Bukobawadau

STARTIMES YACHANGIA MADAWATI MKOANI MTWARA

 Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Bi. Anastazia Wambura (kushoto) pamoja na Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif (kulia) wakiwa kwenye baadhi ya madawati yaliyochangiwa na kampuni hiyo ikiwa ni jitihada za kuunga mkono kampeni ya kuchangia madawati nchi nzima iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John Pombe Magufuli. Zoezi hio la uchangiaji wa madawati lilifanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mtwara mwishoni mwa wiki hii.


 Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Bi. Anastazia Wambura (kushoto) pamoja na Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif (kulia) wakiwa wamekaa kwenye madawati hayo. 

 Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Bi. Anastazia Wambura (kulia) , akizungumza wakati wa kupokea madawati hayo. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mh. Dkt. Khatib Malimi Kazungu
Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif (kushoto), akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo.

Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Bi. Anastazia Wambura amepokea madawati hamsini yenye thamani ya shilingi milioni tano kutoka kwa kampuni ya matangazo ya dijitali ya StarTimes ikiwa ni jitihada za kuunga mkono kampeni ya kuchangia madawati iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John Pombe Magufuli.

Akizungumza mara baada ya hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika mwishoni mwa wiki moani Mtwara, Mh. Bi. Wambura amebainisha kuwa zoezi la kuchangia madawati ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri linawahusu watu wote na sio serikali pekee.

“Ningependa kuchukua fursa hii kuzipongeza taasisi za umma na sekta binafsi kwa mwitikio wao mkubwa wa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika kampeni ya kuchangia madawati. Wote tunafahamu ni kwa kiasi gani shule nyingi nchini zinavyokabiliwa na uhaba wa madawati jambo linalopelekea mazingira magumu ya kufundishia na kujinzia. Lakini kwangu mimi suala la wanafunzi kuongezeka sioni kama ni tatizo bali ni changamoto kwa serikali yetu na jamii kwa ujumla kuendana na mwamko mkubwa wa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shule. Kwa muda mrefu sana serikali imekuwa ikiwahamasisha wananchi wake wawapeleke watoto shule na wakafanya hivyo, sasa suala hilo tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa na vivyo jinsi walivyoitikia mwamko huo basi waitikie na wa huu wa kuchangia madawati.” Alisema Mh. Bi. Wambura

Naibu Waziri huyo aliendelea kwa kuelezea kuwa serikali ina wajibu wa kuhamasisha maendelea kwa wananchi wake kwa njia mbalimbali ikiwemo hii ya kuwasilisha maeneo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele kama vile suala la elimu nchini.

“Elimu ndio suala la msingi katika taifa lolote duniani iwe lililoendelea au linaloendelea na ndio maana kwa nchi za wenzetu wanawekeza fedha nyingi katika sekta hii. Nchi yoyote yenye wasomi wengi lazima itakuwa na maendeleo makubwa kutokana na raia wake kuelimika lakini hayo yote haya hayatowezekana kama tusipowawekea mazingira mazuri wanafunzi wetu tangu ngazi ya msingi,” alisema Mh. Naibu Waziri na kumalizia, “Ningependa kumalizia kwa kuwapongeza na kuwashukuru wenzetu wa kampuni ya StarTimes kwa kuguswa na suala hili na kuamua kuja huku Mtwara kuchangia madawati kwani huku ndiko kwenye changamoto kubwa hasa kutokana na taasisi na makampuni mengi kuwepo sehemu za mijini. Tunawashukuru sana na tunawaomba muendelee na moyo huo huo na mfike sehemu nyingine amabko makampuni mengine hayafiki.”

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa ni mdau mkubwa wa masuala ya kijamii hususani elimu kwa inafahamu umuhimu wake katika kuleta mapinduzi ya kimaendeleo.

“StarTimes ni mdau mkubwa sana wa masuala ya elimu na kwa muda mrefu tumekuwa tukisaidia shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu. Uchangiaji wa madawati ni kampeni ya aina yake iliyoanzishwa na Mh. Rais Magufuli na inahitaji kuungwa mkono kwa nguvu zote kwani yeye aliamini kabisa watanzania tunao uwezo huo ila tulikosa tu uhamasishaji. Na ni kweli uhamasishaji ndio uliokosekana kwani mara baada ya kutoa tamko hilo taasisi, makampuni, mashirikia, wananchi na watu binafsi wameonyesha mwitikio mkubwa. Hii ni dalili njema kwamba watanzania tunaweza kuleta maendeleo yetu wenyewe bila ya kungojea msaada kutoka kwa watu wa nje.” Alisema Bi. Hanif

“Leo hii tumekuja huku Mtwara kuja kukabidhi madawati haya, tunafahamu kwamba ni machache lakini yatakuwa ni msaada mkubwa kwa watoto wetu kusoma katika mazingira mazuri. Wanafunzi wanaposoma katika mazingira mazuri hupelekea kuhudhuria vipindi, kuipenda shule, kuelewa vizuri na hatimaye kupelekea kufaulu masomo yao,” alisema na kuhitimisha Bi. Hanif kuwa, “Wananfunzi wanapowekewa mazingira mazuri ya kusomea pia hutoa hamasa kwa walimu kufanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa kwani ufundishaji unakuwa ni rahisi na vivyo hivyo uelewa kwa wanafunzi. Hivyo basi, ningependa kutoa wito kwa wanafunzi wayatunze madawati haya ili yaje kuwanufaisha na wenzao watakaokuja siku za usoni na tunawaahidi kuwa tuko pamoja nao katika kutatua changamoto zinazowakabili.”
Next Post Previous Post
Bukobawadau