MAALIM SEIF AZUNGUMZA NA WAZANZIBARI BOSTON
Na Mwandishi wetu Boston
Karibuni wapenzi Wasomaji wetu katika sehemu ya nne ya mfululizo wetu wa makala ya "Maalim Seif azungumza na Wazanzibari Boston" katika mkutano wake na Wazanzibari uliofanyika katika jimbo la Massachusetts, Marekani 30 Julai 2016.
Katika sehemu iliyopita, Maalim Seif alielezea kile kilichotokea katika uchaguzi wa Oktoba, 2015 mpaka uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, 2016. Sasa endelea na sehemu ya nne:
Baada ya Uchaguzi wa Marudio
Kile kinachoitwa uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar, hakikupata uungwaji mkono tangu ndani hadi nje ya visiwa hivyo. Jamii ya Kimataifa ilikataa kushiriki katika uangalizi wa uchaguzi huo kwa vile haukuwa na mashiko yoyote ya Uhalali.
Na kwa upande wa ndani, Chama Kikuu cha upinzani Cha Wananchi (CUF) ambacho kiliususia uchaguzi huo hakikuitambua serikali mpya iliyoundwa na Mheshimiwa Ali Mohammed Shein, na kikaamua kuisusia kama kilivyoususia uchaguzi wenyewe.
Maalim Seif alisema kuwa wananchi wa Zanzibar wameigomea serekali hiyo na sasa iko taabani, na kusisitiza: "Na wala hatushirikiani nayo kwa jambo lolote lile" Aliendelea kuelezea kuwa CUF walikaa kimya kwa muda, jambo ambalo liliwafanya viongozi wa chama Tawala cha CCM waamini kuwa wamemaliza Simba wa Nyika. "Tulikaa kimya kwa muda na wao wakadai CUF tumeimaliza......, mpaka tulipoanza ziara za Wilaya mbalimbali Unguja na Pemba zikifuatiwa na kuwatembelea wagonjwa..."
Ni vizuri kukumbusha kuwa Maalim Seif alianza ziara zake hizo kwa kuzitembelea wilaya za Pemba ambako alipokelewa na halaiki ya wananchi waliokuwa wakisema "raisi..raisi...raisi". Kufuatia ziara hizo aliitwa Makao Makuu ya Polisi Zanzibar na kuhojiwa kwa muda wa masaa kadhaa.
Mgomo wa wananchi umeimarika, na umekuwa ukiitikisa serikali na kupelekea ukamataji ovyo wa wananchi kinyume na sheria: "Wameghumiwa, mgomo wa wananchi umeshika kasi...., wakaanza kukamata watu kinyume cha sheria" alisisitiza Maalim Seif.
Badala ya kushughulikia maendeleo ya nchi, serikali imejikita kwenye mikakati ya kuimaliza CUF na wafuasi wake. Hata hivyo, mikakati hiyo imekuwa ikiwaathiri wananchama wa CCM pia. Alitoa mfano wa sakata la kukamatwa ng'ombe na wenyewe kutakiwa kwenda kuwagomboa.
"Kila wanachofanya ni kuwamaliza CUF, lakini ukweli ni kwamba wenye ng'ombe wengi ni wanachama wa CCM", alisema . Maalim Seif aliendelea kufafanua juu ya dhulma wanazofanyiwa raia na mali zao na kutoa mfano wa "jumba la treni", kwa kusema "Watu walihamishwa, kwa ajili ya ukarabati wa jengo lile, na mpaka leo hata ramani haipo" Itakumbukwa kuwa michoro ya kile kinachodaiwa kuwa ni ramani mpya ya mwonekano wa jengo hilo litakavyokuwa ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, lakini kwa mujibu wa maelezo ya Maalim Sif, ilikuwa ni kiini macho tu.
Aidha Maalim Seif alifafanua kuwa Mji Mkongwe ni sehemu ya Turathi za Kimataifa. Kwa hivyo uvunjaji wa jengo lolote la kihistoria unapaswa kupata ridhaa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni. Hata hivyo, mpaka wakati tunaingia mitamboni hakuna karatasi yoyote inayoonesha kuwa tayari Serikali ya Zanzibar imewasiliana na kushauriana na shirika hilo. Kwa hivyo ni wazi kuwa uhamishwaji wa wanachi kutoka jengo la treni ulikuwa na malengo ya kisiasa na kuwadhalilisha wananchi.
Upande wa Tanzania.
Kwa vile Tanzania ni Jamhuri ya Muungano nchi mbili huru Tanganyika na Zanzibar, yanayotokea upande mmoja yanaathiri upande mwengine wa Muungano huo kwa njia moja au nyengine. Kwa hivyo, Makamo wa Rais Mstaafu wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, hakusahau kuigusia hali ilivyo nchini Tanzania chini ya Utawala wa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. Maalim Seif aliilezea hali ilivyo nchini Tanzania kisiasa kuwa si yakuridhisha, na serikali iliyopo madarakani inaipelekea nchi pabaya.
Maalim Seif alikosoa hatua ya kuzuiliwa vikao vya Bunge kuonehswa moja kwa moja kwenye televisheni, na kusema lengo lake kuu ni kuua upinzani. Hii ni kutokana na kuwa Bunge lenye mijadala huru ndilo linalojenga upinzani.
Akakosoa hatua ya Wabunge 11 wa upinzani kuzuiliwa kushiriki katika vikao vya Bunge bila ya sababu yoyote ya kimsingi: "Nini kosa lao?, alihoji Maalim Seif, na kujibu mwenyewe kuwa: "Kosa lao kubwa ni kuikosoa Serikali".
Alielezea masikitiko yake kuwa majimbo ambayo Wabunge wao wamezuiliwa yatakosa uwakilishi Bungeni kwa muda mrefu kwani wengine wamefungiwa mpaka mwezi wa Januari mwakani.
Akijibu swali iwapo kuna Mbunge yeyote wa CUF kati ya 11 waliofungiwa, Maalim Seif mwenye upeo wa kuona mbali alisema kuwa hakuna Mbunge yeyote kutoka chama hicho kati ya hao walioathirika na hatua hiyo na kusisitiza: "Nia ni kuugawa upinzani, ili waseme kuwa CUF ni wasaliti"
Alifafanua kauli hiyo kwa kusema kuwa kuna Wabunge wengi wa CUF ambao ni wasemaji wazuri na wakosoaji wakubwa wa Serikali, lakini hawakufungiwa ili watu wenye nyoyo dhaifu waone kuwa CUF ni wasaliti, au vibaraka.
Aidha, mwanasiasa huyo shupavu, aliifananisha hali ilivyo Bungeni na uwanja wa vita kutokana na kuwepo kwa askari wengi ambao mara kadhaa wamekuwa wakiingia ndani ya Bunge."Ukienda Bungeni utadhani uwanja wa vita", alisema.
Alitoa mfano wa nchi kama Uturuki amabko kumetokea mitafatuku Bungeni, lakini hakuna Polisi aliyeingia ndani ya Bunge. Halkadhalika Maalim Seif alielezea wasiwasi wake mkubwa juu ya matumizi mabaya ya Sheria ya Mtandao (Cyber Act) nchini Tanzania.
Aliendelea kwa kuelezea kutoridhishwa kwake na jinsi rais Magufuli anavyoingilia kazi za Mawaziri wake, akitoa mfano wa matamshi ya vitisho aliyoyatoa Mheshimiwa Magufuli dhidi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukhusu tangazo lao la kutisha mikutano ya nchio nzima mnamo tarehe mosi Septemba. "Swali kama hilo umwachie Waziri wako wa Mambo ya Ndani kuingiulia", alisema Maalim.
Kukhusu amri ya kuhamia Dodoma, Maalim Seif alisema kuwa hakuna umuhimu wowote wa kuhamia Dodoma kwa lazima, na kukosoa kauli za vitisho za rais Magufuli dhidi ya watendaji amabao hawataki kuhamia Dodoma waache kazi, na kuelezea khofu yake kuwa hakuna maandalizi ya kutosha."Maandalizi gani yamefanywa?" Alihoji Maalim Seif.
Alielezea wasiwasi wake juu ya upatikanaji wa huduma muhimu katika mji wa Dodoma: "Sote Dodoma tunaijua..., kuna watu wana watoto wanakwenda shule, halafu uwaambie wahame kwa ghafla, rais anapohama ni lazima Mabalozi wamfuate, watakaa wapi Mabalozi?" alihji Maalim Seif.
"Kwa hiyo, hivyo ndivyo Tanzania inavyoendeshwa, ninaposema uvunjaji wa haki za binadamu, siyo Zanzibar tu, bali ni Tanzania kwa ujumla" alisema na kuonya kuwa Visiwani kukichafuka, Bara pia kutaathirika" Akijibu swali kukhusu Masheikh wa UAMSHO walioko gerezani Tanzania Bara, Maalim Seif alijibu kwa kusema: "Hatukuona sababu yoyote ya kupelekwa Bara", na kendelea kuwa Mahakama ya Zanzibar ina mamlaka ya kisheria kuwahukumu watu wote wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali, bila kuwajibika kuwapeleka Bara.
Aliongeza kuwa: "Kama wana makosa, wangeshtakiwa Zanzibar", akisistiza: "Huu ni udhaifu wa serikali iliyopo, kila lisemwalo na Bara, wao hewallah" Ni vizuri kukumbusha kuwa, Masheikh kadhaa wa Jumuiya ya UAMSHO kutoka Zanzibar walikamatwa na kupelekwa Bara bila kufunguliwa mashtaka katika Mahakama za Zanzibar, jambo ambalo lilizusha mjadala wa kisheria.
Masheikh hao wanatuhumiwa kwa makosa ya kile kinachoitwa ugaidi, na kwa muda wa miaka kadhaa sasa wako rumande na wamenyimwa dhamana kwa madai eti upepelezi bado unaendelea. Hata hivyo Wazanzibari wanaamini kuwa Waumini hao hawana hatia yoyote sipokuwa msimamo wao imara wa kutetea hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano wa Tanzania, khususan ikizingatiwa kuwa walikuwa msitari wa mbele katika kutetea mamlaka kamilii ya Zanzibar wakati wa mchakato wa Katiba mpya iliyofeli ya Tanzania.