Bukobawadau

SERIKALI KUBORESHA KIVUTIO CHA UTALII CHA ENEO LA BARABARA YA LAMI INAYOPITA JUU ZAIDI KUTOKA USAWA WA BAHARI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) akiongozwa na Meneja wa shamba la Miti Kawetire, Arnorld Shoo kukagua moja ya eneo katika shamba hilo ilipopita barabara ya lami ambayo ipo juu zaidi ya nyingine nchini ikiwa na urefu (Altitude) wa mita 2961 kutoka usawa wa bahari wakati wa zaira yake ya kikazi jana mkoani Mbeya. Alisema Serikali itaboresha mazingira ya eneo hilo ili yatumike kama kivutio cha utalii nchini.
Bofya kitufe cha PLAY kuangalia VIDEO

Na Hamza Temba, Mbeya
........................................................
Serikali imesema itaboresha mazingira ya kivutio cha utalii cha barabara ya lami ambayo ipo juu zaidi kutoka usawa wa bahari kuliko barabara zote nchini ili kupanua wigo wa vivutio vya utalii na kuongeza idadi ya watalii na mapato.

Hayo yameelezwa jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga baada ya kutembelea shamba la miti la Kawetire wilayani Mbeya na kujionea sehemu ya barabara ya lami inayopita katikati ya shamba hilo katika mlima Kawetire kwenye safu za milima ya Mbeya.

Eneo hilo la barabara hiyo ambayo hupitisha magari kutoka Jijini Mbeya kwenda katika Wilaya ya Chunya na Mikoa ya Singida na Tabora lina urefu (Altitude) wa mita 2961 kutoka usawa wa bahari katika Latitude 08’ 35 S na Longitude 33’ 25 E.

“Hatutaki ule utalii wa kutegemea wanyamapori pekee, hii sasa ni sehemu ya aina nyingine ya utalii ambayo ni lazima tuiboreshe tuweke kibao kizuri tuweke mazingira mazuri pamoja na kukitangaza ili watanzania na watalii kutoka nje waweze kutembelea hapa,” alisema Hasunga.

Alisema ili kufikia lengo liliwekwa na Serikali la kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni mbili mwaka 2020 na milioni 8 mwaka 2025 vivutio vyote vya utalii vilivyopo nchini vitatambuliwa, kuimarishwa na kuviwekea miundombinu itakayowavutia watalii kuvitembelea.

Aidha aliuagiza uongozi wa shamba hilo kushirikiana na wakala wa huduma za barabara –Tanroads katika kuboresha mazingira yanayozunguka eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuweka bango la kisasa la kutambulisha eneo hilo, kujenga bustani na maeneo rafiki ya kupumzikia kwa ajili ya kuwavutia watalii kutembelea eneo hilo na kupiga picha.

Mbali na kivutio hicho aliuagiza uongozi wa shamba hilo kutobomoa majengo ya kale yaliyotumiwa na wakoloni katika shamba hilo na badala yake yatumike kwenye utalii wa mambo ya kale sambamba na utalii wa misitu ya kupandwa inayopatikana pia katika shamba hilo.

Hata hivyo alisema kupitia mradi wa REGROW wa kuendeleza utalii kanda ya kusini Serikali imepokea mkopo wa masharti nafuu wa dola za Kimarekani milioni 150 sawa za zaidi ya bilioni 340 za kitanzania kutoka benki ya dunia kwa ajili ya kusaidia kuboresha miundombinu ya vivutio vya ukanda huo.

Kwa upande wake Meneja wa shamba hilo, Arnorld Shoo alisema eneo hilo la barabara limekuwa ni kivutio cha kipekee cha utalii katika shamba hilo ambapo pia hupata mapato kupitia watu na vikundi mbalimbali ikiwemo wanakwaya na wanafunzi ambao hufika eneo hilo kwa ajili ya kupiga picha za kumbukumbu.  
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) na Meneja wa shamba la Miti Kawetire, Arnorld Shoo wakiangalia bango linaloonesha eneo katika shamba hilo ilipopita barabara ya lami ambayo ipo juu zaidi ya nyingine nchini ikiwa na urefu (Altitude) wa mita 2961 kutoka usawa wa bahari wakati wa zaira yake ya kikazi jana mkoani Mbeya. Alisema Serikali itaboresha mazingira ya eneo hilo ili yatumike kama kivutio cha utalii nchini.
Next Post Previous Post
Bukobawadau