TISHIO LA NJAA BEI ZA VYAKULA HAZIKAMATIKI, WANANCHI WASHINDIA MAEMBE
NA WAANDISHI WETU-DAR/MIKOANI
UKAME, njaa kila kona. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya maeneo mengi ya nchi kukumbwa na njaa ambayo imesababishwa na kukosekana mvua muda mrefu.
Baadhi ya mikoa haikupata kabisa mvua za masika na zile za vuli, huku maeneo mengine zikinyesha chini ya wastani.
Katika maeneo hayo, kuna njaa na ukame mkali, mifugo imeanza kufa na wananchi wakishindia maembe kama mlo wao wa siku.
Wakati hali ikiwa hivyo, Serikali kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa mkoani Ruvuma wiki iliyopita, iliagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kutunza akiba iliyopo hadi msimu ujao wa mavuno.
Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA kwa baadhi ya mikoa na wilaya, umebaini kuwapo uhaba mkubwa wa chakula, huku mifugo nayo ikikosa malisho na maji jambo ambalo linazidisha uwezekano wa mifugo mingi kuendelea kufa kwa njaa.
Katika Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani na Morogoro ambako kuna wafugaji wengi, ng’ombe zaidi ya 1,000 wameripotiwa kufa kwa njaa.
Kutokana na tatizo hilo, baadhi ya wafugaji wametishia kujiua baada ya kushuhudia mifugo yao ikifa mfululizo kwa kukosa chakula.
Mmoja wa wafugaji katika Kitongoji cha Chaua, Mamlaka ya Mji Mdogo wa Chalinze, Hamisi Meya, aliliambia MTANZANIA kuwa amepoteza ng’ombe zaidi ya 100, wakati mwenzake aliyemtaja kwa jina moja la Karanga kutoka Mdaula, Bagamoyo, akipoteza ng’ombe 220 waliokufa hivi karibuni.
“Hali ni mbaya, baadhi ya wenzetu wanataka kujiua baada ya kushuhudia mifugo yao ikiteketea kwa kukosa chakula na maji.
“Kibaya zaidi, hawa ng’ombe sasa hawauziki, hawana nyama, wamekonda mno, hawawezi hata kutembea, ni hasara kubwa kwetu… sijui ni msaada gani unaweza kutusaidia, tunaelekea kurudi kwenye umasikini, tunamwomba Mungu atupe mvua ili tuponyeshe mifugo yetu,” alisema Meya.
Mfugaji mwingine, Mzee Malimingi wa Kijiji cha Gumba, alisema amepoteza ng’ombe zaidi ya 300 kutokana na ukame.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chaua, Rashid Maisha, aliliambia gazeti hili kuwa njaa imetokana na ukame wa muda mrefu ulioikumba Chalinze tangu Aprili, mwaka jana.
“Tunategemea zaidi kilimo cha mahindi ambacho kinahitaji mvua za kutosha, tangu Aprili, mwaka jana hatukupata mvua na hata mazao tuliyopanda yaliishia njiani, kilo moja ya sembe inauzwa kati ya Sh 1,600 na 1,700.
“Familia nyingi hivi sasa zinashinda na kulala njaa, ukipatikana unga kidogo watoto wanakorogewa uji, tunaomba Serikali itusaidie chakula vinginevyo baadhi ya watu wasiokuwa na uwezo watakufa,” alisema Maisha.
RIDHIWANI KIKWETE
Akizungumzia hali hiyo, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete (CCM), alikiri kuwapo njaa katika jimbo lake.
Alisema unahitajika msaada wa dharura kunusuru hali hiyo.
“Nimekuwa kwenye ziara ya kukagua jimbo langu, nimebaini hali inatisha, njaa ni tishio. Kibaya zaidi wanaochunga mifugo wamechoka sambamba na mifugo yao, bei ya vyakula inazidi kupaa zaidi.
“Tumejaribu kutafuta ufumbuzi kupitia Halmashauri ya Chalinze, tumeomba tani 1,421 za mahindi, tumefanikiwa kupata 600, kati ya hizo tani 250 tumezitawanya kwa kaya masikini sana na zilizobaki tumezisambaza sokoni zinauzwa kwa bei ya chini kidogo,” alisema Ridhiwani.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, alikiri kuwapo njaa na ukame, huku akiahidi kutoa ufafanuzi.
“Niko safarini, unaweza kuja ofisini kuanzia Jumatatu (jana), nitakuwa na nafasi nzuri ya kulitolea ufafanuzi sula hilo,” alisema Mwanga.
MOROGORO
Mkoani Morogoro, zaidi ya ng’ombe 15,000 wamekufa katika vijiji vitano wilayani Mvomero kutokana na ukame.
Katika vijiji vya Dakawa, Sokoine, Kambala, Mera na Melela, MTANZANIA lilishuhudia baadhi ya wafugaji wakilalamikia mifugo yao kuanguka na kufa baada ya kukosa chakula na maji.
Katibu wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Morogoro, Kochocho Mgema, alivitaja vijiji vilivyoathirika zaidi na ukame na idadi ya ng’ombe waliokufa kwenye mabano ni Dakawa (2,723), Sokoine (4,246), Kambala (1,328), Mera (1,284) na Melela (1,057).
Kwa upande wa Wilaya ya Kilosa, Mgema alisema zaidi ya ng’ombe 3,328 wamekufa.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji Taifa (CCWT), Joshua Lugasi, aliiomba Serikali kutangaza ukame kama janga la Taifa kutokana na hali halisi ilivyo.
Aidha wafugaji hao wameitaka Idara ya Hali ya Hewa (TMA) kutoa taarifa sahihi na kuhakikisha zinawafikia wadau kwa wakati ili waweze kufanya shughuli zao kwa tahadhari.
TAHARUKI
Baadhi ya wakulima katika maeneo ya Malinyi, Morogoro, Gairo, Mvomero na Ulanga, wamedai kama hali ya ukame itaendelea, inaweza kusababisha maafa makubwa.
Mkazi wa Kilombero, Said Timbuko, alisema ni jambo la kawaida kwa kaya kula mlo mmoja, huku mfumuko wa bei za vyakula ukizidi kushika kasi.
“Mfuko wa kilo 25 za sembe tulikuwa tunanunua Sh 18,000, sasa umepanda mpaka Sh 35,000,” alisema.
Alisema bei hiyo ya kilo hizo 25 za sembe uuzwa mjini, lakini kwa wilayani imefika hadi Sh 40,000.
MA-DC
Wakizungumzia hali hiyo, wakuu wa wilaya za Mvomero, Ulanga, Malinyi na Kilosa, walisema ukosefu wa mvua katika misimu husika ndiyo chanzo cha ukame.
Hata hivyo, wamewaomba wananchi kujenga tabia ya kulima mazao yenye kustahimili ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
ARUSHA
Mkoani Arusha, mahindi na mchele vimeadimika, huku mifugo ikidhoofu na mingine kufa.
Ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda na wanyamapori, wameanza kufa kutokana na kukosa malisho na maji baada ya mito, vijito na mabonde yenye maji kukauka.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini bei ya kilo moja ya unga wa sembe na dona katika Soko Kuu la Arusha na Kilombero, inauzwa kati ya Sh 1,600 na 1,800, wakati debe moja la mahindi likiuzwa Sh 15,000 na gunia la kilo 100 Sh 90,000 hadi 110,000.
Masoko ya Arusha na Kilombero, mchele unauzwa Sh 2,200 hadi 2,400 kwa kilo moja, huku mazao mengine kama ngano, maharagwe, mbaazi na kunde nayo yakipanda bei na kusababisha sintofahamu kwa wananchi.
Katika Kijiji cha Kitumbeine wilayani Longido, wananchi wanalazimika kubadilishana mbuzi mmoja mkubwa mwenye thamani kati ya sh 40,000 na 50,000 kwa debe moja la mahindi.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Daniel Chongolo, alionyesha hofu yake na kuomba Serikali kupeleka chakula ili wananchi wakinunue kwa bei nafuu, baada ya kuuza mifugo yao wakati huu ambao bado mifugo haijadhoofika zaidi.
Akizungumza na MTANZANIA, Mkurugenzi wa Kampuni ya usagishaji na usafirishaji nafaka ya Monaban, Dk. Philemon Mollel, alisema hali katika ghala lake ni mbaya na amebakiwa na tani 2,000 tu kiasi ambacho hakitoshelezi mahitaji.
“Kinga ni bora kuliko tiba, hali ni mbaya, tunaomba Serikali iruhusu tuagize chakula kutoka nje ya nchi ili kuokoa maisha ya Watanzania.
“Pia tunaomba kodi na ushuru wote ufutwe kwenye chakula kilichoko nchini na kile kitakachoingizwa kutoka nje na wafanyabiashara wasiwekewe vikwazo na ucheleweshaji usio wa lazima,” alisema.
Baadhi ya wakulima wa Kata ya Mang’ola wilayani Karatu, walidai upatikanaji wa chakula na hasa mahindi ni mbaya ikilinganishwa na mwaka juzi.
Mkulima Samweli Basso, alisema bei ya gunia la mahindi katika kata hiyo imefikia Sh 70,000 hadi 75,000.
DODOMA
Juma Matokeo ambaye ni mfanyabiashara mkoani Dodoma, alisema Juni, mwaka jana, bei ya mchele ilikuwa kati ya Sh 1,200 na 1,400 kwa kilo moja mkoani Shinyanga, ikiwa ni bei ya jumla huku wao wakiuza kwa Sh 1,500 hadi 1,600 bei ya rejareja.
MTWARA
Meneja wa Umoja wa Ushirika wa Wafanyabiashara wa Soko Kuu Mtwara, Said Namata, alisema wakulima wengi wameweka kipaumbele katika kilimo cha mbaazi, hivyo kusababisha kuadimika kwa zao la mahindi.
Alisema mwaka jana pekee, wakulima waliuza mbaazi kwa wastani wa Sh 3,000 na 4,000 kwa kilo moja hivyo waliacha kulima mahindi.
Naye Rajabu Hamis mfanyabishara wa Soko kuu Mtwara alisema mfuko wa kilo 25 wa unga wa sembe unauzwa Sh 40,000 badala ya Sh 27, 000 bei ya zamani.
RUVUMA
Mwananchi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema pamoja na Mkoa wa Ruvuma kulima mahindi, hatua zinapaswa kuchukuliwa, hasa maeneo ya vijijini.
Kilo moja ya mahindi inauzwa wastani wa Sh 730 na 750.
TANGA
Uchunguzi wa MTANZANIA umebaini bei ya gunia moja la mahindi Tanga mjini linauzwa kati ya Sh 95,000 hadi Sh 97,000 badala ya Sh 67,000 za awali kutokana na kuadimika.
Mfuko wa sembe wa kilo 25 ulikuwa ukiuzwa kati ya Sh 25,000 na 24,000 lakini hivi sasa unauzwa Sh 30,000 hadi 27,000 na ile ya kilo 50 iliyokuwa ikiuzwa Sh 50,000 na Sh 55,000 hivi sasa inauzwa hadi Sh 60,000.
PANGANI
Diwani wa Kata ya Pangani Magharibi, John Semkande (CCM), alisema mchele unauzwa kilo moja Sh 2,400 wakati awali uliuzwa Sh 1,600, sembe Sh 1,400 badala ya Sh 1,000 na 1,200.
Alisema sababu kubwa inayosababisha hali hiyo ni ukame ambao umechangia kukosekana kwa mahindi.
LUSHOTO
Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Malibwi wilayani Lushoto, Mwinjuma Salehe (CCM), alisema hali ya chakula si nzuri kwani unga wa sembe umefikia Sh 1,500 badala ya Sh 1,200 za awali.
Kutokana na hali hiyo, Salehe aliwataka viongozi wa Serikali wilayani humo kuwa wakweli na wawazi kuwaeleza ukweli viongozi wa kitaifa badala ya kukaa kimya na kuogopa kutumbuliwa, huku wananchi wakizidi kuumia.
KILINDI
Wakazi wa Vijiji vya Mvungwe, Kwamba, Kwekivu, Tunguli na maeneo mengine katika Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, wanakula maembe kama mlo wao wa siku.
Akizungumza na MTANZANIA juzi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Musa Semdoe, alikiri kuwapo njaa katika baadhi ya maeneo, lakini akasema wamejipanga kukabiliana nayo.
“Ni kweli njaa ipo, tumejipanga kuwapelekea mbegu zitakazovumilia ukame ili ziweze kuwasaidia kukabiliana na njaa hiyo,” alisema.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Sauda Mtondoo, alisema wilaya hiyo haina njaa kama inavyoelezwa na baadhi ya wananchi.
HANDENI
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alisema mabadiliko ya tabianchi yamesababisha wakulima kupata mavuno kidogo.
Alisema kwa wastani wilaya hiyo inazalisha tani 81,000 za mahindi, kunde na muhogo, lakini mabadiliko hayo
yalisababisha ukosefu wa mvua na kuzalisha tani 47,000 pekee.
IRINGA
Mkuu wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Asia Abdalah, amepiga marufuku utengenezaji wa pombe za kienyeji zinazotumia mahindi (komoni) ili kujihami na njaa inayotishia kuikumba wilaya hiyo.
Kwa kawaida wakulima wilayani humo huanza kuvuna mahindi mabichi kati ya Januari na Februari, lakini hali imekuwa tofauti kwani mahindi yamekauka kabla ya kuzaa.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kimala, Barnabas Nyamoga, alisema wananchi wamejitahidi kulima, lakini mazao yao yameishia kukauka.
Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto (CCM), amewataka watendaji wa kata zote za Kilolo kutoa taarifa mapema juu ya wananchi wanaokabiliwa na njaa ili waweze kusaidiwa na Serikali.
KANDA YA ZIWA
Wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, wameomba viongozi wa wilaya na mikoa yao kufikisha haraka ujumbe wa njaa Serikali kuu ili iweze kuwapatia chakula cha msaada.
Ili waweze kuweka msisitizo wao, wananchi hao walitumia mabango ya mabua ya mahindi yaliyokauka kumwonyesha Mkuu wa Mkoa, John Mongella hali halisi ya ukame.
Hali hiyo imetokana na ukame wa muda mrefu ambao umesababisha mazao yote kukauka, huku bei za vyakula zikipanda kila kukicha. Gunia la mahindi linauzwa kati ya Sh 100,000 na 125,000.
Akizungumzia hali hiyo, Mongella alisema kilio cha njaa ni kikubwa katika maeneo mengi ya wilaya za mkoa wake, hivyo aliahidi kutuma timu kufanya utafiti wa hali ya chakula.
KWIMBA
Wananchi wa Kijiji cha Mwabilanda wilayani Kwimba, wakiongozwa na Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), juzi walimpokea kwa mabua ya mahindi yaliyokauka Mkuu wa Mkoa, Mongella na kuonyesha ukubwa wa tatizo la njaa.
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mhandisi Mtemi Msafiri, alisema wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula unaotokana na ukame, hivyo kutishia uhai wa wananchi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Solwe, Joseph Nkonoki, alisema hali ya chakula kijijini hapo ni mbaya.
UKEREWE
Mbunge wa Ukerewe mkoani Mwanza, Joseph Mkundi (Chadema), ameutaka uongozi wa wilaya hiyo kuchukua hatua haraka ili kuwanusuru wananchi.
Alisema hali ni mbaya na tayari dalili zimeanza kuonekana na kuwataka viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa kuacha kuogopa kauli ya Rais Dk. John Magufuli ya kuwatumbua iwapo watasema ukweli.
Gunia la mahindi wilayani Ukerewe linauzwa kati ya Sh 105,000 na 120,000 tofauti na mwaka jana ambapo lilikuwa linauzwa kati ya Sh 70,000 na 80,000.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Estomihn Chang’ah, alisema wananchi wake wanayo akiba ya kutosha ya chakula huku akiwasisitiza kupanda mazao yanayostahimili ukame.
SENGEREMA
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole, alisema hali ya chakula si nzuri kutokana na ukame unaoendelea hivi sasa.
Aliwataka wananchi kutunza akiba ya chakula walinacho, huku akisisitiza walio na fedha kununua chakula sokoni ili kukitunza kwa matumizi ya baadaye.
ILEMELA
Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema licha ya ukame kuwapo, hali ya chakula ni nzuri kwani wakazi wote wanakwenda kukinunua soko kuu la Mwanza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk. Leonard Maselle, alikataa kuzungumzia suala hilo.
SIMIYU
Serikali mkoani Simiyu, imewahakikishi wananchi kuwa hakuna mtu atakayekufa kwa njaa, licha ya kukumbwa na upungufu wa mvua msimu huu wa kilimo wa 2016/2017.
BUNDA
Bei ya mahindi katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara, imepanda kutoka Sh 14,500 kwa debe moja hadi kufikia Sh 20,000, huku unga wa muhogo (udaga) ukipanda kutoka Sh 12,500 hadi 17,500.
Nafaka nyingine kama mtama zimepanda kutoka Sh 10,000 hadi Sh 17,500 kwa debe, wakati ulezi unauzwa Sh 30,000 kwa debe moja.
Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA, maeneo mbalimbali, unaonyesha bei ya chakula imepanda kuanzia Agosti na Septemba, mwaka jana.
Diwani wa Kata ya Nyamuswa, Fyeka Sumera, alisema wakazi wa kata yake wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula.
MUSOMA
Mkuu wa Wilaya ya Musoma mkoani Mara, Dk. Vicent Naano, alisema hali ya chakula si mbaya, licha ya mvua kuchelewa kunyesha na chakula kinapatikana sokoni.
Mbunge wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo (CCM), alisema hali ya chakula si nzuri na hatua madhubutu zinapaswa kuchukuliwa mapema.
TARIME, RORYA
Diwani wa Kata ya Kitembe, Thomas Lisa (Chadema), alisema hali ni mbaya, lakini cha kushanagza ni pale wakuu wa wilaya wanaposhindwa kuweka wazi kwa hofu ya kutumbuliwa.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Dagopa, Kijiji cha Nyambogo, Kata ya Kitembe wilayani Rorya, Elias Amara, alisema hali ya chakula ni mbaya na wanaomba Serikali ipeleke chakula cha msaada.
KAGERA
Wakazi wa Bukoba mkoani Kagera, wamesema hali ya chakula ni mbaya kutokana na ukame.
Wamesema wanategemea zao pekee la ndizi kwa chakula. Mkungu mmoja unauzwa Sh 7,000 hadi Sh 15,000.
Hata hivyo, viongozi wa wilaya na mkoa hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, huku Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Luteni Kanali Denis Mwilla, akidai jambo hilo ni zito, linahitaji takwimu kulizungumzia.
GEITA
Mkuu wa Wilaya ya Geita mkoani Geita, Herman Kapufi, alikataa kuzungumzia hali ya njaa, licha ya wananchi kuiambia MTANZNIA kuwa hali ya chakula ni mbaya.
TMA
Nayo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema msimu wa mvua wa kuanzia Januari hadi Februari, unatarajiwa kuwa chini ya wastani.
Meneja Ofisi Kuu TMA, Samuel Mbuya, alisema jana kuwa kunyesha mvua chini ya wastani kunatokana na kupungua kwa joto la bahari eneo la Ikweta.
UKUAJI KILIMO
Hivi karibuni, wakati akitoa tathimini ya ukuaji wa uchumi kwa nusu mwaka na matarajio ya hadi Juni mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliitaja sekta ya kilimo kuwa ndiyo inayoongoza kwa kukua polepole.
Alisema licha ya kilimo kuwa miongoni mwa sekta inayochangia kukua kwa pato la Taifa, lakini yenyewe inakua kwa asilimia 2.7 hadi 0.3.
KAULI YA MAGUFULI
Taarifa hizi za ukame na njaa, zimekuja siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kuhutubia wananchi mkoani Kagera na kusema Serikali yake haitatoa chakula cha msaada ili kila mtu afanye kazi.
Rais Magufuli pia aliwaonya wakuu wa mikoa na wilaya wajiandae kuwajibika endapo maeneo wanayoongoza yatakuwa na ukosefu wa chakula na kusababisha wananchi kukumbwa na njaa ilhali maeneo mengi ya nchi yamepata mvua za
akutosha.
CHANZO. Gazeti la Mtanzania
10/1/2016.