MARAIS WASTAAFU, VIONGOZI WAANDAMIZI WA SERIKALI NA MABALOZI WAMLILIA MAGUFULI
Na mwandishi wetu
Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi waandamizi wa Serikali na mabalozi waonaziwakilisha nchi zao hapa Nchini wamewataka watanzania kuendelea kudumisha uzalendo, fikra na maono aliyokuwa nayo Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ili kuiwezesha Tanzania kukua kimaendeleo
Akizungumza mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo katika viwanja vya Karimjee, Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Kikwete amesema kifo cha Hayati Magufuli hakikutarajiwa hasa wakati huu ambapo taifalilimuhitaji na kuwasihi watanzania kudumisha mema aliyoyaasisi kwa maslahi ya taifa.
“Kwa kweli kifo chake hakikutarajiwa, tulitegemea kwa kweli aendelee kuliongoza taifa kwani katika mhula wake wa kwanza aliliongoza taifa vizuri sana…….naamini kuwa yale ambayo hayakukamilika, Rais wa Jamhuri ya Tanzania mhe. Samia Suluhu Hassan atayaendeleza kikamilifu,” Amesema Dkt. Kikwete na kuwasihi watanzania kuendelea kudumisha uzalendo, fikra na maono aliyokuwa nayo Hayati Dkt. Magufuli.
Rais wa Awamu ya Pili, Mhe. Alhaji Ali Hassan Mwinyi nae amefika katika viwanja vya Karimjee na kusaini kitabu cha maombolezo akifuatiwa na Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri yaMuungano wa Tanzania Mhe. Mohamed Gahib Bilali, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma na pamoja na Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai nae pia amefika na kusaini kitabu hicho akifuatiwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mhe. Zubeir Ali Maulid ambaye amesema kuwa Hayati Magufuli katika kipindi kifupi cha uongozi wake amefanya mambo mengi yatakayosalia kuwa historia katika taifa la Tanzania.
“Msiba huu ni wetu sote watanzania na umetugusa sana kwani hayati Magufuli ameyafanya mengi katika mhula wake wakwanza ambapo mengi hayo tumekuwa tukinufaika nayo sisi watanzania…..kwa sasa tushikamane kudumisha umoja wetu ili kuweza kusonga mbele kimaendeleo,” Amesema Mhe. Maulid
Aidha, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini nao wameungana na watanzania kuomboleza kifo cha Hayati Dkt. Magufuli kwa kusaini kitabu cha maombolezo ambapo baadhi yao wamemuelezea kuwa katika uhai wake Hayati Magufuli alitamani kuiona Tanzania inayojitegemea kiuchumi na watu wake kuondokana na umasikini.
Naibu Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Mhe. Prefere Ndayishimiye amesema kuwa msiba wa Hayati Magufuli umewagusa sana kwani alikuwakiongozi aliyependwa na kujulikana na bara lote la Afrika.
“Amefanya maendeleo makubwa ambapo naamini kuwa vizazi vijavyo vitayaona na kuendeleza pale alipoishia Dkt. Magufuli,” Amesema Naibu Balozi
Kadhalika, mbali na viongozi wastaafu pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali wananchi wa kada mbalimbali wamejitokeza kwa wingi kusaini kitabu cha maombolezo na kumuelezea hayati Magufuli kuwa alikuwa kiongozi aliyeweka maslahi ya nchi mbele kwa manufaa ya watanzania.