NMB KUTOA MKOPO WA BIL 200 KWA WANAFUNZI ELIMU YA JUU-WAZIRI MKENDA
Na
Mathias canal, WEST-Dar es salaam
Wanafunzi wamepata ahueni
baada ya Benki ya NMB katika mwaka wa fedha 2022/2023 kutenga Bilioni 200 kwa
ajili ya kutoa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 9 kwa wanafunzi wa Elimu ya
Juu.
Mikopo hiyo itatolewa kwa
wazazi na walezi ambao ni waajiriwa wa serikali na sekta binafsi au
wafananyakazi wanaotaka kujiendeleza.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 11 Julai 2022 wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi Ruth
Zaipuna ofisini kwake Jijini Dar es salaam.
Waziri Mkenda amesema kuwa mikopo
hiyo itasaidia kupunguza idadi ya waajiriwa wanaowaombea watoto wao mikopo
kwenye Bodi ya mikopo ya Elimu ya juu (HESLB) na hivyo kutoa fursa kwa waombaji
wenye uhitaji zaidi.
“Naipongeza Benki ya NMB kuwa
mstari wa mbele kuinua sekta ya elimu nchini kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa
elimu ya juu na pia kutoa ufadhili kwa watoto wanaotoka kwenye familia zenye uhitaji” Amekaririwa Waziri Mkenda
Ameongeza kuwa serikali
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan
inaendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya kugharamia elimu ya juu ili kuendana
na mahitaji yanayotokana na ongezeko kubwa la uhitaji wa mikopo kwa wanafunzi
wa Elimu ya juu.
Kwa upande wake Afisa
Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi Ruth Zaipuna amesema kuwa, hivi karibuni Benki
hiyo ilizindua “Nuru Yangu Scholaship and Mentorship Program” kwa ajili ya
kusaidia elimu nchini kwa lengo la kukata mnyororo wa umasikini na kuendeleza
kizazi kijacho cha viongozi kwa kutumia njia ya kuongeza idadi ya wanafunzi
wanaojiunga na Elimu ya Juu.
Amesisitiza kuwa kupitia
Programu hiyo wanafunzi watalipiwa kila kitu ikiwemo ada, fedha za kujikimu,
fedha za mafunzo kwa vitendo, Bima ya afya, na Kompyuta mpakato.
Bi Zaipuna amesema kuwa
utoaji wa mikopo hiyo ya Bilioni 200 ni utekelezaji wa ahadi waliyoitoa ambayo
waliahidi kuanza mchakato wa kutoa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 9.
MWISHO