KWAMBA AIRTEL NI MALI YA TTCL KWA 100%: RAIS MAGUFULI
Rais Magufuli amtaka waziri wa fedha kufuatilia kwa karibu suala la umiliki wa kampuni ya mawasiliano ya Airtel, akidai kwamba kwa taarifa alizonazo Airtel Tanzania ni mali ya TTCL Tanzania kwa asilimia miamoja.
“Kuna michezo michafu sana inaendela...hakikisha unafuatilia suala hili kabla ya mwaka huu kuisha, alisema Rais Magufuli wakati wa uwekwaji wa jiwe la msingi la ofisi ya taifa ya takwimu Dodoma.
Katika hafla hiyo Rais Magufuli alitoa onyo kwa wale ambao wanakuja na takwimu zao za mifukoni na kuzitaka mamlaka husika kutumia sheria zilizopo kuwabana wale ambao wanataka kuwapotosha Watanzania kwa takwimu zao za uongo. “Ukikosea kutoa takwimu...umeichafua nchi,” alisema Rais Magufuli.
“Hata mtu akija na takwimu za kupikwa kwamba vyuma vimekaza...mpelekeni mahakamani akaeleze ametoa wapi hito takwimu. Ninaomba kurudia tena, Watanzania tujifunze kuheshimu takwimu. Ukitoa takwimu za uongo athari yake ni mbaya sana kwa taifa.
Ninasikia watu wanalalamika kwamba vyuma vimekaza. Ninaomba niwahakikishie kwamba vitakaza kweli kweli…tutabana vichwa, tutabana miguu, tutabana matumbo, tutabana kila kitu.”
Rais magufuli alitoa faraja kwa wachapa kazi na kuwaeleza kwamba, “tutalegeza vyuma kwa wale ambao wako radhi kufanya kazi kwa juhudi,” na kuongeza kwamba “tunachukua hizi hatua ili kutengeneza maisha mazuri ya watanzania.”