Bukobawadau

SERIKALI YATAKIWA KULINDA BARABARA ZA LAMI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga, akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu hatua zinazochukuliwa katika ulindaji wa miundombinu ya barabara wakati walipokagua barabara ya Dodoma – Mayamaya iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso akitoa maoni kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga, juu ya ulindaji wa miundombinu na kuzingatia usalama wa mazingira wakati walipokagua barabara ya Dodoma – Mayamaya iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga, (watatu kushoto), akiwaonesha kingo za barabara baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakati walipokagua barabara ya Dodoma – Mayamaya iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga (katikati), wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakitoka kukagua daraja la Kelema linalounganisha Wilaya ya Chemba na Kondoa, mkoani Dodoma. Daraja hilo limekamilika kwa asilimia 98.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga, akitoa maelekezo kwa Mhandisi wa mradi wa barabara ya Mayamaya – Mela yenye urefu wa KM 99.3, Eng. Leornado Licari, wakati walipokagua Daraja Kelema lililopo katika barabara hiyo lenye urefu wa mita 205, mkoani Dodoma.
Mhandisi Mshauri wa mradi wa barabara ya Mayamaya – Mela yenye urefu wa KM 99.3, Eng. Leornado Licari akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu katika ziara ya ukaguzi wa daraja la Kelema lenye urefu wa mita 205 lilipo katika barabara hiyo mkoani Dodoma.
SERIKALI YATAKIWA KULINDA BARABARA ZA LAMI
Serikali imetakiwa kuweka mkakati wa kuzilinda, kutunza na kuhifadhi   barabara zote zinazojengwa kwa kiwango cha lami nchini ili kuziwezesha kudumu kwa muda uliokusudiwa na hivyo kuepuka gharama za ukarabati wa mara kwa mara.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu mheshimiwa Moshi Suleman Kakoso amesema hayo mara baada ya kukagua barabara ya Dodoma – Babati yenye urefu wa kilomita 263, ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika.
“Hakikisheni ujenzi wa barabara unaendana na uboreshaji wa huduma na maisha ya wananchi sehemu ambapo barabara hizo zinapita ili kuchochea maendeleo”, amesema mheshimiwa Kakoso.
Makamu mwenyekiti huyo amesema Kamati yake imeridhishwa na hatua zilizofikiwa za ujenzi wa barabara Dodoma –Babati KM na daraja la Kelema linalounganisha Wilaya za Chemba na Kondoa ambalo litawezesha barabara hiyo kupitika kwa uhakika wakati wote.
"Nimefurahishwa na taarifa aliyoitoa Meneja mradi wa barabara hii kwamba pamoja na kujenga barabara pia mkandarasi amechimba visima vya maji katika maeneo haya kwa ajili ya kusaidia wananchi jambo ambalo ni jema na la kuigwa na makandarasi wengine”, amesisitiza Makamu Mwenyekiti Kakoso.
Aidha, Makamu Mwenyekiti ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi),  kuwa na mpango endelevu wa kuweka kingo zinazoonesha mipaka ya hifadhi ya barabara mapema na kwa uwazi ili kuepusha migogoro kwa wananchi na ulipaji wa fidia zinazoweza kuepukika.
Ameongeza kuwa Serikali ihakikishe inasimamia ipasavyo sheria zinazolinda barabara ikiwemo kuweka alama za vivuko vya wanyama mahala panapostahili ili kudhibiti mifugo kukatiza ovyo katika barabara.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema katika kuhakikisha kuwa Serikali inailinda barabara ya Dodoma - Babati tayari imeagiza uongozi wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma na Manyara kuhakikisha wanatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa mizani ili kudhibiti madereva wanaozidisha uzito usiokubaliwa kisheria.

Ameongeza kuwa Wizara inaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuhamasisha utunzaji wa miundombinu ya barabara kama kutomwaga mafuta barabarani,kutopitisha mifugo na kutoiba alama za barabarani.
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu imefanya ziara katika mradi wa barabara ya Dodoma - Babati (Km 263), na daraja la Kelema lenye urefu wa mita 205 lililopo wilaya ya Chemba mkoani
Dodoma na kuridhishwa na miradi hiyo ambapo wameitaka Serikali kupitia wizara ya ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), kuhakikisha inalinda na kutunza miundombinu hiyo ili idumu muda mrefu.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Next Post Previous Post
Bukobawadau