SHEIKH KICHWABUTA :WAZAZI WAPENI WATOTO ELIMU KUWAEPUSHA NA MIGOGORO YA MIRATHI
WAZAZI na walezi Mkoani Kagera wametakiwa kutoa umuhimu wa pekee kwa elimu ya watoto wao, ili kupunguza migogoro ya mirathi ambayo inatokea kutokana na jamii kutokuwa na elimu inayojitosheleza.
Akizungumza wakati wa mahafali ya 18 ya shule ya sekondari Kanyigo inayomilikiwa na taasisi ya Kanyigo Muslim Education Fund (Kamefu) iliyoko wilayani Missenyi, shekhe wa mkoa wa Kagera, Haruna Kichwabuta, alisema kuwa watoto watatumia elimu hiyo kujitegemea badala ya kusubiri kurithi mali za wazazi.
Alisema kuwa migogoro mingi ya watoto kugombea mirathi inachangiwa na asilimia kubwa ya wazazi kushindwa kuwapa watoto wao elimu inayojitosheleza kuajiriwa au kujiajiri.
“Elimu kwa watoto inawajengea msingi wa kujitegemea badala ya kusubiri kurithi mali za wazazi wao, lakini pia kuna umuhimu wa jamii kulinda haki za watoto yatima, maana hili ni kundi linalohitaji uangalizi wa kila mwananchi” alisema.
Aliwataka kufikiria kuanzisha kidato cha tano na sita katika maeneo mbalimbali, na kuwataka kuzingatia kutoa elimu bora kwa watoto wao, badala ya kusubiri kuwarithisha mashamba na mali nyingine.
Aidha alisisitiza umuhimu wa kulinda amani huku akiwapongeza wazazi na walezi kutoka mikoa mbalimnbali hapa nchini, waliotambua umuhimu wa kuwatafutia watoto wao elimu kwa kuwapeleka katika shule hiyo, ambayo pia inafundisha maadili ya dini ya Kiislamu.
Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo Rashid Tegeyeko, alisema kuwa wameanza kuboresha miundombinu ya shule hiyo, ili iweze kumudu ongezeko la wanafunzi baada ya kuwa na mafanikio kielimu, kutokana na juhudi za walimu.
Tegeyeko alisema kuwa shule hiyo ambayo ni chimbuko la baadhi ya wataalamu katika fani mbalimbali hapa nchini, inajivunia baadhi ya wanafunzi wake ambao wamepitia hapo, na baada ya kuhitimu vyuo vikuu wanaosomea taaluma ya ualimu, hurudi kufundisha watoto katika maeneo mbalimbali, ikiwamo shuleni hapo
mwisho
Na Mwandishi wetu
BukobaWadau Media