HOSPITALI TEULE YA RUBYA YAPOKEA VIFAA TIBA
Mganga mkuu wa Hospitali ya Rubya Dr George Kasibante wilayani Muleba mkoani Kagera (kulia) akitoa maelezo kwa Askofu msaidizi wa jimbo katoliki la Bukoba mkoani Kagera Methodius Kilaini na wajumbe wa bodi ya afya ya Hospitali hiyo baada ya kupokea pikipiki mbili zilizotolewa na wafadhili kutoka nchini Uholanzi ikiwa ni sehemu ya vifaa tiba vilivyotolewa na wafadhili hao kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa yasiyotibika ili kuwaongezea siku zao za kuishi.
Muleba:Hospitali teule ya Rubya iliyoko wilaya ya Muleba mkoani Kagera imepokea vifaa tiba kutoka kwa marafiki wa Hospital hiyo walioko nchini Uholanzi vyenye thamani ya Sh232.32milioni kwa ajili ya kuboresha huduma za matibabu na kupunguza vifo visivyo kuwa vya lazima kwa wagonjwa
Mganga mkuu wa hospital ya Rubya Dkt George Kasibante alitoa taarifa ya kupokea vifaa hivyo jana mbele ya Askofu msaidizi wa jimbo la Bukoba Methodius Kilaini na wajumbe wa kamati ya afya ya wilaya ya Muleba katika hafla ya kupongeza marafiki wa Uholanzi wanaofadhili hospitali hiyo.
Dkt Kasibante amesema katika fedha hizo zimetumika kujenga vyumba vitatu vya upasuaji na kuboresha viwili vilovyokuwepo na kuviwekea vifaa vya kisasa kwa ajili ya wanawake wanaojifungua zikiwemo mashine za kusafisha vifaa tiba
Alisema mashine hizo zinatumika kusafisha mashuka yanayotumika kwa ajili yan upasuaji na vifaa vinginevyo kwa lengo la kuepuka maambukizi ya virusi vya magonjwa kutoka kwa mzazi mmoja na mwingine wakati wa zoezi la upasuaji.
Aidha alisema mradi wa huduma za kuthibiti maambukizi ya Virus vya Ukimwi (MDH) katika wizara ya Afya jamii jinsia wazee na watoto umesaidia ujenzi wa jengo lenye miundombinu mbalimbali kwa ajili ya shughuli ya tohara kwa wanaume ambapo inadaiwa asilimi 60 wanapata maambukizi ya UKIMWI
Alisesema pia MDH wametoa mashine(Generator) kwa ajili ya kuboresha huduma ya nishati ya umeme itakayosaidiana na umeme wa TANESCO ili kuinua kiwango cha huduma bora kwa wagonjwa kisha kuepuka vifo katika vyumba vya upasuaji hasa wanawake wanaohitaji kujifungua au wanaokuwa katika vyumba mahututi
“Upatikanaji wa vifaa hivi utasaidia kupunguza vifo kwa wajawazito na watoto wanaozaliwa lakini hata wagonjwa wengine wanaofika kupata huduma za matibabu wengi wao wakihitaji upasuaji” Alisema Kasibante
Hospitali ya Rubya inamilikiwa na jimbo katoliki la Bukoba iliyoanza mwaka 1957 chini ya Masista wa Fransiscan kutoka nchini Uholanzi ikiwa na vitanda 70 na sasa inavyo vitanda 207 na kwa mujibu wa wizara ya afya usatawi wa jamii jinsia na watoto inatakiwa iwe na vitanda 162 kutosheleza mahitaji ya wagonjwa.
Pia Hospitali hiyo inapata ruzuku ya serikali lakini huduma zinazotolewa wagonjwa wanachangia gharama zinazotumika kuwamotisha watumishi 382 wanaohitajika lakini waliopo ni 195 na wanapungua 187 ambapo ni changamoto ikiwemo miundombinu nyinginezo katika kutoa huduma bora za matibabu
Askofu wa Jimbo katoliki la Bukoba Methodius Kilaini aliwashukuru wahisani hao kutoka uholanzi na kuwaomba kuongeza juhudi za kuisaidia jamii ya jimbo hilo kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma bora za kiafya.
Askofu Kilaini aliishauri serikali uboreshaji huduma za afya nchini kwa kutenga fedha za kuhudumia vituo vya taasisi binafsi kutokana na watumishi wa taasisi hizo kufanya kazi na kupata maslahi yasiyolingana na huduma inayotolewa.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Muleba Richard Ruyango , Afisa elimu idara ya msingi wilayani humo Dkt Charles Katarama aliwataka watumishi wa hospitali hiyo kuitumia miungombinu iliyoboreshwa na vifaa tiba kwa uangalifu na uaminifu viweze kufanya kazi kwa malengo yaliyokusudiwa.
Alisema serikali tayari imeboresha huduma za afya kwa kuziwekea fedha hospitali zinazomilikiwa na taasisi za dini na ina mpango wa kuzifanya hospitali za taasisi kuwa chini ya halmashauri za wilaya na kuwalipa watumishi wa taasisi hizo kupitia halmashauri hizo.
PICHA na Habari kwa hisani ya Shaaban Ndyamukama