TUME MAALUMU YAELEZA CHANZO CHA MOTO ULIOUNGUZA SOKO LA KAYANGA KARAGWE
Tume maalumu niliyoundwa na mkuu wa wilaya ya Karagwe Godfrey Mheruka na kupewa jukumu la kuchunguza chanzo cha moto ulizuka katika soko la Kayanga lililoko wilayani humo na kuteketeza kabisa vibanda 52 vya wafanyabiashara katika soko hilo na meza 24 kwa pamoja vilivyokuwa mali zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 632 imekabidhi taarifa ya chanzo cha moto uliounguza soko hilo.
Akisoma matokeo ya tume iliyochunguza chanzo cha moto huo, mkuu wa wilaya ya Misenyi Godfrey Mheruka amesema kulingana na taarifa ya tume hiyo ni kwamba soko hilo lilihujumiwa kwa kuchomwa moto na baadhi ya wafanyabiashara katika soko hilo waliokuwa na migogoro na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe hivyo wala chanzo cha moto hakikutokana na hitilafu ya umeme kama ilivyodhaniwa hapo awali.
Kufuatia uchunguzi matokeo ya uchunguzi wa tume hiyo, kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera, kamishina msaidizi mwandamizi, Augustine Ullomi amesema jeshi la polisi kwa sasa limewafikisha mahakamani watu wanne ambao hakuwataja majina yao kwa sababu za kiupelelezi kwa kuwa bado jeshi hilo linawasaka watuhumiwa wengine zaidi.
Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe, Godwin Kitonka amesema kwa sasa halmashauri hiyo imewaruhusu wafanyabiashara katika soko hilo kujenga vibanda vya muda wakati wa mchakato wa ujenga soko jipya la kisasa ukiendelea, nao baadhi ya wafanyabiashara katika soko hilo wameomba wasitozwe kodi ya pango kwa sasa ili waweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha waliyonayo kwa sasa.