WABUNGE WAPAZA SAUTI KUHUSU UZAZI WA MPANGO, KUPUNGUZA VIFO VINAVYOTAKANA NA UZAZI NA KUPANGA MAENDELEO TAIFA
Asasi ya Kibunge inayojihusisha na masuala ya
Idadi ya watu na maendeleo (TPAPD) imeelezea umuhimu wa kuweka kipaumbele
kwenye masuala ya uzazi wa mpango ili kukabiliana na ongezeko la kasi la idadi
ya watu ambayo kwa sasa ni wa asilimia 2.7 kwa mwaka.
Tamko la TPAPD lilitolewa leo katika kuadhimisha siku ya
Kimataifa ya Wanawake Machi 8, limesema matumizi ya njia za uzazi wa mpango
yanaweza kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi (MMR) kwa asilimia 44, na
kupunguza vifo vya watoto kwa asilimia 35. Vifo vya wanawake katika uzazi
vimefikia 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015 kutoka vifo 454 katika
kila vizazi hai mwaka 2010.
TPAPD chini ya Mwenyekiti wake Mhe Dkt Mary Mwanjelwa
iliamua kutoa tamko hili hivi karibuni katika kikao cha kamati tendaji mjini
Dar es Salaam kilichojadili umuhimu wa uzazi wa mpango katika harakati za
kujenga Tanzania ya uchumi wa kati na uchumi wa viwanda.
Tamko hilo lililotiwa saini na Mwenyekiti Dkt Mwanjelwa
limesema:
“uzazi wa mpango unahitajika katika kuiwezesha nchi
kukabiliana na ongezeko la kasi la idadi ya watu inayochangiwa na uzazi wa
kiwango cha wastani wa watoto sita kwa kila mwanamke aliye katika umri wa
uzazi. Hali hii huchangia utegemezi pamoja na umaskini; na pia hudumaza juhudi
za taifa za kufikia malengo ya maendeleo”.
“TPAPD inatambua na kuunga mkono kwa dhati kasi
ya utekelezaji wa mpango Mkakati wa Taifa wa kuimarisha afya ya
uzazi, afya ya mama na mtoto, na vijana (RMNCAH II 2016-2020),” na inaahidi
kuwa bega kwa bega katika kufanikisha upatikanaji
wa huduma bora za uzazi wa mpango kwa wote hapa nchini”,
limesema Tamko hilo.
Mhe Mwanjelwa amesema TPAPD inatambua mafanikio
yaliyopatikana katika kulifanya suala la uzazi wa mpango kuwa nguzo
muhimu katika mpango wa taifa wa RMNCAH ambao pia unajulikana kama One Plan II,
unaolenga kuongeza matumizi uzazi wa mpango kila mwaka, kupunguza vifo vya
wanawake na watoto, na kuimarisha afya ya uzazi kwa vijana. Ifikapo 2020,
Tanzania imeweka lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kufikia 293 kwa
kila vizazi hai 100,000.
Ikitambua mchango wa wabunge wote katika kuweka mazingira
wezeshi ya kisera na kwa serikali kutenga bajeti ya uzazi wa mpango, TPAPD
imetaka jitihada za dhati ziendelee kufanyika kuhakikisha ununuzi na usambazaji
wa taarifa sahihi, njia za uzazi wa mpango, na vifaa vya kuimarisha afya ya
uzazi kote nchini.