Bukobawadau

PROFESA KAMUZORA AHITIMISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA KAGERA KWA KUWAKUMBUSHA WATUMISHI WAJIBU WAO WA KUCHAPA KAZIKWA UADILIFU

Na: Sylvester Raphael
Wiki ya Utumishi wa Umma Mkoani Kagera yahitimishwa na Katibu Tawala Mkoa Profesa Faustin Kamuzora ambaye ni msimamizi mkuu wa watumishi wa umma katika Idara na taasisi zote za umma mkoani humo ambapo alihitimisha kwa kuongea na watumishi hao katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera.
Profesa Kamuzora akiongea na watumishi hao kutoka Idara, Taasisi, Serikali za Mitaa na Serikali Kuu aliwakumbusha wajibu wao wa kuwahudumia wananchi kwa kutumia muda mfupi sana lakini kutekeleza majukumu au shughuli nyingi za kuwaletea wananchi hao maendeleo.
“Sote tunajua kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya uhakiki na kuwaondoa watumishi ambao walikuwa hawastahili kuwa watumishi wa umama na sisi tuliobaki tunatakiwa kuufurahia utumishi wa wetu kwani sasa Serikali imeanza kurekebisha maslahi yetu kwa kupandisha vyeo na kurekebisha miundo ili kila mtumishi apate anachostahili kulingana na miundo ya utumishi wa umma iliyopo.” Alisisitiza Profesa Kamuzora.
Kwa upande mwingine Profesa Kamuzora alitoa rai kwa Watumishi wa Umma mkoani Kagera kuhakikisha wanatumia fursa za uwepo wa Hifadhi za Taifa za Chato - Burigi, Ibanda na Rumanyika kuzitembelea hifadhi hizo ili kupumzisha akili lakini pia kuangalia fursa ambazo zinaweza kuingiza kipato kwao kuzichangamkia ili kujiongezea kipato kuliko kuacha na fursa hizo zinachukuliwa na watu toka nje ya mkoa wakati zipo wazi kwa kila mmoja.
Fursa ya pili alioingelea kwa watumishi Profesa Kamuzora ni kuhusu Bomba la mafuta kutoka Ohima nchini Uganda kwenda mkoani Tanga litakaloingilia Mkoani Kagera kuhakikisha kila mtumishi anatimiza wajibu wake na kufanya kila liwezekanalo katika nafasi yake kutokwamisha bomba hilo kuanza kufanya kazi kama inavyotarajiwa kufanyika.
Tatu Profesa Kamuzora aliwakumbusha watumishi wa umma kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu 2019 lakini watumishi hao wanatakiwa kuzingatia kanuni na taratibu za utumishi wa Umma ambazo zinaelekeza namna mtumishi anavyoweza kushiriki katika Uchaguzi bila kuvunja sheria zilizowekwa.
Aidha, Profesa Kamuzora aliwataka viongozi wa taasisi, na mbalimbali za Serikali kuhakikisha wanatoa motisha kwa watumishi walio chini yao ili kuwatia moyo na morali wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mahala pa kazi na kufikia lengo la Serikali ya Awamu ya Tano la kuufikia Uchumi wa Kati.
Profesa Kamuzora aliendelea kusisitiza watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kagera kuongeza jitihada za kutoa elimu ya lishe kwa wananchi kwani mkoa pamoja na kuwa na vyakula vingi lakini tatizo la udumavu bado lipo juu. Tatizo si vyakula bali elimu kwa wananchi kujua namna bora ya kula au kutumia vyakula vya aina mbalimbali walivyonavyo.
“Unaweza kuona kuwa kuna shida katika hili na sitaki kuamnini au kulilinganisha hili la udumavu na ninacotaka kukisema , juzi nilikwenda Mkoani Ruvuma kuona timu yetu ya Mkoa ya UMISETA inavyoshiriki mashindano lakini namba walioshika vijana wetu inaedana na namba ya udumavu katika mkoa wetu, sasa sisi kama watumishi wa umma tunalo jambo lakufanya inamaana kwenye ligi ya maendeleo kuna sehemu hatutimizi majukumu yetu ipasavyo.” Alikazia Profesa Kamuzora
Naye Bw. Abbas Marikela Mkuu wa Hazina Ndogo Mkoani Kagera akitoa maoni yake katika kuhitimisha Wiki ya Utumishi wa Umma alitoa wito kwa Maafisa Utumishi katika Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali kutunza nyaraka za watumishi hasa wastaafu kwani wanapata shida sana wanapokutana na malezo tofauti na nyaraka zao walizonazo.
Bw. Abbas alitoa mfano kuwa watumishi wastaafu wengi unakuta hawapo katika masharti ya kudumu ya utumishi wa umma lakini wanakuwa hawajui na Maafisa Utumishi wao hawawaelezi jambo ambalo huleta usumbufu kwa mstaafu mwenyewe lakini pia na ofisi za hazina za mkoa kumbe kama Afisa Utumishi kama angetekeleza wajibu wake tatizo hilo lisingejitokeza.
Mwisho katika kuhitimisha Wiki ya Utumishi wa Umma Mkoani Kagera iliyoanza Juni 19 hdai 25, 2019 watumishi wa umma walikumbushwa na kushuriwa kula vizuri, kupumzika kwa mda mrefu na kuomba ushari pale wanapokwazika au kukumbwa na matatizo kuliko kukaa kimya kuwa ni tiba kwa kiwango kikubwa kwa afya zao bila kusahau kufanya mazoezi ya mara kwa mara kuiweka miili yao imara.
Next Post Previous Post
Bukobawadau