“SHIRIKI KUTOKOMEZA MALARIA KABISA KWA MANUFAA YA JAMII”
Zoezi la Upuliziaji wa dawa ya Ukoko Majumbani Lazinduliwa Rasmi Mkoani Kagera
Na Sylvestera
Raphael
Hiyo ni kaulimbiu ya uzinduzi wa zoezi la upuliziaji wa dawa ya ukoko majumbani kwa
ajili ya kuua mbu waenezao malaria katika Mkoa wa Kagera kwa mwaka 2017 zoezi
lililozinduliwa leo tarehe 23 Januari, 2017 katika Halmashauri ya Wilaya ya
Missenyi eneo la Kyaka na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M.
Kijuu.
Akizindua zoezi hilo Mkuu wa Mkoa alilishukuru
shirika la TBT Associates kwa kuendendelea na juhudi za kunyunyizia dawa ya ukoko majumbani ili
kupunguza tatizo la ugonjwa wa Malaria katika mkoa wa Kagera kwa muda wa miaka
kumi sasa tangu mwaka 2007.
Aidha, Mhe. Kijuu alisema kuwa Kimkoa, kiwango cha
maambukizi ya malaria kilikuwa 42% mwaka 2007. Baada ya utekelezaji yakinifu wa
afua mbalimbali za kupambana na ugonjwa wa malaria ikiwemo, matumizi sahihi
ya vyandarua, unyunyiziaji wa dawa ya
ukoko majumbani, kupima na kutoa tiba sahihi, pamoja na usafi wa mazingira kwa
ajili kupunguza mazalia ya mbu, kiwango cha maambukizi kilishuka na kufikia 9%
mwaka 2011.
Mwaka 2016, takribani wagonjwa 446,285 waliugua
malaria. Asilimia 24.5% ya wagonjwa waliohudhulia katika vituo vya kutolea
huduma za Afya katika Mkoa walikutwa na Malaria. Kwa Wilaya ya Missenyi
wagonjwa wanaougua malaria wamepungua kwa asilimia 54% kwa mwaka 2016, kwa
watoto chini ya miaka 5 wagonjwa wamepungua kwa asilimia 64% na kwa watu wazima
asilimia 45%. Hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na upuliziaji wa dawa ya ukoko
uliofanyika mwaka 2016. Alisistiza Mkuu wa Mkoa.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Kagera alitoa wito kwa wananchi
wa Halmashauri za Wilaya za Bukoba (Vijini) Ngara na Missenyi kutoa ushirikiano
kwa maafisa wanaohusika na zoezi hilo ili kila nyumba iliyopangiwa kunyuziwa
dawa ya ukoko unyunyiziwe bila kipingamizi chochote ili kufanikisha lengo
lililokusudiwa la kutokomeza ugonjwa wa Malaria.
Dk. Magesa Mratibu wa Mradi wa TBT Associate alisema
kuwa zoezi la upuliziaji wa dawa ya ukoko mjumbani kwa mwaka 2017 inaanza rasmi
tarehe 25.01.2017 kwa Halmashauri za Wilaya tatu Bukoba Ngara na Miseenyi na
litadumu kwa siku 24 na litahitimishwa tarehe 21 Februari, 2017. Aidha, nyumba 163,299
zinatarajiwa kupuliziwa dawa hiyo na kikosi cha wapuliziaji 743.
Zoezi la upuliziaji wa dawa ya ukoko majumbani
litavihusisha vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kuhakikisha linafanikiwa vizuri
kutokana na baadhi ya wananchi kuwa na mitazamo tofauti au imani potofu juu ya
dawa ya ukoko na kupelekea kuwahamsisha wananchi kutotoa ushirikiano katika
majumba yao yapuliziwe dawa hiyo.
Wito kwa wananchi wa Halmashuri za Wilaya za Bukoba,
Ngara na Missenyi ni kutoa ushirikiano ili kila nyumba iweze kupuliziwa dawa ya
ukoko ili kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa malaria unaoenezwa na mbu. Kama
zoezi hilo litafanikiwa kwa kiwango kikubwa ugonjwa wa malaria utatokomezwa na
kuwaacha wananchi kufanya kazi zao bila madahara yoyote ya mwili
yanayosababishwa na ugonjwa wa malaria