SERIKALI: MATUMIZI YA DOLA NCHINI HAYAATHIRI KUSHUKA KWA THAMANI YA SHILINGI
Serikali
imesema kuwa kushuka au kupanda kwa thamani ya shilingi nchini hakusababishwi
na bidhaa na huduma mbalimbali kutozwa kwa dola bali kunatokana na misingi ya
shughuli mbalimbali za kiuchumi (Macroeconomic
fundamentals) pamoja na hali halisi ya uchumi wa nchi zinazofanya biashara
na Tanzania.
Hayo
yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Vwawa Mhe.
Japhet Hasunga (CCM), aliyetaka kujua mikakati ya Serikali katika kuimarisha
thamani ya shilingi ya Tanzania na kupiga marufuku matumizi ya fedha za kigeni
nchini.
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji aliainisha kuwa nakisi ya urari wa biashara, mfumuko wa
bei na tofauti ya misimu (seasonal
factors) ni sababu kuu zinazosababisha kushuka na kupanda kwa thamani ya
shilingi nchini.
Dkt.
Kijaji aliliambia Bunge kuwa ili kuimarisha thamani ya shilingi Benki Kuu
inaendelea kuthibiti mfumuko wa bei ili usitofautiane sana na wabia wa biashara
nchini.
“Benki
Kuu imethibiti biashara ya maoteo (speculation)
katika soko la fedha za kigeni ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa miamala ya
fedha za kigeni inafanywa na benki kwa ajili ya shughuli za kiuchumi tu na sio
biashara ya maoteo, hali hii itasaidia upatikanaji wa fedha za kigeni katika
soko la rejareja ili kupunguza shinikizo la kuporomoka kwa thamani ya
shilingi.”Alisema Dkt Kijaji.
Dkt.
Kijaji alifafanua kuwa pamoja na hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu ufumbuzi wa
kudumu wa kutengamaa kwa thamani ya shilingi nchini hutegemea zaidi kupungua
kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nchi za
nje.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
11/9/2017