SOKO KUU LA MADINI YA TIN KAGERA LAZINDULIWA RASMI WACHIMBAJI WADOGO WAANZA KUUZA MADINI KWA BEI YA SOKO LA DUNIA
• Kagera Bado ni Tajiri Katika Madini ya TIN Vitalu Saba Havijawahi Kuguswa – RC Gaguti
Na: Sylvester Raphael
Mkoa wa Kagera hatimaye wazindua Soko Kuu la Madini ya TIN Wilayani Kyerwa na mara ya kuzinduliwa rasmi soko hilo biashara ya madini ya TIN imeanza kufanyika mara moja katika soko hilo. Soko la madini ya TIN Wilayani Kyerwa ni mojawapo kati ya masoko kumi na sita ya madini nchini ambayo tayari yamezinduliwa katika mikoa mbalimbali.
Mkoa wa Kagera hatimaye wazindua Soko Kuu la Madini ya TIN Wilayani Kyerwa na mara ya kuzinduliwa rasmi soko hilo biashara ya madini ya TIN imeanza kufanyika mara moja katika soko hilo. Soko la madini ya TIN Wilayani Kyerwa ni mojawapo kati ya masoko kumi na sita ya madini nchini ambayo tayari yamezinduliwa katika mikoa mbalimbali.
Akizindua soko Kuu la Madini ya TIN Mei 8, 2019 Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo alisema kuwa nia ya Rais John Magufuli kuagiza masoko ya madini kuanzishwa nchini ni kutaka wananchi wanufaike na raslimali ya madni katika maeneo yao kwa kuwa na mfumo rasmi wa kukusanya, kuhifadhi na kuuza madini katika masoko maalumu.
Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa Wizara ya Madini imejidhatiti vyema kudhibiti utoroshaji wa madini nchini na ndiyo maana ilianzisha kanuni za masoko ya madini za mwaka 2019 na kufuta kodi mbili za kero za ongezeko la thamani ya asilimia 18% (VAT 18%) na kodi ya zuio ya asilimia 5% (Withholding Tax 5%) ili kuhakikisha kila mtu katika nafasi yake ananufaika Serikali, Wafanyabiashara, Wananchi na wachimbaji pia.
“Uwepo wa Soko la Madini ya TIN Kyerwa utatatua changamoto za bei ya madini haya hasa kwa wachimbaji wadogo ambapo wafanyabiashara hawataruhusiwa kununua madini ya TIN chini ya bei elekezi ya soko la dunia. Wachimbaji wadogo sasa ni fursa kwenu kunufaika kama mlivyoona leo madini yanauzwa kutokana na bei ya soko la dunia ya leo.” Alisisitiza Naibu Waziri Stanslaus Nyongo.
Agizo; Katika uzinduzi huo pia Naibu Waziri Nyongo alitoa muda wa mwezi mmoja kuanzia Mei 8, 2019 kwa wachimbaji wote wa madini wenye leseni za uchimbaji kuhakikisha zinafanya kazi na kama muda huo ukipita bila leseni hizo kuwa hai na kufanya kazi wahusika watanyanganywa na Serikali itazitoa kwa watu wengine ambao wapo tayari kuzitumia kuchimba madini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenenrali Marco E. Gaguti katika uzinduzi huo alisema kuwa uzinduzi wa soko la madini ya TIN Kyerwa ambalo tayari limeanza kufanya kazi utaziba uvujifu na utoroshaji wa madini ya TIN kwani hakutakuwa na sababu tena ya kutorosha madini ghafi wakati soko ambalo lina bei ya soko la duni lipo.
Mkuu wa Mkoa Gaguti alionya kuwa mtu yeyeyote asithubutu kufanya utoroshaji kwani Mkoa na Wilaya wamejipanga vizuri katika udhibiti wa madini hayo. Pia aliwahakikishia wachimbaji wadogo kutatua changamoto zao za kuwafikishia umeme katika machimbo yao na kushirikiana nao katika kutatua changamoto za ukosefu wa mitaji ili uzalishaji wa TIN uongezeke katika mkoa wa Kagera.
“Nataka kuona wachimbaji wadogo wa TIN mnatajirika katika mkoa wetu, kwa utafiti wa awali ambao ulifanyika bado kuna vitalu saba vya madini ya TIN hapa Mkoani Kagera ambavyo bado havijawai kuchimbwa na namuomba Waziri hapa mbele yenu mara baada ya utaratibu kukamilika nyinyi wachimbaji wadogo mpewe kipaumbele na tutajirike na madini yetu.” Alisisitiza Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Nao Wachimbaji wadogo wa madini ya TIN Wilayani Kyerwa kupitia umoja wao (KAREMA) waliishukuru Serikali kuanzisha Masoko ya Madini nchini hasa soko la madini ya TIN kwani walikuwa wanashindwa kunufaika na kazi yao na kupunjwa na wafanyabiashara wa madini hayo kutokana na kutokuwa na bei elekezi ya kuuza madini yao pia na soko maalum linalojulikana.
“Kwa mfumo huu wa kuchimba, kuhifadhi na kuuza madini yetu tena kwa bei za soko la dunia tutanufaika na kazi yetu kwani wakati mwingine tulikuwa tunalazimika kutorosha madini haya ili kutafuta bei nzuri lakini sasa tutakuwa tunauza kulingana na bei ya soko la dunia ya siku hiyo na wakati huo tunashukuru sana Serikali na tupo tayari kulipa kodi zote za Serikali bila shuruti.” Walieleza Wachimbaji Wadogo
Kwa mujibu wa Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kagera Mhandisi Lucas Mlekwa hadi April 2019 Mkoani Kagera kulikuwa kuna jumla ya leseni za uchimabaji mdogo wa madini ya TIN 248 zinazomilikiwa na wazawa na leseni 29 ndizo zinafanya uzalishaji kwa sasa, Leseni 124 zimeandikiwa hati ya makosa (default note) na leseni 95 zipo hai lakini hazifanyi kazi kwa kukosa mtaji.
Aidha, Mhandisi Mlekwa alisema kuwa tayari kuna wawekezaji wawili wa kuyaongeza thamani madini ya TIN ambao ni Africani Top Minerals Ltd na Tanzaplus Minerals ambao sasa wamepata leseni za kuyeyusha madini ya TIN na kuyaogezea thamani na katika kiwango cha kupata metali ya TIN (Tin ingot) ya ubora ili waweze kuuza ndani na nje ya nchi na tayari wameanza kununua madini hayo Wilayani Kyerwa.
Takwimu za uzalishaji wa madini ghafi ya TIN na makusanyo yake kwa miaka minne mfurulizo, Mwaka 2015/16 zilizalishwa tani 92 thamani yake ilikuwa ni shilingi bilioni 1,226,268,910 mrahaba wa Serikali uliokusanywa ni shilingi milioni 48,773,723 sawa na asilimia 0.1% ya mchango wa makusanyo ya kila madini mkoani Kagera.
Mwaka 2016/17 zilizalishwa tani 103 thamani yake ilikuwa ni shilingi bilioni 1,887,365,750 mrahaba wa Serikali uliokusanywa ni shilingi milioni 75,494,770 sawa na asilimia 4.8% ya mchango wa makusanyo ya kila madini mkoani Kagera. Pia mwaka 2017/2018 zilizalishwa tani 11.06 thamani yake ilikuwa ni shilingi milioni 203,921,700 mrahaba wa Serikali uliokusanywa ni shilingi milioni 14,274,519 sawa na asilimia 1.1% ya mchango wa makusanyo ya kila madini mkoani Kagera.
Mwaka 2018/19 zilizalishwa tani 7.21 thamani yake ilikuwa ni shilingi milioni 114,894,900 mrahaba wa Serikali uliokusanywa ni shilingi milioni 9,199,002.61 sawa na asilimia 0.3% ya mchango wa makusanyo ya kila madini mkoani Kagera, uzalishaji ulishuka mwaka huo kutokana na zuio la Serikali la kuuza nje ya nchi madini ghafi na matarajio ya mwaka 2019/20 uzalishaji wa TIN hafi utapanda tena.
Matumizi ya madini ya TIN, TIN hutumika kuunganisha vitu mbalimbali kama mabomba ya chuma na metali (Steel/ Metal), mifumo ya umeme (electric circuit), mifumo ya kielektroniki ya simu (mobile phone), vyuma vya reli, mifumo ya ndege, mifumo ya lifti za umeme kwenye magorofa.
Pia madini ya TIN hutumika kuzuia kutu kwenye vyombo vya kuhifadhia chakula (Tin plated steel containers au Tin cans food storage containers) kwa muungano wa madini ya chuma. Tin vilevile hutumika kuzuia kutu kwenye mabati ya kujengea nyumba (Iron sheet tin coating).
Elimu, ni vyema sasa umma wa Watanzania hasa wananchi wa Mkoa wa Kagera ukafahamu vizuri matumizi ya madini ya TIN yanayopatikana Wilayani Kyerwa kuwa hayatumiki kutengeneza mabati ya kujengea bali ni sehemu tu ya kuzuia kutu katika mabati hayo.
Kabla ya uzinduzi wa soko kuu la Madini ya TIN Wilayani Kyerwa Mkoani Kagera Mei 8, 2019 takwimu za utoroshaji wa madini hayo ulikuwa ni kilo 2,371 za madini ghafi zenye thamani ya shilingi milioni 45,049,000 watuhumiwa walikamatwa na kesi zao zinaendelea Mahakamani. Pia kilo 5,894.05 za madini ghafi ya TIN zenye thamani ya shilingi milioni 111,986,950 ziliripotiwa Polisi kuibiwa kwenue stoo za wachimbaji na wafanyabiashara za madini