MAONESHO YA NANE NANE MKOANI KAGERA YAZINDULIWA RASMI NA MKUU WA MKOA NA KUKEMEA VIKALI VITENDO VYA UCHOMAJI MOTO HOVYO KAGERA
Maonesho ya Wakulima ya Nanenane
ya mwaka huu 2016 Mkoani Kagera tayari yamezinduliwa rasmi na Mkuu
wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu katika uwanja wa
kilimo wa Kyakairabwa uliopo nje kidogo ya Manispaa ya Bukoba.
Akifungua Maenesho hayo Mhe.
Kijuu Agosti 3, 2016 alitembelea mabanda na bustani mbalimbali za vipando
vilivyoandaliwa na wadau mbalimbali wa kilimo, mifugo na uvuvi ambao ni kutoka
katika Mkoa mzima wa Kagera zikiwemo Halmashauri za Wilaya zote za Kagera.
Aidha Mhe. Kijuu mara baada ya
kutembelea shughuli za wadau wa kilimo, Mifugo na Uvuvi aliongea na wananchi walihudhuria katika
maonesho hayo na kutoa wito kwa wananchi ambao hawajafika katika viwanja hivyo kufika
ili kujifunza shughuli mbalimbali za kilimo cha kisasa katika kujikomboa na
umasikini kwa kutumia eneo dogo na kulima kwa tija.
Kaulimbiu ya maonesho ya Nane
Nane kitaifa mwaka huu 2016 ni “Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni Nguzo ya Maendeleo,
Vijana shiriki kikamilifu Hapa kazi tu.” Akisistizia Kauli mbiiu hiyo
Mhe. Kijuu aliwakumbusha vijana kushiriki katika shughuli za kilimo, ufugaji wa
kisasa na ufugaji wa samaki ili kujiajili na kuacha kulalamika kuwa hakuna
ajira.
Katika hatua nyingine Mkuu wa
Mkoa alitoa agizo kwa Wakuu wa
Wilaya wote wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha wadhibiti vitendo vya uchomaji moto
ambapo vitendo hivyo vimekithiri mkoani hapa kwa kuchoma mashamba ya misitu ya
hifadhi, misitu ya kupandwa na mashamba ya wananchi hasa kwa kipindi cha miezi
miwili ya Juni na Julai 2016.
Wakuu wa Wilaya waliagizwa pia
kuhakikisha wanawasimamia viongozi katika ngazi zote na kuwabaini wananchi
wanaojihusisha na vitendo vya uchomaji moto na kuwachukulia hatua kali za
kisheria aidha, Kwa viongozi ambao hawatawajibika watachukuliwa hatua kali za
kisheria wao wenyewe.
Agizo la pili la Mkuu wa Mkoa wa Kagera lilikuwa ni kuhusu Wanansiasa
kufanya mikutano katika maeneo yao na si viongozi wa kisiasa kutoka katika
maeneo mengine kwenda sehemu zisizo kuwa zao na kufanya mikutano ya kisiasa na
kuwasumbua wananchi katika shughuli zao za maendeleo ambapo Mhe. Kijuu alisema
hatakuwa tayari kuwavumilia viongozi wa namna hiyo katika mkoa wake.
Pamoja na kufungua rasmi maonesho
ya Nane Nane Mkoani Kagera pia Mkuu huyo wa Mkoa alizindua wiki ya Unyonyeshaji
Kitaifa ambayo inaadhimishwa Mkoani Kagera ambapo maonesho yake, Elimu na
ushauri vinatolewa katika uwanja huo wa Kyakailabwa na kilele chake kitakuwa ni
Julai 7, 2016.