HALMASHAURI TENGENI FEDHA ZA LISHE
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (aliyekaa katikati) akiwa na Wakuu za Wilaya Sumbawanga Sebastian Waryuba (kulia) pamoja na Kaimu Katibu Tawala Mkoa Dkt. Boniface Kasululu (kushoto). Waliosimama kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Tano Mwera na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijuakali mara baada ya kikao cha tathmini ya lishe mkoa.
Na .OMM Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
Joseph Mkirikiti amezionya halmashauri za mkoa huo kwa kutokutoa fedha za
utekelezaji wa afua za lishe katika kipindi cha Octoba hadi Desemba 2021.
Ametoa onyo hilo jana
(25.02.2022) wakati akiongoza kikao cha tathmini ya mkataba wa shughuli za
lishe kipindi cha Julai hadi Desemba 2012 kilichofanyika mjini Sumbawanga
ambapo halmashauri zote nne ziliripotiwa kutoa fedha za lishe asilimia 17.5 tu
hatua inayokwamisha shughuli za lishe.
“Leo ndio siku ya mwisho
nisisikie kuwa Afisa Lishe anasema hajapewa fedha za kutekeleza shughuli wakati
mkoa bado una tatizo la udumavu na utapiamlo
Wakurugenzi nendeni mkabadilike
.Suala la lishe ni agenda muhimu kwa uhai wa watu wetu” alisisitiza Mkirikiti.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa
Rukwa Dkt. Bonoface Kasululu ilionyesha kuwa halmashauri za Sumbawanga
Manispaa, Sumbawanga Vijijini, Nkasi na Kalambo zimetoa asilimia 17 na
kupelekea mkoa uwe kwenye rangi nyekundu.
Dkt. Kasululu aliongeza
kusema matokeo ya ujumla yanaonesha kuwa mkoa wa Rukwa una wastani wa alama
asilimia 87 ambapo kiasi hicho kimechangiwa na kutokutolewa kwa fedha za afua
za lishe kwa upande wa halmashauri.
“Asilimia ya bajeti ya halmashauri iliyotumika kutekeleza shughuli za lishe kati ya iliyotengwa rangi nyekundu ni asilimia 17.5 kiashiria hiki kinaendelea kufanya vibaya zaidi
ikilinganishwa na matokeo ya asilimia 54 kipidi cha mwaka 2020/2021” alieleza Dkt. Kasululu.
Taarifa ya tathmini kwa
kiashiria cha asilimia ya fedha zilizotumika kwa shughuli za lishe katika
kipindi cha Julai hadi Desemba 2021 kwenye halmashauri na asilimia zake kwenye
mabano Manispaa ya Sumbawanga (0.0), Sumbawanga DC (18.9), Nkasi DC (0.0) na
Kalambo DC (47.7) hatua inayofanya mkoa kuwa na jumla ya asilimia 17.5
Mmoja wa Maafisa Lishe
toka Halmashauri ambaye hatuka jina litajwe alisema “tumekuwa tukiandika
madokezo kuomba fedha za shughuli za lishe lakini hatupatiwi bila kupewa
sababu. Octoba –Desemba 2021 niliomba
shilingi 800,000 lakini hadi leo sijajibiwa na kazi zimesimama” alisema mtaalam
huyo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Jukwaa la Lishe Tanzania (PANITA) Aron Isaack alisema licha ya mkoa wa Rukwa kushika nafasi ya 13 kati 26 mwaka
2020/21 bado kuna
changamoto kubwa ya shughuli za lishe kutopewa kipaumbele hatua inayosababisha
utapiamlo na udumavu kuendelea.
Isaack aliongeza kuwa
kunahitajika utashi wa kisiasa ili kutekelezwa kwa mkataba wa lishe miongoni
mwa viongozi na watendaji wa serikali wakiwemo Waganga Wakuu wa Wilaya za
Rukwa.
“Tunaishukuru serikali kwa
kusimamia suala la lishe hasa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020
iliyotamka suala la lishe kupewa kipaumbele “alisema Isaack.
Kwa mujibu wa taarifa ya
lishe iliyotolewa na Wizara ya Kilimo Desemba 2020 ilionesha kuwa mikoa
inayoongoza kwa uzalishaji mazao ya chakula ndio ina kiwango kikubwa cha
udumavu unaotokana na utapiamlo ikiwemo Rukwa (47.9), Njombe (53.6) na Iringa
(47.1).
Mwisho.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu akitoa taarifa ya hali ya lishe jana kwenye kikao cha tahmnini mjini Sumbawanga ambapo wito ulitolewa kwa halmashauri kutoa fedha kutekeleza afua za lishe
Sehemu ya Maafisa Lishe wa Halmashauri wakiwa kwenye kikao cha tathmini ambapo walieleza kutopata fedha kutekeleza afua za lishe kutoka halmashauri kipindi cha Julai hadi Desemba 2021.