VIONGOZI WA MADHEHEBU YA DINI KAGERA WAMPONGEZA RAIS MAGUFULI WAHAIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUDUMISHA AMANI NA UTULIVU
Viongozi wa Madhehebu ya Dini Mkoani Kagera waipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kwa kuchukua hatua na maamuzi yanayolenga kumuinua mwananchi mnyonge ili afaidike na raslimali za nchi yake.
Na: Sylvester Raphael
Na: Sylvester Raphael
Viongozi hao wa Madhehebu ya Dini Mkoani wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti ofisini kwake Januari 16, 2019 walimpongeza Rais Magufuli kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo nchini na yenye manufaa kwa umma mfano ununuzi wa ndege, ujenzi wa Reli ya Kisasa na ujenzi wa mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge pamoja na miradi mingine mingi ya maendeleo ya wananchi.
Pia Akiongea kwa niaba yao Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoriki la Bukoba Methodius Kilaini alisema kuwa wanaipongeza Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli kwa kudumisha amani, utulivu na mshikamano kwa Watanzania na kuendelea kutekeleza shughuli mbalimbali ambazo zinalenga maslahi mapana ya wananchi.
Vilevile katika mazungumzo hayo Viongozi hao wa Madhehebu ya Dini walimweleza Mkuu wa Mkoa Mhe. Gaguti kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali ya mkoa katika kudumisha amani na utulivu kati wananchi wa Kagera ili kudumisha mshikamano kama ilivyo desturi yao.
Pia wataendelea kuhamasisha wananchi kuchapa kazi kwa bidii kujiletea maendeleo na kukuza uchumi wa mkoa kama jina la Mwaka 2019 kwa lugha ya Kihaya linavyohimiza kila mwananchi kufanya kazi likimaniisha kuwa kila mmoja atakula kwa jasho lake “Biluga Omumpiita”.
Naye Mkuu wa Mkoa Mhe. Gaguti katika mazungumzo hayo aliwahakikishia Viongozi hao wa Madhehebu ya Dini kuwa yeye Binafsi kama Mkuu wa Mkoa wa Kagera pamoja na Serikali ya Mkoa wataendelea kushirikiana nao kwani wao ndiyo nguzo kuu ya amani katika mkoa lakini pia nguzo kuu ya maadili hasa kwa kuiunganisha Serikali na wananchi wake.
“Sisi Serikali tutaendelea kushirikiana na nyinyi kama ilivyo desturi ya Mkoa wetu wa Kagera na tunawategemea sana katika kuhakikisha mkoa wetu unaendelea kudumisha amani na utulivu kwani kila mara mnapokutana na waamini wenu mkahubiri juu ya amani na utulivu sisi kwetu kazi inakuwa ndogo. Pia mnapowahimiza wananchi wafanye kazi kwetu sisi Serikali inakuwa rahisi mnokuweka msukumo kwa wananchi.” Alisistiza Mhe. Gaguti
Katika mazungumzo hayo na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Viongozi wa Madhehebu ya Dini waliokuwepo ni pamoja na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoriki la Bukoba Method Kilaini, Sheikh Aruna Kichwabuta Sheikh wa Mkoa wa Kagera na. Askofu Dkt. Abedinergo Keshomshahara wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania Dayosisi ya Kasikazini Magharibi.
Mkuu wa Mkoa akimalizia mazungumzo na Viongozi hao alitoa rai yake kuwa Mkoa wa Kagera kwa ukiongozwa na Kaulimbiu ya “Kazi, Amani na Maendeleo” umejipanga kwa mwaka huu wa 2019 kuwa ni mwaka wa kazi lakini pia ni mwaka wa wananchi wote hasa wanaojihusisha na biashara iwe kubwa au ndogo kulipa kodi, kodi ambayo ni rafiki ili kuhakikisha Kagera inarudi kwenye enzi zake za uchumi
imara.
Viongozi wa Madhehebu ya Dini Mkoani Kagera katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti.