IJUE MITAZAMO YA VIONGOZI WETU KUELEKEA WIKI YA UWEKEZAJI KAGERA AGOSTI 12 HADI 17, 2019 GYMKHANA MANISPAA YA BUKOBA
Tunapoelekea katika Wiki ya Uwekezaji Mkoani Kagera sasa tunakuletea makala fupi fupi ili ujue malengo ya wiki hiyo na mtazamo wa viongozi wa Mkoa wa Kagera kuelekea Wiki hiyo Agosti 12 hadi 17, 2019 wiki ambayo ni fursa kubwa kwa Wanakagera na wadau mbalimbali wa maendeleo kuzijua fursa zinazopatka Kagera na kuzichangamkia.
Kaulimbiu ya Wiki ya Uwekezaji Kagera ni “Kagera Eneo la Kimkakati kwa Uchumi Wetu na Afrika Mashariki” kaulimbiu hii inamaanisha kuwa Mkoa wa Kagera unapakana na nchi tano za Kenya, Uganda, Burundi, Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi hizo ni fursa ya biashara kutokea Kagera.
Katika kuelekea Wiki ya Uwekezaji Kagera Mkuu wa Mkoa Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti tayari amefanya mawasilianao na Balozi wa Nchi ya Kongo ambaye tayari amethibitisha kushiriki wiki hiyo jambo ambalo kwa wadau wa biashara wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo ya kufanya biashara na nchi ya Kongo (DRC) mfano biashara ya Samaki, Dagaa, mbogamboga, mahindi na ndizi.
Pili, Mhe. Gaguti tayari Julai 7, 2019 amekutana na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda Mhe. Ernest Mangu ili kuweka mazingira sawa kati ya wafanyabiashara wa Rwanda na Tanzania na Wanankagera kutumia fursa ya mpaka wa Rusumo kufanya biashara nchini Rwanda kwa kutumia fursa ya ukaribu na kuwa na mpaka mrefu katika wa Kagera.
Balozi wa Tanzania nchini Rwanda Mhe. Ernest Mangu katika kikao hicho cha Julai 7, 2019 kilichofanyika Wilayani Ngara alihaidi kuwaleta wafanyabiashara wa Rwanda kuja kushiriki katika Wiki ya Kagera kuona fursa za uwekezaji pamoja na biashara mbalimbali wanazoweza kufanya kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa Mkoa wa Kagera au Watanzania, hiyo ni fursa inakuja.
Naye katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Profesa Faustin Kamuzora akiwa Mwenyekiti wa kikao cha kupitia andiko la uwekezaji Mkoani Kagera kilichofanyika Julai 11, 2019 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa alisema kuwa ni bahati kubwa ambayo haijawahi kutokea tangu uhuru mkoa kuwa na andiko la uwekezaji ambalo litazinduliwa rasmi Agosti 14, 2019 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ambaye atakuwa mgeni Rasmi katika Wiki ya Uwekezaji Kagera.
Naye Sheikh Haruna kichwabuta Sheikh wa Mkoa wa Kagera akitoa neno katika uzinduzi wa mpango mkakati wa miaka mitano wa maendeleo wa Baraza la Waislamu Tanzania Mkoa wa Kagera Juni 22, 2019 katika Shule ya Nyanshenye Manispaa ya Bukoba alitoa wito kwa Waislamu wenzake kuiona Wiki ya Kagera kama fursa na wasibaki nyuma bali washiriki kikamilifu mkoa wa kagera usonge mbele kwa kuzitumia fursa uliobarikiwa nazo
Askofu Dk. Abednego Keshomshahara wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Magharibi akitoa neno katika mkutano wa SINODE wa mwaka Kiizi Halmashauri ya Bukoba aliwakumbusha wachungaji Maaskofu na viongozi wote waliokuwepo katika mkutano huo kuwa Mkuu wa Mkoa Kagera anataka Kagera ifunguke na anatakiwa kuungwa mkono kwa dhati katika Wiki ya Uwekezaji Kagera.
Katika Wiki ya Uwekezaji Kagera pamoja na fursa nyingi zitakazokuwepo lakini fursa ya utamaduni katika mkoa wa Kagera pia itaangaliwa kwa karibu hasa utamaduni wa watu wanaoishi katika mkoa huu ambapo tamaduni hizo zinaweza kuwa kivutio kikubwa na kuleta watalii na kuacha fedha za kigeni ili kukuza zaidi uchumi wa mkoa.
Jipange kushiriki Wiki ya Uwekezaji Kagera na kuzitumia fursa za Kagera kujenga uchumi wako binafsi, uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla “Kagera Eneo la Kimkakati kwa Uchumi Wetu na Afrika Mashariki” Kagera Kazi, Amani na Maendeleo.