HOTUBA YA ZITTO KABWE JUU YA HALI YA ELIMU YA JUU NA SUALA LA MADAWA YA KULEVYA
Hotuba Yangu Bungeni Kuhusu Taarifa za Kamati za Bunge za Huduma na Maendeleo ya Jamii na Masuala ya UKIMWI
Mheshimiwa Spika, Nasimama kuunga mkono Taarifa za Kamati zilizowasilishwa katika Bunge lako Tukufu leo.
Nawapongeza sana Wenyeviti wa Kamati zote mbili na wajumbe wa kamati hizo kwa kazi nzuri waliyoifanya na kuwezesha kuwasilisha Taarifa zao, na ninalishawishi Bunge lako tufukufu kuzipitisha Taarifa zote mbili pamoja na mapendekezo yaliyomo humo.
Taarifa za Kamati ni kazi za Bunge katika Kuisimamia na Kuishauri Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Hivyo ninaamini kwa dhati kwamba Bunge litaweka utaratibu wa wazi utakaowezesha ufuatiliaji wa maoni na mapendekezo ya Kamati za Bunge kama yalivyopitishwa.
Mfumo huo kwa sasa haupo kwa hiyo wakati mwengine wabunge tunakuwa kama tunaimba kwaya au kaswida tu tunapojadili na kuazimia kuhusu Taarifa za Kamati za Bunge. Mabunge mengine duniani yana kamati maalumu ya Ufuatiliaji wa maamuzi ya Bunge. Ni matarajio yangu kwamba Wabunge wataona umuhimu wa kuwepo kwa kamati hiyo ili kuweza kutendea haki kazi zetu za Kamati na Bunge kwa Ujumla.
Mheshimiwa Spika, tumeona Taarifa ya Kamati inayohusika na Elimu na mapendekezo yake. Naunga mkono mapendekezo yote. Hata hivyo ninaomba kuongeza maudhui kidogo katika suala zima la Elimu ambalo nimelizungumzia sana katika michango yangu mbalimbali ya siku zilizopita.
Nimepata kuzungumza kuhusu kuongeza vyuo vikuu vya umma hapa nchini ili kupanua Elimu ya Juu na kuweza kuongeza uwezo wa vyuo vya umma kudahili wanafunzi. Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2016 inaonyesha kuwa katika jumla ya wanafunzi 234,506 wa vyuo vikuu nchini, wanafunzi wa vyuo vya Serikali ni 154,393. Hivyo wanafunzi wengine hubidi kwenda vyuo binafsi hata kama ni kinyume na matakwa yao na Serikali kulazimika kuwapa mikopo kuweza kumudu masomo yao huko.
Iwapo vyuo vya umma vitaweza kuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wote wenye sifa kuingia elimu ya juu, tutaongeza ushindani kati ya vyuo vya umma na vyuo binafsi na hivyo kutatua tatizo kubwa la ubora katika vyuo. Mzazi atampeleka mtoto chuo kikuu binafsi kwa sababu ya kutaka ubora na sio kwa sababu hakuna nafasi kwenye vyuo vya umma.
Mheshimiwa Spika nimepata kushauri siku za nyuma kuwa kuna haja ya kuanzisha vyuo vikuu vipya kwa umma angalau vitatu vyenye uwezo wa kudahili wanafunzi 20,000 kila chuo. Narudia pendekezo hilo tena na ninapendekeza kuwa Serikali ijenge Chuo Kikuu cha Pemba, Chuo Kikuu cha Mtwara na Chuo Kikuu cha Ziwa Tanganyika ili kupanua vyuo kwenda mikoa ya Kusini na Magharibi kwa upande wa Tanzania Bara na kuwepo na Chuo Kikuu cha Umma cha Muungano huko Pemba (Union University of Pemba).
Mfumo uliotumika kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma utumike kujenga vyuo vikuu hivi kuanzia mwaka wa fedha ujao. Vile vile Serikali ipanue uwezo wa Vyuo Vikuu vya Umma vilivyopo nchini kwa kufungua ajira kwa walimu wa Vyuo Vikuu ili kuweza kuhudumia wanafunzi wengi zaidi na kwa uwiano mdogo wa Mhadhiri kwa Wanafunzi anaowasimamia. Aina ya Uchumi tunaotaka kuujenga unahitaji uwekezaji mkubwa kwenye Rasilimali watu kwa kada zote za utaalamu. Nashauri kuwa tufanye uwekezaji huo kwa faida ya vizazi vya sasa na vizazi vya baadaye.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ninalotaka kulizungumzia ni suala la vita dhidi ya madawa ya kulevya. Kamati ya Bunge inayohusika na suala la Madawa ya kulevya imeainisha katika Taarifa yake kwamba Serikali imeshindwa kukiwezesha chombo kilichoundwa na Sheria ili kudhibiti Biashara na utumiaji wa madawa ya kulevya.
Kamati imelalamika kuwa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya kulevya wana bajeti finyu na hata hiyo Bajeti haitolewi na hivyo kusababisha Mamlaka kukosa vitendea kazi, kushindwa kutoa elimu kwa umma, kushindwa kufanya operesheni za ukamataji wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kushindwa kutoa ushauri nasaha kwa waathirika wa madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Spika, kwa siku kadhaa sasa kuna 'crackdown' (ukamataji mkubwa) ya watumiaji wa madawa ya kulevya ambapo Watanzania kadhaa na wengi wao vijana wametiwa nguvuni na jeshi la polisi kwa tuhuma kwamba ni watumiaji wa madawa haya. Watuhumiwa hawa inasemekana wameagizwa wataje wananunua wapi madawa wanayotumia kwa kuhojiwa na polisi na wengine kulazwa ndani kwa zaidi ya siku 3 bila kufikishwa mahakamani.
Baadhi ya watuhumiwa wameelezwa kuteswa na kupigwa na polisi na kulazimishwa kutoa maelezo kwa Polisi. Umma haujaelezwa kama watu hawa wamekamatwa na madawa hayo ama wamehisiwa kuwa ni watumiaji tu. Kampeni hii sasa inaendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Kuthibitisha msemo wa kiha kwamba "ukiona kifaranga kipo juu ya chungu ujue chini kuna mama yake", leo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametamka kuwa vita ile sio ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam bali ni vita ya wote. Vita ya wote kuendeshwa na Mkuu wa mkoa mmoja ni jambo la kushangaza kidogo lakini halina ubaya kwani 'lazima awepo wa kubutua kombolera'.
Mheshimiwa Spika, Katiba ya nchi yetu inamhakikishia kila Mtanzania kuwa hana kosa lolote mpaka mahakama ithibitishe ni mkosaji (Innocent until proven guilty). Hata hivyo tunachoona katika vita hii ni kana kwamba sasa nchi yetu raia yeyote ni Mkosaji ukituhumiwa tu ('guilty until accused'). Hii si sawa, tunajenga jamii ya hovyo sana na anayeongoza kujenga jamii hiyo ni Kiongozi Mkuu wa nchi kwa kubariki misingi ya mfumo wetu wa haki kuvunjwa vunjwa na watendaji wa chini yake.
Leo hii akitokea Mkuu wa Mkoa wowote anamchukia tu Mbunge katika mkoa wake, anaweza kuagiza aende kuripoti polisi kesho kwa kuhusika na madawa ya kulevya. Tunajenga nchi ya namna gani? Hii si 'Banana Republic', hii ni nchi ya Kikatiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Ninaliomba Bunge lako tukufu kuungana na Mheshimiwa Rais katika kupambana na madawa ya kulevya na kutaka mpambano huo kufuata sheria za nchi bila uonevu wowote kwa mtu yeyote, awe na jina au asiye na jina. Hata kama ni mke wa Rais anahusika na madawa, achukuliwe hatua kwa mujibu kwa sheria na sio kwa sababu mume wake kasema akamatwe. Hata kama ni mtoto wa mkubwa Fulani, achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nawakumbusha waheshimiwa wabunge kwamba vita hizi sio za kushabikia. Huu ni mtego wa panya, hujui utamnasa nani. Wajibu wetu ni kama wabunge ni kufanya yafuatayo:
(1) Kuunga mkono na kushiriki vita dhidi ya madawa ya kulevya na
(2) Kuisimamia Serikali kuhakikisha kuwa inaendesha vita hii kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi yetu.
Tusikalie kimya uvunjaji wa Katiba na misingi ya nchi yetu hata kama uvunjaji huo unaendeshwa na Amiri Jeshi Mkuu wa Nchi. Ifikie wakati tumwambie kuwa Nchi yetu haifuati Presidential Supremacy bali inafuata Constitutional Supremacy.
Nashukuru sana Mheshimiwa Spika.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini (Ujiji)
Februari 6, 2017
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini (Ujiji)
Februari 6, 2017