SERIKALI KUHAKIKI WASTAAFU KIDIJITALI
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu
swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Nachingwea, Mhe. Amandus Julius
Chinguile aliyehoji sababu za Serikali kutoweka utaratibu wa Wastaafu
kuhakikiwa kwenye Halmashauri au Kata badala ya utaratibu wa sasa wa
kuhakikiwa mikoani.
Mwisho
Serikali inatengeneza mfumo wa kidigitali
utakaowawezesha Wastaafu kujihakiki wenyewe (Self verification) kupitia
simu zao za mkononi au kwa kutumia huduma za kibenki ili kuwapunguzia
Wastaafu gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kwenda
kuhakikiwa.
Hayo
yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad
Hassan Chande, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea, Mhe.
Amandus Julius Chinguile, aliyehoji kwa nini Serikali isiweke utaratibu
wa Wastaafu kuhakikiwa kwenye Halmashauri au Kata badala ya utaratibu wa
sasa wa kuhakikiwa Mikoani.
Mhe.
Chande alisema uhakiki wa wastaafu wanaolipwa na Hazina umekuwa
ukifanyika katika ngazi ya Halmashauri, hata hivyo, ili kuwapunguzia
Wastaafu gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kwenda kuhakikiwa,
Serikali inatengeneza mfumo wa kidigitali utakaowawezesha Wastaafu
kujihakiki wenyewe.
Alisema
baada ya kukamilika kwa taratibu zote, Wastaafu watapewa elimu ya jinsi
ya kujihakiki wenyewe na watatangaziwa siku ya kuanza kujihakiki.
Katika
hatua nyengine, Mhe. Chande aliliambia Bunge kuwa Serikali inatambua
umuhimu wa kuimarisha uchumi wa maeneo yote ya nchi ili kuweka mazingira
yatakayovutia benki na taasisi za fedha kuanzisha huduma za kibenki
katika maeneo mbalimbali nchini.
Alitoa
maelezo hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Wingwi, Mhe. Omar
Issa Kombo, aliyetaka kujua wakati ambao Serikali itajenga Benki za NMB
na CRDB kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Micheweni.
Mhe.
Chande alisema kuwa uamuzi wa kufungua matawi ya benki hufanywa na
benki yenyewe ambapo kabla ya kufanya uamuzi huo, benki hufanya upembuzi
yakinifu ukiwa na lengo la kuangalia kama kuna uwepo wa biashara ya
kutosha ambayo italetea faida.
“Mabenki
yakishafanya upembuzi yakinifu katika sehemu husika huwasilisha
uamuzi/pendekezo lao Benki Kuu ya Tanzania”, alisema Mhe. Chande.
Aliongeza
kuwa Serikali kupitia Benki Kuu haina kizuizi chochote katika suala la
mabenki kufungua matawi, kama benki husika itatimiza masharti yote ya
kufungua matawi kama yalivyoainishwa katika kanuni namba 31 ya Kanuni za
Utoaji Leseni za Mabenki na Taasisi za Fedha za Mwaka 2014.
Mhe.
Chande alibainisha kuwa Benki za NMB na CRDB hazina matawi kwenye Makao
Makuu ya Wilaya ya Micheweni lakini , wananchi wa Wilaya ya Micheweni
wanapata huduma za kibenki kutoka benki za CRDB na NMB kupitia mawakala
wa benki, ambapo hadi kufikia Oktoba 2024, kulikuwa na jumla ya mawakala
4 wa Benki ya CRDB na 14 wa Benki ya NMB wanaotoa huduma za kibenki
katika Wilaya hiyo.