Simbachawene aagiza Fedha zilizotolewa kwa kaya zisizokuwa na Sifa katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kurejeshwa.
Na
Rebecca Kwandu
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George Simbachawene ameziagiza
Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa,
Miji na Wilaya kuhakikisha kuwa fedha zilizotolewa kwa kaya zisizokuwa na sifa
katika Mpango wa kunusuru kaya maskini unaofanywa kwa uratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF) kurejeshwa ili ziweze kuwanufaisha walengwa.
Mhe. Simbachawene pia amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuwasimamisha kazi
Waratibu wote wa TASAF wilaya ili kufanya uchunguzi wa jinsi walivyojihusisha
katika kuvuruga utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya maskini kwa kuandikisha
kaya zisizokuwa na sifa na ametaka wale wote watakaobainika kuhusika katika
kutenda makosa mamlaka za kinidhamu kuchukua hatua za kisheria haraka
iwezekanavyo.
Akizungumza katika mkutano
na waandishi wa habari mjini Dodoma leo, Mhe. Simbachawene amesema usimamizi
dhaifu wa mpango wa TASAF katika ngazi za halmashauri hususani Waratibu wa
Mpango wa TASAF Wilaya wasiokuwa waaminifu katika kutekeleza majukumu yao
imesababisha fedha za Mpango wa TASAF kutumiwa na watu wasiokuwa walengwa.
Waziri Simbachawene pia
amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuwachukulia hatua watumishi wa ngazi za
Kata, Mitaa na Vijiji ambao kwa namna moja au nyingine watabainika kuhusika katika
kuvuruga Mpango wa kuzinusuru kaya maskini kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Aidha, Mhe. Simbachawene
amewataka Wakuu wa Mikoa kujiridhisha katika mikoa yao ikiwa Wakurugenzi
watachukua hatua stahiki dhidi ya watumishi wasiokuwa waaminifu na kuwataka
kumpelekea taarifa hiyo ndani ya siku kumi na nne kuanzia leo tarehe
25/11/2016.
Mheshimiwa Simbachawene
ameitaja mikoa inayoongoza kwa matumizi mabaya ya fedha za Mpango wa kunusuru
kaya maskini unaotekelezwa na TASAF kuwa ni Dar es Salaam, Kilimanjaro,
Morogoro, , Shinyanga, Arusha, Kigoma, Dodoma, Arusha na Mbeya.