UJENZI WA CHUO CHA KISASA CHA UFUNDI STADI VETA KAGERA MBIONI KUANZA MARA MOJA BURUGO HALMASHAURI YA WILAYA YA BUKOBA
Na:
Sylvester Raphael
Ujenzi wa Chuo cha kisasa cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kagera
wakaribia kuanza katika eneo la Burugo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba nje
kidogo ya Manispaa ya Bukoba ili kutoa Elimu au Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa vijana
wengi wanaohitimu elimu ya Msingi na Sekondari kutoka ndani na nje ya mkoa.
Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
Kagera kinatarajiwa kujengwa kwa ufadhili wa Serikali ya China, aidha, Serikali hiyo imetuma wataalam wa sekta mbalimbali
za ujenzi na tayari wamewasili mkoani hapa kuanzia Septemba 7, 2016 ili kufanya
upembuzi yakinifu wa gharama za ujenzi wa chuo katika eneo kitakapojengwa.
Wataalamu hao wanane kutoka
nchini China waliwasili mapema asubuhi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa kumsalimia
na kujitambulisha ambapo kati yao kuna Mhandisi wa masuala ya Maji, Ujenzi, na
Umeme ambao kwa mujibu wa kiongozi wao watafanya upembuzi yakinifu wa gharama
za ujenzi, katika eneo husika, mfano kuona eneo kama linafaa, upatikanaji wa
vifaa, gharama za vifaa na masuala yote yanayohusu ujenzi.
Mara baada yakuwapokea ofisini
kwake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu
aliwaeleza kuwa Serikali ya Mkoa ipo tayari kutoa ushirikiano kwao ili ujenzi
wa chuo hicho uanze mara moja . Pia liwakaribisha mkoani Kagera pamoja na kuja
kufanya upembuzi yakinifu lakini watembelee mkoa na kuona Kagera ilivyobarikiwa katika fursa
mbalimali za utalii na kiuchumi.
Chuo cha Kisasa cha Mafunzo ya
ufundi stadi (VETA) Kagera kinatarajiwa kujengwa na kuwa chuo cha mfano wa vyuo
vya ufundi nchini ambapo kitadahili wanafunzi wengi na kitakuwa na fani
mbalimbali za ufundi stadi ambazo zitakuwa zinaendana na hali halisi ya sasa ya
Sayansi na Technolojia .
Mkoa wa Kagera tangu mwaka1987 hadi
sasa hauna chuo cha (Vocational Educational and Training Authority, VETA) cha
ufundi isipokuwa kuna Kituo cha mafunzo
ya ufundi (Vocational Training Center) VTC Rwamishenye ambacho ni kimojawapo
kati ya vituo 27 vinavyomilikiwa na VETA chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi nchini.
Kutokana na VTC kagera kutokuwa
na uwezo wa kudahili wanafunzi wengi aidha, kuwa kituo cha mafunzo kisichokuwa
na wanafunzi wa kulala (bweni) na kupelekea wanafunzi ambao ni wa nje ya Manispaa
ya Bukoba kukosa elimu ya ufundi na kuishia mitaani baada ya kumaliza elimu ya
msingi na sekondari ndiyo sababu Serikali ya Tanzania iliamua kujenga chuo cha
kisasa Kagera ili kupunguza tatizo hilo.
Ni baada ya Serikali ya Awamu ya
Nne chini ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya
Kikwete kuamua kujenga Chuo cha Kisasa cha Ufundi, Rais Kikwete aliiomba nchi rafiki ya China
kujenga chuo hicho na kupendekeza kijengwa mkoani Kagera.
Aidha Mhe. Rais Kikwete alitangza
uamuzi wa Serikali ya China kukubali kujenga chuo hicho cha Ufundi Stadi Mkoani
Kagera Wakati akiongea na wazee wa Mkoa wa Dodoma katika Ukumbi wa Kilimani
tarehe 04/11/2014 na kuipongeza Serikali ya China kwa kukubali ombi lake kwa
dhati.
Wananchi wa Mkoa wa Kagera hatuna budi kuupokea mradi wa
ujenzi wa chuo hicho kikubwa cha kisasa na kitakachotoa elimu ya ufundi wa
kisasa unaoendana na sayansi na teknolojia , pia na kutoa ajira kwa wananchi wa
mkoa wetu wakati wa ujenzi na mara baada ya kumalizika kujengwa kwa chuo hicho.