Magufuli aisifia ‘Sizonje’ ya Mrisho Mpoto, ategua fumbo la mashairi yake
Utunzi mahiri wa mashairi na ughani uliotukuka wa Mrisho Mpoto, umeligusa
sikio la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
ambaye ameeleza kuwa shabiki mkubwa wa kazi za msanii huyo hususan wimbo wake
‘Sizonje’.
Akizungumza na Mpoto jana, muda mfupi baada ya kuwasili jijini Dar es
Salaam katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Rais Magufuli
alimueleza msanii huyo kuwa anazifahamu vizuri kazi zake na kwamba anaupenda
sana wimbo wake wa ‘Sizonje’ huku akichambua baadhi ya mistari iliyomo kwenye
beti za wimbo huo.
Mpoto alikuwa msanii pekee aliyeongozana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye, Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Paul Makonda, Wakuu wote wa
Wilaya za Dar es Saalam pamoja na viongozi wengine waliofika katika uwanja huo
wa ndege kumpokea Mkuu huyo wa nchi.
“Nasikiliza nyimbo zako sana, ila huu wimbo wako wa Sizonje nimeuelewa sana
na nausikiliza kila siku, kwangu umekuwa kama wimbo wa taifa, mwanzoni nilipata
tabu kuuelewa lakini sasa hivi… aaaah, nimeuelewa vizuri sana. Halafu Sizonje
namjua, nimtaje?,” yalisikika baadhi ya maneno ya Rais Magufuli kwa Mrisho
Mpoto.
Akielezea tukio hilo lililoleta msisimko wa aina yake uwanjani hapo, Mpoto
alisema kuwa baada ya kumsikia Rais ameanza kuusifia wimbo wake alishtuka na
kujawa na furaha ya aina yake kwani kwa msanii ni jambo la thamani kubwa
kusifiwa kazi yake na Mkuu wa Nchi.
Alisema kuwa pamoja na kuusifia wimbo huo, Rais alionesha kuufahamu vizuri
zaidi baada ya kuanza kuipitia baadhi ya mistari na kuahidi kumfumbulia fumbo
lililofichwa kwenye wimbo huo watakapokutana tena.
“Unapopata thamani kutoka kwa Mkuu wa Nchi inaleta faraja sana,"
amesema Mpoto. "Kwahiyo, mheshimiwa Rais leo kuniambia kwamba yeye ni shabiki
wa kazi zangu na kwamba anapenda sana wimbo wa Sizonje, na akafunguka kwa
mistari ‘minane’ ya Sizonje ikiwa ni pamoja na ile inayosema ‘huyu mgeni
anayepitia madirishani wakati milango ipo!’ Na akaniambia siku tukikutana
ataniambia vile vyumba vitatu kwanini havifunguki,” ameongeza.
Msanii huyo amemshukuru Rais Magufuli kwa kuthamini mchango wake katika
sanaa kwakuwa anaamini kuthaminiwa ni hitaji kubwa la kila msanii.
“Kwakweli leo ni siku yenye furaha sana. Najisikia furaha sana. Asante sana
mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. Umenifanya nimekuwa na siku nzuri sana,”
Mpoto amefunguka kwa furaha.
Mwaka huu mwanzoni, Mrisho Mpoto aliachia audio na video ya ‘Sizonje’
aliomshirikisha Banana Zorro ambapo kwa muda mfupi tu, wimbo huo uligeuka kuwa
mkubwa na kufanya vizuri. Kutokana na ufanisi wa kazi zake, Mpoto ameendelea
kukubalika akipata mikataba ya ubalozi wa mashirika na taasisi kubwa nchini
ikiwa ni pamoja na mfuko wa pensheni wa PSPF.