Bukobawadau

PROF. MBARAWA AZITAKA KAMPUNI KUTOA HUDUMA ZA MAWASILIANO SAA 24


Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigalla King (wa kwanza kulia) akifafanua jambo kwa wananchi wa kijiji cha Kweinsewa kilichopo kata ya Nkolamo, wilaya ya Korogwe Vijijini mkoani Tanga wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua ujenzi wa minara na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye vijiji. 
Bibi Mwanafuraha Nyange, mkazi wa kijiji cha ziwa Jipe kilichopo Kata ya Jipe wilaya ya Mwanga kwenye mkoa wa Kilimanjaro akieleza umuhimu wa mawasiliano vijijini kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara yao ya kukagua ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini. 


MBARAWA AZITAKA KAMPUNI KUTOA HUDUMA ZA MAWASILIANO SAA 24
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kufikisha huduma za mawasiliano kwenye vijijini vyote nchi nzima na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara ili kuchochea ukuaji wa uchumi na utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi wote, kwa wakati, uhakika na muda wote.
Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga wakati wa ziara iliyoandaliwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia UCSAF ya kuwapeleka wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kukagua maendeleo ya ujenzi wa minara ya simu za mkononi, hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi na changamoto zilizopo kwa wananchi wa maeneo husika. Wakiwa kwenye ziara hiyo kata ya Jipe iliyopo Wilaya ya Mwanga mkoa wa Kilimanjaro Eng. Ulanga amesema kuwa mnara wa Vodacom uliojengwa kwenye eneo hilo unahudumia zaidi ya wananchi 1,200 kwenye vijiji zaidi ya nane. Hadi hivi sasa UCSAF imejenga minara ya simu za mkononi kwenye maeneo saba yaliyopo Wilaya ya Mwanga na Same mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na kampuni za simu za mkononi. Vile vile, Kamati imetembelea minara iliyopo kata ya Nkalamo iliyopo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Eng. Ulanga ameongeza kuwa Serikali kupitia UCSAF inaendelea kutoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi  ili ziweze kufikisha mawasiliano kwenye vijiji vyote nchi nzima ambapo hadi hivi sasa UCSAF imetoa jumla ya dola za marekani milioni 41.5 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 93.3 kwa ajili ya kufikisha huduma za mawasiliano vijijini kwenye kata 518 ambazo zitajengwa minara ya mawasiliano. Mpaka sasa jumla ya kata 391 kati ya kata 518 zimefikishiwa huduma ya mawasiliano katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwezi Machi 2013 mpaka mwezi Agosti 2017 mwaka huu.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa alipofanya ziara ya mawasiliano vijijini kwenye Wilaya ya Bahi, Chamwino mkoani Dodoma na Gairo kwenye mkoa wa Morogoro, ameziagiza kampuni za simu kuhakikisha kuwa huduma za mawasiliano vijijini zinapatikana masaa yote 24, siku saba za wiki na katika kipindi cha mwaka mzima bila kukatika, kwa uhakika na kwa wakati wote. Hali ya ukosefu wa mawasiliano kwa nyakati za usiku imekuwa ikijitokeza kwenye baadhi ya maeneo ya vijijini ambako hakuna nishati ya uhakika ya umeme ambapo kampuni za simu zinatumia umeme wa jua kuendesha minara ili iweze kutoa mawasiliano kwa wananchi. Hali hiyo imedhihirishwa na wananchi wa kijiji cha Kweinswa,  waishio kata ya Nkalamo  iliyopo Wilaya ya Korogwe Vijijini mkoani Tanga ambapo mzee Kajembe Kijarala ameiambia Kamati kuwa changamoto hiyo wanaipata wanakijiji kwa nyakati za usiku hasa wakati wa kipindi cha masika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King amesema kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania kupitia Kamati yake itaendelea kuhakikisha kuwa Serikali inafikisha huduma za mawasiiano vijijini kwa wananchi wote mikoa mbali mbali. Prof. King amesisitiza kuwa wananchi wa vijiji mbalimbali kulikojengwa minara ya simu za mkononi washirikiane na kampuni za simu kulinda miundombinu ya mawasiliano ili waendelee kunufaika na uwepo wa minara hiyo kwenye makazi yao.
Nao wananchi wanaoishi kwenye makazi hayo wamesema kuwa uwepo wa minara ya simu za mkononi imewawezesha kupata huduma mbali mbali za mawasiliano ikiwemo kurahisisha mawasiliano baina yao, kutuma na kupokea pesa, kupeana taarifa za ugonjwa na misiba na kutumia kama huduma za kibenki. “ Mawasiliano yanashika kila siku, hamna tatizo lolote, Serikali imefanya vizuri kuweka mnara badala ya wananchi wa Jipe kwenda mbali mpaka Moshi au kutumia mnara wa Ugweno, nikiwasiliana na simu mara moja naenda hapo SACCOSS natoa hela,” amesema Bibi Mwanafuraha Nyange, mkazi wa kijiji cha Ziwa Jipe, kata ya Jipe iliyopo Wilaya ya Mwanga mkoa wa Kilimanjaro.
Aidha, ujenzi, usimikaji wa minara na ufiishaji wa huduma za mawasiliano vijijini zimekuwa zikifanywa kwa pamoja kati ya Serikali na kampuni za simu za mkononi ikiwemo Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Airtel, MIC TIGO, Vodacom, Zantel na Halotel. Kampuni hizi zinapatiwa ruzuku na Serikali kwa njia ya ushindani na wao kuongeza fedha zao kukamilisha ujenzi wa minara na ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini na kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara. Changamoto zinazoyakabili maeneo ya vijijini ni idadi ndogo ya wakazi, uwezo mdogo wa kifedha wa wakazi wa eneo husika kwenye matumizi huduma za mawasiliano vijijini (ARPU-Average Revenue Per User), ukosefu wa nishati ya uhakika ya umeme na barabara. UCSAF imeanzishwa kwa sheria ya Bunge Na. 11 ya mwaka 2006 kwa lengo la kufikisha mawasiliano vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Next Post Previous Post
Bukobawadau