Bukobawadau

UCHONGAJI KATIKA JAMII YA WAHAYA

Nchini Tanzania ukizungumzia suala la uchongaji sijui kama hutaambiwa Wamakonde na vinyago vyao. katika suala la uchongaji kwa Wahaya ni tofauti kabisa na Wamakonde. Wahaya ni wachongaji tena wazuri sana ila si wachongaji wa vinyago wala mapambo, hawakujishughulisha kabisa na hivi vitu. Wahaya wa zamani walijishughulisha na uchongaji wa zana za kazi. Walichonga mitumbwi kwa ajili ya kutengenezea pombe, walichonga mitumbwi ya kuvulia, vyombo vya kukamulia maziwa (ebyanzi), mashine za kusaga na kukoboa, zana za kutengenezea nguo (enshaimo) sahani na bakuli (Obwabya).
Vyombo hivi vilichongwa kwa ustadi mkubwa kwa kuzingatia matumizi ya chombo husika, utafiti ulifanyika na kubaini miti inayofaa kulingana na malengo ya matumizi ya chombo kinachotarajiwa kutengenezwa, Mti aina ya Mkunyu ulitumika kutengeneza mtumbwi kwa ajili ya kuvulia, lakini mtumbwi kwa ajili ya kutengenezea pombe ulitengenezwa kwa kwa mti aina ya Mjuju .
Utaalamu katika uchongaji ulikuwa umefikia hatua ya juu zaidi mpaka kutengeneza mashine tata (complex machine) kama mashine za kusaga na kukoboa. Mashine hizi zilitengenezwa kwa kutumia sehemu kubwa ya miti, magogo yaliyochongwa vizuri kwa nje kwa ndani  kuliwekwa vyuma laini kama mabati viliwekwa kwa mitindo tofauti kutegemea matumizi ya mashini.
 Mtumbwi wa kutengenezea pombe
 Mitunbwi kwa ajili ya kutengenezea pombe ilikuwa ya aina mbili tofauti, kulikuwepo mtumbwi kwa ajili ya kutengenezea togwa (kujunga) na mtumbwi kwa ajili ya kuchanganyia togwa na mtama (kusiya).
Pia jamii hii kama zilivyo jamii nyingi za kiafrika kinu ilikuwa zana muhimu kwa matumizi ya nyumbani, kwa Wahaya kinu kilikuwa kwa ajili ya kutwanga dawa na karanga. Vilichongwa vinu vya ukubwa tofauti kutegemea matumizi ya kinu.
Pamoja na uchongaji huo mkubwa pia walichonga vifaa vingine vidogo vidogo kama mipini ya; visu, majembe, mundu zana za kuchimbia viazi na vyoo. Kwa ujumla uchongaji ulikuwa sehemu ya maisha ya wahaya.
shafiabdunuru@mtaalamu.net
+255764192464
Next Post Previous Post
Bukobawadau