DUBAI: WAZIRI NDUMBARO KUINADI TANZANIA KATIKA MAONESHO MAKUBWA YA EXPO 2020-DUBAI
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ( katikati) akizungumza na Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Francis Michael ( kushoto) wakiangalia picha mbalimbali za uwekezaji, miundombinu pamoja na vivutio Vya Utalii vilivyopo Tanzania katika Maonesho ya EXPO 2020 Dubai, ambapo Tanzania ni Miongoni kwa Nchi 192 zinazoshiriki Maonesho hayo. Kulia ni Mkurugenzi wa Wanyamapori. Dkt. Maurus Msuha
DUBAI: WAZIRI NDUMBARO KUINADI TANZANIA KATIKA MAONESHO MAKUBWA YA EXPO 2020-DUBAI
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ameungana na Mawaziri wengine kutoka Tanzania kushiriki katika Maonesho Makubwa ya Dunia ya Expo 2020 Dubai kwa ajili ya kuongeza nguvu katika ushiriki ikiwa ni jitihada za kuinadi Tanzania katika nyanja mbalimbali za uwekezaji ikiwemo sekta ya Uwekezaji na utalii
Aidha, Dkt.Ndumbaro amewapongeza Waoneshaji wa Banda la Tanzania katika Maonesho ya EXPO 2020 Dubai kwa kazi kubwa wanayoifanya ambapo Banda hilo limeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wageni wengi kutokana na uwepo wa maudhui ya picha na video za vivutio mbalimbali vya Utalii, madini ya thamani na vito mbalimbali ikiwepo Tanzanite, historia na utamaduni wa Tanzania, mazao ya kilimo, Miradi ya maendeleo, fursa za uwekezaji na ufundishaji wa maneno ya Kiswahili kwa wageni wanaotembelea banda hilo.
Akizungumza nchini Dubai leo mara baada ya kutembelea Banda la Tanzania katika Maonesho Makubwa ya Dunia Expo 2020 Dubai, Dkt. Ndumbaro amesema muonekano wa kipekee (Branding) uliopo katika Banda la Tanzania ni mkakati wa kuinadi Tanzania katika fursa za Uwekezaji, Kilimo, Utalii, Viwanda na Biashara
''Mimi na Mawaziri wenzangu tumekuja kuongeza nguvu kuhakikisha fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania zinajulikana dunia kote ambapo katika maonesho hayo zaidi ya nchi 192 zinashirikia hivyo ni fursa kwetu kama nchi kunadi utajiri wetu ili kuvutia Wawekezaji'' alisisitiza Dkt. Ndumbaro
Dkt. Ndumbaro amesema picha na maudhui ya video za vivutio vya utalii viilivyopo katika banda hilo vimekuwa chachu kwa wageni kuendelea kumiminika kutembelea banda hilo.
“Hii inaonesha jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuimarisha Diplomasia ya uchumi kwa kutangaza fursa za uwekezaji katika nyanja mbalimbali imeongeza muitikio chanya kwa wageni kuja na wanapofika hapa wana vitu mbalimbali vya kuona katika banda letu ambalo lina upekee na picha zenye uhalisia’’ amefafanua Dkt. Ndumbaro .
Katika hatua nyingine, Dkt. Ndumbaro amesema Tanzania imejipanga kutumia vyema ushiriki katika jukwaa hilo ambapo tarehe 27 mwezi huu ni Siku ya Tanzania ( Tanzania Day) katika Maonesho hayo, Hivyo imejipanga kuinadi Tanzania katika sekta ya Utalii kwa mafanikio makubwa ambapo Mgeni rasmi atakuwa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan
Kufuatia uwepo wa Siku hiyo, Diaspora, Wafanyabiashara wakubwa, Mabalozi kutoka nachi mbalimbali na Wadau wa utalii kutoka kona mbalilmbali za dunia watashiriki katika Siku hiyo ya Tanzania kwa lengo kuwashawishi Wawekezaji kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali.
Katika maonesho hayo Mawaziri wengine waliowasili nchi Dubai kwa ajili ya kunadi fursa za uwekeaji zilizopo Tanzania ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Ashatu Kijaji pamoja na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe pamoja na viongozi wenginne wakiwemo Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Uwekezaji pamoja na Madini
Miongoni mwa taasisi za Tanzania zinazoshiriki maonyesho hayo ni pamoja na Mamlaka ya maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Wakala wa Huduma za Misitu Tazania (TFS).
Taasisi nyingine ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Shirika la Biashara la Zanzibar (ZSTC) pamoja na Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania uliopo Abu Dhabi na Ofisi ya Ubalozi Mdogo wa Dubai katika nchi ya Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu.
Maonesho hayo ya kimataifa yaliyoanza tarehe 01 oktoba, 2021 yanaendelea hadi tarehe 31 Machi, 2022.