SERIKALI YAFUTA TOZO 42 ZAO LA KAHAWA-MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametangaza uamuzi wa Serikali wa kuondoa tozo 42 kati ya 47 ambazo walikuwa wanatozwa wakulima wa kahawa wa Mkoa wa Kagera hadi kufikia tozo 5 tu ambazo itakuwa ni jumla ya Shilingi 267 kwa kila kilo ya kahawa, kutoka Shilingi 830 za awali.
Waziri Mkuu ametoa maamuzi hayo kufuatia tume maalum aliyoiunda ili kupitia utaratibu na mfumo wa uendeshaji wa vyama vya Ushirika wa zao la kahawa Mkoani Kagera.
Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza viongozi wa vyama vya Ushirika, wasimamie vyama vyao kwa uaminifu na weledi ili vilete tija kwa wakulima.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewata viongozi wa vyama vikuu vya ushirika kuacha tabia ya kukopa pesa benki kwa ajili ya kununua kahawa kwa wakulima.
Waziri Mkuu ameyatoa maagizo hayo leo (Jumanne, Machi 29, 2022) Wakati alipoendesha Mkutano Maalum wa Wadau wa zao la kahawa mkoani Kagera uliofanyika wilayani Karagwe Mkoa wa Kagera.
Amesema kuanzia sasa mauzo ya kahawa katika Mkoa wa Kagera yatafanyika kwa njia ya mnada. “Mnada huo utafanyika kwenye ngazi ya vyama vya msingi.”
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema baadhi ya vyama vya ushirika vimekuwa vikiwaumiza wakulima wa kahawa kwa kuwaongezea tozo zisizokuwa na tija.
Amesema jambo hilo linafanyiwa kazi kwani wakulima wa kahawa mkoani Kagera wamekuwa wakilia na tozo kubwa zaidi ya 47 na bado wamekuwa wakicheleweshewa malipo.
Waziri huyo amemuagiza Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa kugawa miche ya kutosha ya kahawa kwa wakulima ili ilete tija na kuwaongezea kipato.
Amesema ili kuhakikisha maafisa ugani wanatekeleza majukumu yao ipasavyo Wizara imeandaa utaratibu wa kutoa usafiri pamoja na vifaa vya kupimia udongo.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora alisema katika msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022 mkoa ulizalisha jumla ya tani 52,000 za kahawa ya maganda iliyokuwa na thamani ya sh. bilioni 69.
"Bei ya kahawa imeendelea kuimarika kwani katika msimu huu wakulimwa walilipwa shilingi elfu 1,300 kwa kilo moja ya kahawa ya maganda na Shilingi elfu 3,300 kwa kilo moja ya kahawa hai (Organic cofee)."
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa alisema kutokana na usimamizi mzuri wa Serikali ya awamu ya sita katika zao la kahawa, tayari wakulima wemeanza kuona manufaa kwani bei ya zao hilo imepanda.
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Tume Maalumu ya kuchunguza mwenendo wa zao hilo. Dkt. Fabian Magawa Madele, alisema katika uchunguzi waligundua ubadhirifu wa zaidi ya shilingi bilioni saba ambazo zilitumika nje ya utaratibu wa vyama vya Ushirika.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MACHI 29, 2022.