yatakayowezesha kutatua changamoto za kimtaji za Twiga Bancorp.
Ninaposema changamoto za kimtaji sijasema kwamba benki hiyi ipo kwenye hali mbaya ya kushindwa kujiendesha, ila inahitaji nyongeza ya mtaji kwa ajili ya kutekeleza matakwa ya kisheria na vilevile kuimarisha na kusambaza huduma mbalimbali katika maeneo ya nchi. Hatua hizo zinafuatia agizo la Mheshimiwa Rais kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipangokufuatilia utendaji wa benki ya Twiga Bancorp na kuhakikisha kasoro zilizopo zinatatuliwa.
“Kuna njia mbalilimbali za kuiwezesha benki kupata mtaji ikiwemo nje ya utaratibu wa Serikali, ndiyo maanaWizara na Ofisi ya Msajili wa Hazina ikishirikiana na Manejiment ya Twiga Bancorp zinaandaa mapendekezo yatakayoiwezesha Benki hii kupata mtaji ili kuiwezeshakutimiza malengo yake ya kiukuaji na kujiendesha kwa faida.”
Hatua mbalimbali zilianza kuchukuliwa na Wizara ya Fedhana Mipango na ofisi ya Msajili wa Hazina kwa ajili ya kuboresha utendaji wa Benki ya Twiga Bancorp. Kwa mfano, mnamo mwaka 2015, Muundo wa Shirika ulibadilishwa ambao pamoja na mambo mengine ulipelekea kuteuliwa kwa Menejimenti mpya, kwa kupitia Menejimenti hiyo mpya umetengenezwa Mpango Mkakati wa miaka mitano ambao umeanza kutumika Januari 2016, serikali pia ilifanya mabadiliko katika bodi ya wakurugenzi kwa kuteuaBodi mpya ya Wakurugenzi.
Kwa ujumla kuna mabadiliko makubwa ya kiutendaji baada ya hatua hizo kuchukuliwa. Kwa mfano benki imeweza kupata Hati Safi ya Mahesabu (Unqualified Opinion) kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Heasabu za Serikali kwa mara ya kwanza kwenye hesabu zake za mwaka 2015 jambo ambalo halikuwezekana toka Mwaka 2011.
“Hizi taarifa zinazosambaa kuwa benki inafungwa sio za kweli. Kwenye benki kuna pesa za wananchi, kuna mikopo iliyotolewa kwa watu mbalimbali, kuna rasilimali za benki ikiwemo rasilimmali watu. Yote hayo yana Utaratibu wake wa kuyasimamia.. Hata ukisikiliza hotuba ya Rais hakusema funga benki ya Twiga Bancorp aliagiza hatua zichukuliwe na kwamba Katibu Mkuu asimamie.”
Hivyo tuna wahakikishia kuwa fedha za wananchi zilizo katika benki ya Twiga Bancorp zipo salama na kwamba uongozi uliopo hivi sasa unaendelea kushughulikia changamoto za kiutendaji zilizokuwepo na kama yalivyokuwa maagizo ya Rais hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa kwa ajili ya kuhakikisha mambo yote yanakuwa sawa. Pia benki hii inaendelea kutoa huduma zake kwa wateja kama kawaida.”
Mwisho, Serikali itaendelea kutoa msukumo kwa benki hiiili kuhakikisha tatizo lililopo sasa la mtaji linatatuliwa na kuhakikisha inajiendesha kwa faida.