OPERESHENI ONDOA MIFUGO KAGERA YASONGA MBELE SASA NG’OMBE WASAKWA KWA NDEGE ZISIZOKUWA NA RUBANI KILA PEMBE YA HIFADHI
Operesheni
ondoa mifugo katika Hifadhi za Misitu na Mapori ya Akiba Mkoani Kagera
yaendelea kwa kasi ambapo tangu kuanza kwa operesheni hiyo Machi 31, 2017 hadi
kufikia Aprili 7, 2107 tayari mifugo
4489 imekamatwa na watuhumiwa wa makosa mbalimbali 115 wametiwa mbaloni.
Mifugo
iliyokamatwa ni pamoja na Ng’ombe 4328, Mbuzi 125 na Kondoo 36. Pia watuhumiwa
115 waliokamatwa kwa makosa mbalimbali
Watanzania ni 109, Warundi 4 na Wanyarwanda 2. Aidha Ng’ombe 144, kondoo
17 na mbuzi 113 wametaifishwa na Serikali baada ya watuhumiwa kushindwa kesi zao
na Mahakamani kuiamurisha Serikali kutaifisha mifugo hiyo.
Serikali
ya Mkoa wa Kagera katika kuhakikisha zoezi la operesheni linafanikiwa kwa
asilimia 100% imeanza kutumika ndege zisizotumia Rubani (Drones) pia
na ndege zinazotumia Rubani ili kukagua maeneo yote ambayo siyo rahisi kuonwa
au kufikika na vikosi vya nchi kavu ambako mifugo hufichwa na wavamizi na
kuendesha shuguli za kinadamu.
Akirusha
ndege isiyotumia Rubani katika kituo Kiteule cha Nyakanazi Bw. Parmena Pallangyo Afisa Wanyamapori kutoka
Pori la Akiba la Lwikwika Lumesule lililopo Wilayani Masasi Mkoani Mtwara alisema
ndege hizo zina uwezo wa kusafiri zaidi ya Kilometa 10 kwa muda mfupi zikiwa
zinapiga picha mnato na picha za video kwa kuonesha viwianishi (coordinates) za kila eneo kila kitu kilichopo ardhini.
“Badala
ya kuangaingaka na kutumia rasilimali magari, mafuta au rasilimali watu kwenda
kutafuta mifugo katika maeneo ambayo hatuna uhakika, tunazituma kwanza ndege
hizi zinatuletea taarifa za picha na eneo walipo mifugo pia picha hizo zinakuwa
na viwianishi (coordinates) ambazo
zinatusaidia kujua eneo husika ndipo sasa vikosi vinaelekezwa eneo husika na kwa
kutumia kifaa kiitwacho GPS huwawezesha kukamata mifugo hiyo.” Alifafanua Bw. Parmena
Wafugaji
na Wafanyabiashara wa Ng’ombe wasemaje?
Katika Mnada wa
Ng’ombe wa Rusahunga ambao hufanyika kila siku ya Alhamisi kila wiki wanunuzi
wa Ng’ombe wanasema kuwa kwasasa Ng’ombe wanapatikana kwa wingi katika Mnada.
Bw. Sena Elias Magoma mnunuzi aliseam
kuwa kwa Ng’ombe aliyekuwa anauzwa bei ya shilingi 1,200,000/= wiki mbili zilizopita kwasasa anauzwa bei ya
shilingi 800,000/= hadi 700,000/= na aliyekuwa anauzwa shilingi 500,000/=
kwasasa anauzwa shilingi 300,000/= hadi 250,000/=.
Naye Bw. Fikiri
Matenya Mashine ambaye ni mfugaji
alisema kuwa katika mnada huo kwa sasa Ng’ombe ni wengi kiasi kwamba bei
imeshuka sana na wafugaji wanawarudisha ng’ombe wao nyumbani kwakukosa soko.
Akiulizwa sababu ya ngo’ombe kuwa wengi katika mnada huo wa Rusahunga kwasasa
na bei kushuka alisema;
“Mimi nadhani kutokana
na ‘parancha’
(akimaanisha operesheni) linaloendelea
huko maporini ndiyo maana ng’ ombe wamekuwa wengi katika mnada na pengine
matajiri wanasubiri mnada wa ng’ombe ambao Serikali imewakamata ili wawanunue
kwenye mnada kwa bei ya chini sana. Lakini mimi naona Serikali imefanya jambo
jema hawa Wafugaji kutoka nje ya nchi wanatunyanyasa sana kama watondoka mimi
naamini kuwa malisho yatatutosha sisi wenyeji.” Alifafanua Bw. Mashine
Aidha, Afisa Mifugo
anayesimamia Mnada wa Rusahunga Bw. Raphael Barakekenwa alisema kwa kipindi
hiki cha operesheni mifugo hasa ng’ombe wamekuwa wengi mno kiasi kwamba
wanakosa soko lakini Serikali kuu na Halmashauri zinapata mapato ya kutosha
kutokana na wingi wa ng’ombe mnadani. Pia alitoa angalizo kuwa kwa wiki mbili
au tatu zijazo huenda kukawa na uhaba mkubwa wa nyama sokoni kwasababu ng’ombe
wengi kuondolewa maporini na kusafishwa kwenda mikoani na nje ya nchi.
Vilevile katika mnada
huo Mwandishi wa habari hii alishuhudia malori mengi yakiwa yanapakia ng’ombe
kwa wingi na kuondoka kuelekea mikoani pia ng’ombe wengi wakiwa katika eneo
hilo la mnada wa Rusahunga wakisubiri kununuliwa aidha wafugaji wengine
wakiamua kurudi nyumbani na ng’ombe wao waliokosa soko katika mnada huo.