MWISHO MBAYA WA STRASSER RAIS WA SIERRA LIONE.
Na Luqman Maloto .
VALENTINE Strasser alipata kuwa Rais wa Sierra Leone. Wakati akiingia madarakani, aliweka rekodi ya kuwa kiongozi mwenye umri mdogo kuwahi kutokea. Hata sasa, hakuna taifa ambalo limewahi kupata Mkuu wa Nchi mwenye umri chini ya miaka 25 ili avunje rekodi ya Strasser.
Aprili 29, 1992, Strasser akiwa kijana mwanajeshi mwenye umri wa miaka 25, aliwaongoza wanajeshi wenzake kuvamia Ikulu ya Sierra Leone, wakamteka aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Joseph Saidu Momoh, wakamlazimisha kukimbia, naye akatorokea Conakry, Guinea.
Baada ya Momoh kutorokea Conakry, Strasser alijitangaza kuwa Rais wa Sierra Leone. Maisha yakabadilika, alishakuwa Mkuu wa Nchi, kwa hiyo hakutaka kuishi kwenye nyoyo za Wasierra Leone.
Hakulipa malimbikizo ya mishahara ya wanajeshi na watumishi wengine wa umma. Alifuja almasi ya Sierra Leone, kwa vile jina lake ni Valentine, basi sikukuu ya Valentine’s Day akaifanya kuwa sherehe ya kitaifa yenye mapumziko.
Strasser alikuwa na mbwembwe nyingi, mwaka 1993 katika mkutano wa Wakuu wa Serikali katika nchi za Jumuiya ya Madola, uliofanyika Limassol, Cyprus, alitinga kwa mbwembwe akiwa amevaa suruali ya jeans na fulana yenye maandishi Sunny Days in Cyprus (Siku za Jua Kali Cyprus).
Alikuwa mtu wa starehe, vurugu nyingi kwa wanawake, aliua watu wasio na hatia. Strasser alisahau kuwa ipo siku uongozi hautakuwa kwenye mikono yake, na ambacho kinaweza kumfaa ni kuishi ndani ya mioyo ya watu ili wamtetee na kumpigania baadaye.
Januari 16, 1996, Strasser alipinduliwa na msaidizi wake, Brigedia Jenerali Julius Maada Bio. Strasser akakimbilia Uingereza, akajiunga na Chuo Kikuu cha Warwick, kilichopo mjini Coventry, akaanza masomo ya sheria, akasema anataka awe wakili ili awatetee Waafrika.
Mwaka mmoja wa masomo, Strasser aliishiwa fedha, akaacha chuo. Maisha Uingereza yakawa magumu, akakimbilia Gambia nako kukawa pagumu, mwisho akarudi Sierra Leone, mjini Grafton, Mashariki ya Mji Mkuu wa nchi hiyo, Freetown.
Kazi ya kwanza ambayo Strasser aliifanya ikawa kuanzisha kichuo kidogo cha kufundisha kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama). Maisha ya chuo yakamshinda.
Baada ya kila kitu kwenda kombo, Strasser alirudi nyumbani kwa mama yake mzazi na kuishi kwenye banda la uani. Hata sasa, akiwa na umri wa miaka 49, anakunywa pombe za kienyeji mtaani. Hana hadhi yoyote kama kiongozi mkuu wa nchi mstaafu.
Strasser anaishi kama mtu tu mtaani. Mlevi na hakuna anayemjali. Hana mtu wa kumtetea wala kumpigania kwa sababu hakuishi kwenye nyoyo za watu. Strasser ndiye Mkuu wa Nchi wa zamani, anayeishi kimaskini kuliko wote duniani.
Ukiwa kiongozi na kugeuka kituko kama Strasser inawezekana kabisa. Ishi vibaya na watu wasikupende, akija mtawala ambaye hatakutambua kama mkuu uliyepita, unaweza kuishi maisha ya hovyo kama ombaomba mtaani au mnywa gongo uliyeshindikana.
Jifunze sasa kwamba ukiishi vizuri kama kiongozi, hata baada ya kutoka au kutolewa, jamii itakuenzi, itakupenda, kukupigania na kukutetea ukiwa nje ya ulingo na hutaishi vibaya. Ukiishi vibaya, utakuwa na mwisho mbaya kama Strasser. Somo hili liingie kwenye damu, lipenye kwenye mifupa.