SERIKALI MKOANI KAGERA YAPOKEA VIFAA VYA KISASA KUTEKELEZA KWA UFANISI OPERESHENI YA KUONDOA MIFUGO NA WAVAMIZI KWENYE HIFADHI
Serikali
ya Mkoa wa Kagera imepatiwa vifaa vya kisasa
ambavyo ni Ndege mbili zisizotumia Rubani (Drones) na Redio Upepo ishirini
(Radio Calls) kwa ajili ya kufanikisha operesheni ya kuwaondoa wavamizi wa
misitu na mifugo inayochungiwa katika Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba na
Vyanzo vya maji ambapo uharibifu mkubwa ulikuwa unaendelea katika hifadhi hizo.
Makabidhiano
ya vifaa hivyo yalifanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera April 2, 2017
katika hafla fupi ambapo Simu 20 za upepo (Radio Calls) zenye thamani ya
shilingi 25,000,000/= (Shilingi Milioni Ishirini na tano) zilitolewa na Meja
Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Wanyamapori
Tanzania (TAWA) kutoka katika Kampuni yake binafsi ya SUN MACHNERY.
Pia
Bw. Martine Loibook Kaimu Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania alikabidhi ndege mbili zisizotumia rubani (Drones)
zenye thamani ya dola 40,000 USD (Dola
elfu arobaini) na kusema kuwa TAWA wamefurahishwa na jinsi Serikali ya Mkoa wa
Kagera ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu inavyoendelea na zoezi la
operesheni ili kunusuru Hifadhi za Misitu na Wanyamapori.
Meja
Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko naye pia alisema lengo la kutoa vifaa hivyo ni
kuhakikisha operesheni inafanikiwa kwa asilimia mia moja na vifaa hivyo vitasaidia kufanya operesheni
kila eneo la Hifadhi la Mkoa wa Kagera bila kuacha wavamizi na mifugo katika
maeneo hayo.
Kwaniaba
ya Serikali Mkoani Kagera Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Deodatus Kinawilo
ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba alivipokea vifaa hivyo na alishukuru
kwaniaba ya Serikali ya mkoa kuwa vifaa vilivyotolewa kuwa vitaongeza ufanisi
katika operesheni hiyo. Aidha Kaimu Mkuu wa Mkoa aliendelea kutoa rai kuwa
operesheni hiyo siyo nguvu ya soda bali maeneo yote ya hifadhi za Misitu na
Wanyamapori yatasafishwa ili yabakie kama ilivyokuwa awali.