Bukobawadau

TANZANIA NA UGANDA ZAKUBALIANA MASUALA MAKUU MANNE YA USHIRIKIANO KATIKA MAENDELEO NA KUTILIANA SAINI MKOANI KAGERA

Na: Sylvester Raphael
Hatimaye mkutano wa ujirani mwema kati ya Tanzania na Uganda umemalizika leo Julai 29, 2017 majira ya jioni kwa Mawaziri wa nchi hizo mbili kutiliana saini hati za makubaliano ya utekelezaji wa masuala makuu manne ya ushirikiano katika maendeleo waliyokubaliana kwenye mkutano huo wa siku moja.

Akitoa Taarifa mara baada ya makubaliano na kutiliana saini katika hati za makubaliano Waziri wa Mambo ya nje wa Uganda Mhe. Sam Kutesa alisema yeye akiongoza jopo la Mawaziri kumi kutoka Uganda pamoja na wataalam wengine wamefurahishwa sana na Mkutano huo kwani umekuwa wa mafanikio kwao.
Aidha Mhe. Kutesa alisema kuwa katika Mkutano huo wamekubaliana masuala makuu manne ambayo yanahusu Kuhakiki mipaka ya kati ya nchi mbili, pili Huduma za maji kutoka Mto Kagera, Tatu Biashara baina ya nchi mbili na nne Kuhusu suala la nishati ya Umeme.
Akitoa ufafanuzi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk.Augustine Mahiga alisema kuwa kuhusu Suala la Mipaka wamekubaliana kuongeza alama za mipaka ili mpaka uonekane vyema kati ya nchi mbili ili kuondoa migongano inyoweza kujitokeza maeneo ya mpakani kwasababu mipaka hiyo iliwekwa na Wakoloni miaka mingi iliyopita.
Pili Dkt. Mahiga lifafanua suala la Huduma ya maji katika Mto Kagera na kusema kuwa nchi ya Uganda wanayo matatizo ya maji kwa baadhi ya sehemu mpakani na Tanzania na maji yanapatika Mto Kagera kwa upande wa Tanzania kwa hiyo katika suala hilo Waganda wameomba na kukubaliana na Tanzania kujenga mabwawa na malambo kwaajili ya kunywesha mifugo yao.
 “Suala hilo tumekubaliana lakini taratibu zote za mazingira zitafuatwa ili kusijekukatokea uharibifu wa mazingira na uvujanjaji wa sheria za mazingiara.” Alisistiza Waziri Dkt. Maiga. Kuhusu suala la Biashara Dkt. Maiga alifafanua kuwa wamekualiana kuimarisha biashara kati ya nchi mbili pamoja na kuwa nchi hizo zote zipo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kuhusu Nishati ya Umeme Waziri Dkt. Maiga alisema kuwa mji wa Bukoba unapata umeme kutoka Uganda kwa hiyo Tanzania imekuwa ikipata nishati hiyo toka Uganda lakini kwa sasa Tanzania pia inatarajia kuzalisha umeme wa kutosha ambapo wamekubaliana pia kuwa mara ya umeme huo kuwa umepatikana Tanzania pia itawauzia Umeme Uganda.
Mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya ELCT Bukoba ulihudhuliwa na Mawaziri kutoka Tanzania saba pamoja na wataalam mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk.Augustine Mahiga. Aidha, kwa upande wa nchi ya Uganda uliongozwa na Waziri wa Mambo ya nje Mhe. Sam Kutesa pamoja na Mawaziri kumi wakiambatana na Wataalamu mbalimbali.
Next Post Previous Post
Bukobawadau