Bukobawadau

SERIKALI YAZIONYA TAASISI ZA UMMA ZISIZOTUMIA WAKALA WA UNUNUZI NA UGAVI SERIKALINI (GPSA)

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza na Viongozi na watumishi wengine wa Wakala wa Ununuzi na Ugavi Serikalini (GPSA) Mkoa wa Kagera (hawapo pichani) alipotembelea ofisi hizo kuhusu kuhakikisha Taasisi zote za Serikali zinapata huduma kutoka Wakala huo, alipofanya ziara katika Mkoa huo.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akitoa maagizo kwa Kaimu Meneja  wa Wakala Ununuzi na Ugavi Serikalini (GPSA) Mkoa wa Kagera, Bi. Dorothea Bugenyi, kuhusu kuwahudumia Taasisi zote za Serikali kwa kuwa ndio wajibu wa Wakala huo, alipofanya Ziara katika Ofisi hizo za Mkoani Kagera.
 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Bw. Deodatus Kinawiro akielezea namna atakavyoshirikiana na Wakala wa Ununuzi na Ugavi Serikalini katika Mkoa huo ili kuhakikisha kunakuwa na matumizi adili ya fedha za Serikali, Naibu Waziri wa  Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alipotembelea Ofisi za Wakala huo Mkoani Kagera.
 Kaimu Meneja wa Wakala wa Ununuzi na Ugavi Serikalini (GPSA) Mkoa wa Kagera, Bi. Dorothea Bugenyi (kulia) akimuonesha Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) namna tetemeko la ardhi lilivyo haribu miundombinu ya Ofisi hizo, alipotembelewa na Naibu Waziri huyo katika Ofisi za GPSA Mkoani humo.
 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba  Bw. Deodatus Kinawiro (kulia) akizungumza jambo wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) alipotembelea Ghala la Wakala wa Ununuzi na Ugavi Serikalini (GPSA) Mkoani Kagera
 Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kulia) akitembelea maeneo ya Ofisi za Wakala wa Ununuzi na Ugavi Serikalini (GPSA) ambapo aliweza kupata maelezo namna  Wakala huo unavyofanya kazi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa nne kushoto), Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Bw. Deodatus Kinawiro (wa tano kulia), Kaimu Meneja wa Wakala wa Ununuzi na Ugavi  Serikalini (GPSA) Mkoa wa Kagera, Bi. Dorothea Bugenyi (wa tatu kushoto) na watumishi wengine wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa ziara ya Naibu Waziri huyo katika Ofisi hizo Mkoani Kagera.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
Benny Mwaipaja, Kagera

NAIBU waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameziagiza Mamlaka na Taasisi zote za Umma kufanya ununuzi wa vifaa na mafuta kupitia Wakala wa Serikali wa ununuzi na ugavi (GPSA) kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge na kuwaonya wahusika wote watakaoendelea kukaidi maagizo hayo kwamba watachukuliwa hatua za kisheria.

Dkt. Kijaji ametoa maagizo hayo mkoani Kagera baada ya kutembelea na kukagua shughuli zinazofanywa na Wakala wa Ununuzi na Ugavi GPSA mkoani humo na kubaini kuwa taasii na idara nyingi za umma zinafanya manunuzi nje ya mfumo wa GPSA jambo ambalo amesema ni ukiukwaji mkubwa wa sheria.

Alisema kuwa lengo la Serikali la kuanzishwa kwa wakala huo pamoja na mambo mengine ilikuwa kudhibiti matumizi ya Serikali na kuonya kuwa Serikali haitakubali kuona sheria zinakiukwa kwa makusudi na kwa malengo yanayoonesha kuna nia isiyo njema katika matumizi ya fedha za umma.

“Hili si ombi ni maelekezo na ni agizo, taasisi zote zipate huduma kutoka kwa wakala wetu (GPSA) kwani Serikali ilikuwa na dhamira ya uwepo wa matumizi sahihi ya fedha za matumizi wanazopelekewa na ndiyo maana ukaanzishwa Wakala huu” Alisema Dkt. Kijaji

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro, akizungumza kwaniaba ya Mkuu wa mkoa wa Kagera, aliiagiza Wakala wa Ununuzi na Ugavi (GPSA) mkoani humo kumpelekea orodha ya taasisi ambazo hazitumii huduma za wakala huo ili aweze kuchukua hatua.

Alisema kuwa ni jambo lisilofaa kwa Taasisi za Umma kukiuka sheria na kwamba watatekeleza maelezo yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango haraka ili kuokoa fedha za Serikali na kuweka uwajibikaji.

Awali, Kaimu Mkuu wa Wakala wa Ununuzi na Ugavi GPSA mkoa wa Kagera Bi. Dorothea Bugenyi alieleza kuwa katika kipindi cha miaka 3 iliyopita Wakala huo umeongeza makusanyo yatokanayo na mauzo ya vifaa na mafuta kutoka Shilingi bilioni 1.9 hadi kufikia Shilingi bilioni 2.34.

Alisema kuwa mapato hayo yangekuwa makubwa zaidi endapo taasisi zote za umma zingetii sheria na kufanya manunuzi yao ya vifaa na mafuta kutoka kwa Wakala huo na kuiomba Serikali kuusaidia Wakala huo kuziagiza taasisi zake za umma kutekeleza sheria hiyo kwa vitendo.
 Mwisho
Next Post Previous Post
Bukobawadau